Dar es Salaam. Licha ya kwamba zaidi ya asilimia 60 ya kaya nchini Tanzania zinajihusisha na kilimo cha mazao ya chakula pamoja na biashara, bado baadhi ya kaya zimekuwa zikikumbwa na changamoto ya uhaba wa chakula unaotokana na kutokuweka akiba au kuweka akiba ndogo kuliko idadi ya wanakaya waliopo.
Serikali ya Tanzania hutafsiri kaya kama idadi ya wanafamilia ambao huishi na kula pamoja yaani hushirikiana kupata mahitaji ya kila siku, anaweza kuwa mke, mume, pamoja na watoto au mtu anayeishi peke yake na kujitegemea kwa kila kitu.
Madhara ya kutoweka akiba ya chakula huonekana zaidi pale yanapotokea majanga ya asili na kuathiri mwenendo wa mazao yaliyoko shambani kama vile ukame, mafuriko au kuchelewa kwa mvua.
Kutokana na hilo viongozi mbalimbali akiwemo Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan mara kwa mara amekuwa akitoa wito kwa Watanzania kuweka akiba ya chakula pindi wanapovuna badala ya kuuza yote kwa walanguzi.
Hata hivyo, huenda kasumba ya kutoweka akiba inatokana na ukosefu wa elimu ya kujua ni kiasi gani kinapaswa kuwekwa kama akiba kwa kila mazao kulingana na idadi ya wanakaya.
Nukta Habari imekuandalia muongozo kwa mujibu wa wataalamu wa chakula juu ya makadirio ya kiwango cha chakula kinachotumika na akiba inayopaswa kuwekwa hususan kwa mazao makuu ya chakula ambayo ni mahindi na mchele.
Ukadiriaji wa akiba ya mahindi
Mahindi ni zao kuu la chakula linalopendwa na kutumiwa na watu wengi nchini Tanzania. Picha/Nukta.
Mahindi ni zao linalolimwa katika mikoa yote ya Tanzania na uzalishaji wake ni asilimia 63 ya mazao ya nafaka na asilimia 36 ya mazao makuu ya chakula.
Utafiti unaonesha wastani wa mahitaji ya nishati kwa Mtanzania ni kilokalori 2,360, ambapo gramu 100 za unga wa dona hutoa kilokalori 363.
Hii inamaanisha kuwa mahitaji ya mtu mmoja kwa mwaka ni takriban kilo 237, sawa na magunia mawili na robo ya mahindi.
Hivyo kwa kutumia kigezo hiki mahitaji ya kaya yenye ukubwa kati ya mtu mmoja na watu watano idadi ya magunia yanayohitajika kwa mwaka, mtu mmoja anahitaji gunia tatu, watu wawili wanahitaji gunia tano, watatu gunia saba, nne gunia tisa na watu watano watahitaji gunia 12 za mahindi kwa mwaka.
Ukadiriaji wa akiba ya mpunga
Baadhi ya wakulima wakivuna mpunga. Picha/Media Wire Express.
Mpunga ni zao lingine la nafaka linalolimwa kwa wingi Tanzania na hutumiwa na watu wengi baada ya mahindi na mtama kama chakula hasa baada ya kukobolewa ili kupata mchele.
Mchele hupikwa kupata vyakula mbalimbali kama vile wali, pilau, biriani, bokoboko ,vitumbua, mikate na vyakula vingine vinavyotia nguvu mwilini.
Kwa kuwa gramu 100 za mchele hutoa kilokalori 325 hivyo, mtu mmoja kwa mwaka atahitaji kilo 265 za mchele, sawa na gunia mbili na nusu za kilo 100 kila moja.
Kilo 100 hupatikana kwa kukoboa gunia mbili za mpunga, ambazo hutoa takriban asilimia 65 ya mchele safi.Kwa mwaka, mtu mmoja anahitaji gunia tano za mpunga ambao haujakobolewa, wawili gunia 11, watatu gunia16, watu wanne wanahitaji gunia 22 na watu watano watahitaji gunia 27 za mpunga kwa mwaka.
Aidha inashauriwa kwa usimamizi bora wa akiba ya chakula, ni muhimu kuanza kwa kuweka akiba kabla ya kutumia mazao yaliyopo. Hii itahakikisha kaya ina chakula cha kutosha kwa mwaka mzima.