Utafiti nishati safi ya kupikia kufanyika Tanzania

Na Lucy Samson
3 Nov 2022
Utasaidia kupata uhalisia wa matumizi ya nishati hizo na athari zitokanazo na matumizi ya nishati chafu ikiwemo kuni.
article
  • Wizara yake itafanya utafiti wa kina ndani ya miezi mitatu.
  • REA kusambaza nishati safi vijijini ndani ya miezi mitatu
  • Serikali yatenga Sh23 bilioni kufanikisha usambazajii huo.

Dar es Salaam. Waziri wa Nishati January Makamba amesema utafiti wa kina kuhusu matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia nchini Tanzania unahitajika ili kupata uhalisia wa athari zitokanazo na matumizi ya nishati chafu ikiwemo kuni. 

Waziri Makamba aliyekuwa akihitimisha mjadala wa kitaifa wa nishati safi za kupikia uliofanyika kwa siku mbili Novemba 1 na 2, 2022 jijini Dar es Salaam amesema utafiti huo utasaidia kikosi kazi kilichoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kutoa mwelekeo wa  suala la nishati safi nchini.

“Kazi hii itafanyika ili tunapoliendea suala hili na kikundi kazi kitakapoanza kazi kiwe kinapata faida ya ushahidi wa kiutafiti wa takwimu siyo kubunibuni,” amesema Makamba.

Serikali imetenga fedha za kutosha za kukamilisha utatafiti huo utakaofanyika ndani ya miezi mitatu na Wizara ya Nishati.

Ukifanikiwa utaleta majibu ya kina kuhusu athari za kimazingira zinazosababishwa na matumizi ya nishati zisizo safi na uhalisia wa sababu za matumzi endelevu ya nishati hizo hususani maeneo ya vijijini.

Akihutubia washiriki wa mjadala huo wa kitaifa, Waziri Makamba amesema nishati safi ya kupikia ni moja kati ya ajenda kubwa  zinazojaadiliwa duniani kote hivyo na Tanzania itashirikiana na  wadau wa  mashirika ya maendeo kufanikisha matumizi ya nishati hizo.

Nishati safi na salama ya kupikia ni pamoja na umemejua, gesi ya majumbani (LPG) na asilia, biogesi na umeme wa kawaida. Zinatajwa kuwa ni nishati rafiki kwa mazingira. 

Majiko banifu na mkaa mbadala yanaweza kunusuru athari zitokanazo na mazingira na madharaya kiafya yatokanyo na moshi wa mkaa na kuni. Picha | Raymond/Twitter.

Mpango kabambe wa matumizi ya gesi asilia 

Wizara hiyo pia imeahidi kuandaa mpango kabambe wa matumizi ya gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na viwandani, ambayo tayari ujenzi wa mabomba yake unaendelea

Oktoba 5, 2022 Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) lilisema  limeanza mchakato wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Ntorya hadi Madimba lenye urefu wa kilomita 35.

Mradi huo unaopita kwenye vijiji 12 vilivyopo mkoani Mtwara utaongeza upatikanaji wa gesi  nchini kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo majumbani na viwandani. 

Hata hivyo, bado kuna malalamiko kwa baadhi ya wananchi wakidai mradi huo kutowanufaisha.

Akijibu malalamiko hayo, Makamba amesema wizara yake inaandaa mpango mkakati na sera juu ya matumizi ya nishati hiyo ili iweze kutumiwa na kila mwananchi.

“Mpango mkakati huo utaweka mazingira ya kutenga gesi kwa kila matumizi, matumizi ya nyumbani, viwandani na kwenye mapishi,” amesisitiza Mkamba.

Waziri wa Nishati January Makamba akijibu hoja mbalimbali kwenye mjadala wa kitaifa wa nishati safi za kupikia. Picha| Wizara ya Nishati.

Nishati safi hadi vijijini

Mkurugenzi mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi  Hassan Said amesema Sh23 bilioni  zimeshatengwa kwa ajili ya kufikisha nishati bora ya kupikia vijini ndani ya miezi mitatu ijayo.

“Pesa hizo tumezigawa katika mafungu matatu tutaanza kwenye mikoa ya majaribio Lindi na Pwani,” amesema Said.

REA itasambaza  mitungi ya gesi asilia 100,000 vijijini na majiko banifu yanayotumia majiko ya bayomasi yatakayopunguza matumizi ya kuni na mkaa kwa wananchi waishio vijijini.

“Kama ilivyoelezwa siyo rahisi watu wote kuwahamisha kutoka njia za asili ya kupikia kuwapeleka kwenye nishati bora hivyo tutaanza na majiko hayo,” amesema Mhandishi huyo aliyekuwa akizungumza na wahudhuriaji wa mjadala wa kitaifa wa nishati safi za kupikia.

Majiko yatakayosambazwa na REA ni pamoja na majiko yenye uwezo wa kubadilisha nishati  iliyopo kwenye mkaa na kuni kuwa nishati ya kupikia na kuzuia utokaji wa gesi zenye athari.

Harakati hizo za REA kuhamasisha matumizi ya nishati safi kumeibua sintofahamu kwa baadhi ya wananchi ya kwamba huenda wakashindwa kusambaza umeme katika ufanisi.

Hata hivyo Mhandisi huyo amewatoa mashaka wananchi ya kwamba usambazaji wa nishati safi vijijini utaenda sambamba na ufanisi katika usambazaji wa umeme.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa