Serikali yaweka mikakati kuwainua mama, baba lishe Tanzania

Na Lucy Samson
21 Apr 2026
Kaulimbiu ya kongamano hilo ni Shiriki kulinda amani na mshikamano wa taifa, amani ni hazina yetu, mama na baba lishe.
article
  • Ni pamoja na kuwapa elimu na ujuzi utakao wasaidia kuboresha kazi zao.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema inaendelea kuweka mikakati mahususi ya urasimishaji na uwezeshaji wa biashara ndogo ndogo ikiwemo kundi la mama na baba lishe ili wawe sehemu ya utekelezaji wa dira ya 2050.

Ahadi hiyo imetolewa na Rais Samia Suluhu aliyekuwa akizungumza leo katika kongamano la Umoja wa Mama Lishe (UMALITA) lililofanyika jijini Dar es Salaam leo Aprili 21, 2026 akikisistiza kuwa kundi hilo ni miongoni mwa sehemu muhimu nchini likiwezesha makundi mbalimbali ya Watanzania kufanya kazi zao.

Hii ni mara ya kwanza kwa kundi hilo kukutana na Rais Samia baada ya uzinduzi wa mkakati wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia (2024 2034) ukiliolilenga zaidi kundi hilo ili kuboresha mazingira yao ya kazi kwa kuhamia katika nishati safi ya kupikia.

Pamoja na mkakati huo kuendelea kupiga hatua bado kundi hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kunyanyaswa na kusumbuliwa ambapo Rais Samia ametaka zikomeshwe haraka.

Awali, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mama na Baba Lishe Tanzania (Umalita), Julieth Malata, ameeleza kuwa, ukosefu wa mitaji na miundombinu mibovu ni vikwazo vikuu vinavyokwamisha ustawi wa sekta hiyo nchini.

Malita ameongeza kuwa upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu bado ni kitendawili, hali inayowafanya wengi kushindwa kuendeleza biashara zao na kubaki katika lindi la umaskini licha ya mchango wao mkubwa katika uchumi wa nchi.

Aidha, amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan, kusaidia kutatua changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo, ikiwemo unyanyasaji kutoka kwa baadhi ya askari mgambo wakati wa kutoa huduma.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa