Waathirika wa maporomoko ya tope Hanang wapewa majiko ya gesi

Na Lucy Samson
21 Dec 2024
Serikali ya Tanzania imekabidhi majiko ya gesi pamoja na nyumba 109 zilizojengwa na Serikali kwa waathirika wa mafuriko yaliyotokea katika wilaya ya Hanang mkoani Manyara.
article
  • Majaliwa asema nyumba hizo ni za kisasa hivyo ni lazima kutumia nishati safi ya kupikia.

Serikali ya Tanzania imekabidhi majiko ya gesi pamoja na nyumba 109 zilizojengwa na Serikali kwa waathirika wa mafuriko yaliyotokea katika wilaya ya Hanang mkoani Manyara.

Hayo yamejiri ikiwa ni mwaka mmoja tangu kutokea kwa tukio hilo la kuporomoka kwa matope na mawe kutoka mlima Hanang Disemba 3, 2023 na kusababisha vifo vya watu 89 na majeruhi 139.

Mbali na vifo maporomoko hayo yalisababisha nyumba zaidi ya 150, mashamba na miundombinu ya barabara katika wilaya ya Hanang kuharibika huku familia 500 zilipoteza makazi yao.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa aliyekuwa akizungumza katika hafla ya kukabidhi nyumba hizo Disemba 21, 2024 amesisitiza utunzaji wa mazingira unaoenda sambamba na matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Tunataka sasa muanze kutumia nishati safi ya kupikia leo hii kutakuwa na zoezi La kukabidhi mitungi ya gesi kuanze kupikia majiko ya gesi moja kwa moja…

…Msianze na kuni, hizi nyumba ni za gesi kwa hiyo mnaanza kupika kwa nishati safi ya kupikia,”amesema Majaliwa.

Muonekano wa nyumba mpya zilizojengwa na Serikali kwa ajili ya waathirika wa maporomoko ya tope Hanang.

Kwa mujibu wa Majaliwa nyumba hizo 109 zitakuwa na ukubwa wa mita za mraba 29 na vyumba vitatu vya kulala, sebule, jiko, bafu na choo pamoja na  miundombinu ya maji, umeme  hivyo kuwezesha jumla ya wakazi  745 kuishi katika mji huo.

Mbali na ugawaji wa majiko hayo ya gesi majaliwa amesema watagawa miti ya 600 ya matunda na mingine 4,256 ikijumuisha ya matunda, kivuli na mbao itakayopandwa na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na halmashauri ya wilaya hiyo na Shirika la Save the Children.

Kutolewa kwa majiko hayo kwa waathirika wa maporomoko ya matope Hanang kutasaidia kulinda afya za watumiaji pamoja mazingira.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa