Serikali yatoa mitungi ya gesi 700 kwa wajasiriamali Mwanza

Na Mariam John
29 Mar 2023
Hakuna tena kupikia kuni na mkaa ni mwendo wa gesi.
article
  • Mitungi hiyo itasaidia kuinua uchumi wa wajasiriamali mkoani Mwanza.
  • Itaongeza uhamasishaji wa kutunza mazingira.

Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya Oryx imetoa mitungi 700 kwa wajasiriamali kutoka wilaya tano za Mkoa wa Mwanza ili kusaidia katika kulinda na kutunza mazingira.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja ametoa kiasi cha Sh21 milioni kwa wajasiriamali hao zitakazowasaidia kujaza gesi pindi itakapoisha kwa awamu ya kwanza.

Akizungumza kwenye mafunzo kwa wajasiriamali kuhusu matumizi sahihi ya mitungi ya gesi, Msanja amesema itasaidia kuokoa na kuhifadhi miti ambayo inaharibiwa kwa ajili ya kupata nishati ya kupikia.

“Pia tunakosa hewa ya safi na ya kutosha, hivyo kupitia kampeni hii ya hifadhi mazingira kwa kupikia nishati safi akina mama wataweza kuepuka moshi ambao una madhara kwenye mapafu,” amesema Masanja.

Ametaja faida za kupikia nishati ya gesi kuwa ni kuokoa muda wa kupika lakini pia kurahisisha shughuli ndogo ndogo za ujasiriamali kufanyika kwa haraka.

“Hata kama baba amerudi usiku wa manane na anataka chakula cha moto kazi yako wewe ni kuswichi na  mambo yanaenda mubashara,” amesema Masanja.

Mbali na utunzwaji wa mazingira majiko ya gesi yatasaidia kuokoa muda uliokuwa unatumiwa na wafanya biashara mkoani Mwanza kutafuta kuni na mkaa.Picha|Innerself.com.

Awali akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Oryx, Benoit Abaman amesema lengo kuu la kutoa mitungi hiyo ni kulinda mazingira ili wananchi wasiendelee kukata miti hovyo.

Amesema lengo lingine ni kuboresha maisha ya wanawake na watoto waweze kwenda shule badala ya kwenda kuokota kuni msituni kwa ajili kupikia.

Hata hivyo, baadhi ya wajasirimali waliozungumza na JikoPoint (www.jikopoint.co.tz) wamesema  mitungi hiyo si tu itapunguza muda wa kupika lakini pia ni kichocheo cha uchumi wao.

“Tumefurahi kunufaika na mitungi hii ya gesi kwani itatusaidia kuinuka kiuchumi kwa sasa hakuna tena kupikia kuni na mkaa ni mwendo wa gesi,” amesema Dotto Lugwisha, mkazi wa Misungwi.

Mnufaika mwingine, Delina Malale mkazi wa Mbarika wilayani Misungwi amesema mitungi hiyo imekuja wakati mwafaka hasa kipindi hiki ambapo bei ya mkaa iko juu.

Kwa sasa, gunia moja la mkaa mkoani Mwanza linauzwa kwa Sh80,000 wakati huo kununua mtungi mdogo wa kilo sita ni Sh55,000 huku ukiisha kwenda kujazwa utagharibu kiasi cha Sh24,000.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa