Mauzo ya nyama nje ya nchi yameongezeka kwa asilimia 22.3 na kuiingizia Tanzania Sh142.7 bilioni suala linalotajwa kuendelea kukuza pato la Taifa.
Dk Bashiru Ally aliyekuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mei 15, 2026 alisema kuongezeka kwa mauzo hayo ni jitihada za Serikali kuendeleza mahusiano ya kidiplomasia nje ya nchi.
“Mheshimiwa Spika, kuendelea kuongezeka kwa mauzo ya nyama nje ya nchi ni matokeo ya hatua zilizochukuliwa na Serikali ya awamu ya sita kwa kuongeza ushirikiano na mahusiano ya kidiplomasia yaliyosababisha kufunguka kwa fursa za kibiashara nje ya nchi,”
Kwa mujibu wa wizara hiyo, hadi kufikia Aprili 2026, jumla ya tani milioni 12.8 za nyama zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 54.7 (Sh142.7 bilioni) zimeuzwa nje ya nchi.
Kiwango hico kimepaa kwa asilimia 22.3 ikilinganishwa na tani milioni 9.9 zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 40.3 (sawa na Sh105.5 milioni) zilizouzwa kaatika masoko mbalimbali kipindi kama hicho katika mwaka wa fedha wa 2024/2025.
Kiasi hicho kinajumuisha tani 8,228 za nyama ya mbuzi, tani 3,787 za nyama ya kondoo, tani 675 za nyama ya ng’ombe, tani 38 za nyama ya nguruwe na tani 33 za nyama ya kuku.
Nyama hizo kutoka Tanzania imeuzwa kwenye masoko ya nchi za Bahrain, Comoro, Hong Kong, Kenya, Kuwait, Oman, Qatar, Saudi Arabia, Ushelisheli, Umoja wa Falme za Kiarabu na Vietnam.