Zaidi ya Sh647 bilioni kumaliza tatizo la umeme Bukoba

Na Lucy Samson
16 Mar 2023
Mradi huo utakapokamilika utawahudumia wakazi 210,000, viwanda vidogo na vya kati pamoja na migodi ya madini kwenye maeneo hayo.
article
  • Changamoto hiyo ya umeme imedumu kwa zaidi ya miaka 10.
  • Waziri Nchemba asema mkopo huo utafufua matumaini mapya kwenye sekta ya madini na uvuvi.
  • Mkopo huo pia utaboresha shule, barabara na afya.

Wafanyabiashara na wakazi wa Mji wa Bukoba mkoani Kagera huenda wakaondokana na changamoto ya kukosa umeme wa uhakika katika maeneo yao baada ya kupatikana kwa fedha za kumaliza tatizo hilo. 

Fedha hizo ni mkopo wa Sh647.5 bilioni kwa ajili ya kufadhili mradi wa umeme wa maji wa Kakono mkoani humo.

Mkopo huo wenye masharti nafuu uliotolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa  (AFD) utatatua changamoto ya umeme iliyodumu kwa zaidi ya miaka 10 kwenye mji huo uliopo Kanda ya Ziwa.

Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu  Nchemba aliyekuwa akizungumza Machi 15, 2023 baada ya kusaini mikataba hiyo amesema  mkopo huo utafufua matumaini mapya kwenye sekta ya madini na uvuvi wa samaki zenye umuhimu mkubwa nchini.

“Kanda ya Ziwa ni eneo lenye tija kubwa katika uzalishaji wa madini na samaki wanaouzwa nje, ambapo uhitaji wa nishati ya umeme kwa gharama nafuu na wa uhakika ni muhimu.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (watatu kulia), akiwa kwenye picha ya pamoja na Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Patricia Laverley  (katikati), Naibu Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Bw. Axel-David Guillon (wa tatu kushoto) na viongozi wengine mara baada ya kusaini mkopo wa Sh647 bilioni.

Kanda ya Ziwa imekuwa na sifa ya matumizi ya mitambo ya kutumia nishati ya dizeli ambayo ni gharama kubwa kuiendesha na kusababisha wakai hao kutokuwa na umeme wa uhakika na wa kutosha,” amesema Waziri Nchemba.

Utekelezaji wa mradi huo utakamilika ndani ya miaka mitano na utahusisha ujenzi wa mtambo wa kufua umeme wa megawati 87.8.

Kazi nyingine ni ujenzi wa shule ya msingi na kituo cha afya pamoja na barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 28 na hivyo kuboresha hali ya maisha ya jamii ya kanda hiyo.

Meneja Mkazi wa AfDB, Dk Patricia Larveley amesema kuwa mradi huo utakapokamilika unatarajia kuwahudumia wakazi 210,000, viwanda vidogo na vya kati pamoja na migodi ya madini eneo la Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati) na Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Patricia N. Laverley  (kushoto) wakionesha Hati za Mkataba wenye thamani ya dola ya Marekani 161.47 (sawa na shilingi 374.9 bilioni), kwa ajili ya mradi wa Umeme wa maji wa Kakono.

Pia mradi huo utachangia kuwapatia watu nishati bora na ya uhakika pamoja na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa ambayo ina athari kwa mazingira.

“Faida za kiuchumi zitakazotokana na uwepo na kukamilika kwa mradi huo  ni upatikanaji wa nishati yenye gharama nafuu, uboreshwaji wa maisha ya wakazi wa Kagera, mambo ambayo  pia  yatachangia ukuaji wa uchumi na shindani wa Taifa,” amesema Dk Laverley.

Hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo imeshuhudiwa pia na viongozi mbalimbali wakiwemo wawakilishi wa nchi na mashirika ya kimataifa, akiwemo Naibu Balozi wa Ufaransa Axel Guillon.

Viongozi wengine ni pamoja na mkuu wa Ushirikiano wa Umoja wa ulaya (EU) nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Cedric Merel, mjumbe kutoka Mradi wa Umeme Kakono na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa