Zaidi ya Sh3 bilioni kuimarisha nishati safi ya kupikia Tanzania

Na Lucy Samson
3 Feb 2023
Ruzuku hiyo itaimarisha teknolojia ya majiko banifu, gesi ya majumbani, mkaa mbadala na nishati ya mafuta itokanayo na mabaki ya mimea.
article
  • Ruzuku hiyo itachochea upatikanaji wa nishati safi ya kupikia nchini Tanzania.
  • Wanufaika waaswa kuitumia ruzuku hiyo kuwafikishia wananchi nishati safi ikiwemo gesi kwa bei nafuu.

Mfuko wa Nishati Safi ya Kupikia (CookFund) Tanzania umetoa ruzuku ya Sh3.2 bilioni kwa kampuni 16 zinazotoa huduma ya uuzaji wa nishati safi ya kupikia ili kuchochea upatikanaji wa nishati hiyo Tanzania.

Ruzuku hiyo inafadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) ikilenga kuimarisha teknolojia ya nishati  safi ya kupikia hususani gesi ya ‘mitungi’ yaani Liquified Petroleum Gas (LPG) na majiko ya umeme (EPC).

Pia ruzuku hiyo itaimarisha teknolojia ya  majiko ya mkaa banifu (ICS) mkaa tofali utokanao na vumbi la makaa ya mawe (briquettes) na nishati ya mafuta itokanayo na mabaki ya mimea (bioethanol).

Waziri wa Nishati, January Makamba(kushoto)akikabidhi mfano wa hundi ya ruzuku itakayoenda kuimaisha upatikaji wa nishati safi nchini.Picha|Wizara ya Nishati\Twitter.

Waziri wa Nishati, January Makamba aliyekuwa akizungumza katika hafla ya kuwakadihi wanufaika hundi ya ruzuku hiyo jijini Dar es Salaam Februari 2, 2023, amewasisitiza wanufaika wa ruzuku hiyo kuzitumia fedha hizo kuleta matokeo mazuri yatakayowafikia Watanzania wengi.

“Ni vyema mkahakikisha Watanzania wananufaika kweli kupitia mpango huu kwa kuwafikishia bidhaa zenu za nishati kwa bei nafuu ili waweze kuondokana na matumizi ya nishati chafu ambazo si rafiki kwa mazingira,’’ amesema Makamba.

Hafla hiyo fupi ya fupi ya kukabidhi hundi za fedha kwa wanufaika hao ilihudhuriwa na viongozi wengine akiwemo Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Manfredo Fanti, na Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF) Tanzania Peter Malika ambaye mfuko wake ndiyo unaratibu programu ya CookFund.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa