Wabunifu wanavyochagiza matumizi majiko banifu

Na Mariam John
3 Jun 2022
Viwanda vya kutengeneza majiko hayo vyazidi kuongezeka. Taasisi mbalimbali zajitokeza kuyatumia. Huenda kasi ya matumizi ya nishati mbadala ya kupikia kwenye shughuli za watu wengi ikiwemo sherehe, misiba au taasisi za shule na vyuo yakaongezeka baada ya kubuniwa kwa majiko banifu yanayokidhi mahitaji ya kada hizo. Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) Mkoa wa Mwanza […]
article
  • Viwanda vya kutengeneza majiko hayo vyazidi kuongezeka.
  • Taasisi mbalimbali zajitokeza kuyatumia.

Huenda kasi ya matumizi ya nishati mbadala ya kupikia kwenye shughuli za watu wengi ikiwemo sherehe, misiba au taasisi za shule na vyuo yakaongezeka baada ya kubuniwa kwa majiko banifu yanayokidhi mahitaji ya kada hizo.

Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) Mkoa wa Mwanza limewawezesha wajasiriamali mkoani humo kuanzisha viwanda vya kutengeneza majiko banifu yanayokidhi mahitaji ya taasisi mbalimbali. 

Majiko hayo banifu ni yale yanayotumia nishati ya kuni na mkaa. Mengine yanayotumia gesi ya majumbani ambayo ni miongoni mwa nishati safi na salama zinazopendekezwa na wadau wa utunzaji wa mazingira.

Donald Baraka, fundi wa kutengeneza majiko ya gesi kutoka kampuni ya Domado Victoria Work iliyopo Sido Mkoa wa Mwanza amesema ameamua kutengeneza majiko hayo na kuyauza kama jitihada za kupunguza tatizo la ukataji miti kwa sababu yanatumia kiasi kidogo cha kuni na mkaa. 

“Na haya siyo majiko pekee tu kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, pia tunatengeneza majiko yanayotumia gesi ambayo yanaweza kutumika kupikia chakula mashuleni, kwenye shughuli mbalimbali za kijamii na hata mahotelini, dhima yetu ni kupunguza matumizi makubwa ya mkaa na kuni kwenye maeneo hayo,” anasema Baraka mwenye uzoefu wa takriban miaka mitatu. 

Kwa mjibu wa fundi huyo majiko wanayotengeneza hayatumii gesi nyingi kama yalivyo ya kisasa na kwamba mtungi mdogo wa wenye ujazo wa lita 14.5 unatumika kwa miezi mitatu hadi minne kwa matumizi ya kawaida ya familia ndogo huku anayetumia kwa matumizi makubwa, gesi hukaa hadi siku tatu.

“Na hawa ni kama wale wanaofanya wanaooka mikate au keki, watu wa mahotelini na shuleni hali inayopunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya mkaa na kuni,” anasema Baraka.

Mbali na majiko hayo, kampuni hiyo pia inatengeneza vifaa vingine kama mashine za kukaanga karanga, majiko ya kuoka mikate na keki.

Moja ya jiko banifu linalotumia mishati ya gesi ya majumbani linalotengenezwa na wajasiriamali mkoani Mwanza. Picha| Mariam John.

Vifaa vinavyotumika kuunda majiko hayo

Ili jiko hilo likamilike na kuanza kutumika vipo vifaa ambavyo vinahitajika katika kuliunda ambavyo ni banner, sahani nzito za milimita 1-2, valvu, udongo  pamoja na nondo.

“Tunalazimika kuweka udongo ili kusaidia jiko hilo kutunza joto, na kwamba jiko hili ni imara na linadumu kwa muda mrefu,” anasema Baraka na kueleza kuwa wanapata oda za kutengeneza majiko hayo kutoka taasisi mbalimbali.

Gharama za majiko haya

Dominic Manchale ni Mkurugenzi wa shirika la Domado mkoani Mwanza anasema majiko hayo hutengenezwa kwa uzito tofauti kuanzia jiko la sufuria la kilo 25 hadi kilo 100 na inategemea na aina ya jiko ambalo mteja anahitaji.

Watu wanaouziwa majiko hayo hutengenezewa na masufuria kulingana na ukubwa wa majiko ili wasipate shida wakati wa kutumia.

“Tunatengeneza sufuria na jiko kuanzia saizi ya kilo 25 hadi kilo 100 ambapo gharama zake ni kwa sufuria ya kilo 25 pamoja na jiko lake huuzwa kuanzia Sh1.6 milioni huku jiko la sufuria ya kilo 100 ni Sh2 milioni,” anasema Manchale.

Majiko hayo hutumika kawaida kama majiko mengine ya gesi na wakati wa kununua, wateja huelekezwa namna ya kuunganisha na mtungi wa gesi, kuwasha lakini pia hupewa warantii ya matumizi.

“Mteja anapewa warantii ya jiko hilo na likiharibika kabla muda uliowekwa hapo kuisha mteja anaruhusiwa kurudisha kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho ingawa toka tuanze kuuza hatujapata tatizo la aina yoyote,” amesema Manchale

Sifa ya majiko hayo hayatumii moto mkubwa ambao unaweza kumsumbua mpishi na kwamba gesi yake haiishi haraka kama yalivyo majiko ya kisasa kwa hutengenezwa kwa kutumia vifaa vya chuma ambavyo kuharibika inachukua muda mrefu kuanzia miaka 10 na kuendelea. 

Ikiwa taasisi za umma na binafsi zitaongeza kasi ya matumizi majiko banifu itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matumizi ya kuni na mkaa na kuchagiza nishati na salama itakayosaidia kutunza mazingira na kuifanya dunia kuwa sehemu nzuri ya kuishi.

Majiko banifu husaidia kupunguza matumizi ya mkaa na kuni na hivyo kupungua pia kasi ya ukataji wa miti ili kuhifadhi mazingira. Picha| Mariam John.
© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa