‘Microwave’ ni kifaa cha kisasa kinachotumika kupasha au kuivisha baadhi ya vyakula kwa kutumia teknolojia ya mionzi joto ambapo mtumiaji ndio huamua kiwango cha joto pamoja na muda kutegemeana matumizi kwa muda husika.
Kifaa hiki kimekuwa mkombozi wa wengi kutokana na ufanisi wake pamoja na kuokoa muda, kwa mfano chakula ambacho kingeweza kutumia nusu saa kuiva kwenye jiko la kawaida microwave inaweza kuivisha ndani ya dakika kumi tu au chini yake.
Hata hivyo si watu wote huwa wanazingatia usafi wa kifaa hiki muhimu, na hiyo huenda inatokana na kutokuwa na muda wa kutosha au kutojua namna bora ya kufanya usafi huo huku kifaa chako kikisalia katika ubora ule ule.
Ikiwa hufahamu jinsi ya kusafisha kifaa hicho usijali, jikopoint (www.jikopoint.co.tz) tumekuandalia mbinu rahisi za kukamilisha zoezi hilo na kukusaidia kuepukana na athari mbalimbali zinazoweza kutokana na mrundikano wa uchafu.
1.Tumia Baking soda na maji
Mara kadhaa ‘baking soda’ imekuwa ikirahisha kazi mbalimbali za nyumbani ikiwemo usafi.
Tovuti ya The Maids,inayojishughulisha na masuala ya usafi inasema kutumia mbinu hii weka kiasi kidogo cha ‘baking soda’ katika bakuli na maji,changanya kupata mchanganyiko mzito na upake katika microwave kisha uache ikae kwa dakika tano au zaidi.
Baada ya muda huo unaweza kupangusa na kitambaa kisafi au ukaosha na maji masafi na kifaa chako kitakuwa safi bila harufu mbaya.
2.Limao na maji
Limao lina msaada mkubwa katika shughuli mbalimbali za usafi mbali na kuongeza ladha katika chakula.
Ukichanganya kiasi kidogo cha maji ya limao na maji ya kawaida unaweza kurahisisha shughuli ya kusafisha ‘microwave’.
Ili kupata matokeo ya mbinu hii weka bakuli lenye mchanganyiko wa maji ya limao katika microwave kisha uwashe na uweke moto wa juu kwa dakika 10 au zaidi.
Baada ya hapo acha ipoe na uifute kwa kitambaa safi na kifaa chako kitakuwa safi tena.
3.Vinegar na maji
Watu wengi hutumia vinegar wakati wa mapishi tu, lakini tovuti ya The Kitchn wanabainisha kuwa inaweza kutumika katika shughuli za usafi hususan wa microwave.
Unachotakiwa kufanya ni kujaza maji katika bakuli (microwave safe bowl) halafu changanya na vijiko viwili vya vinegar.
Baada ya hapo weka ndani ya microwave na uweke joto la juu kwa dakika kumi au zaidi ili mvuke wa mchanganyiko huo ulainishe uchafu wote uliopo na baada ya hapo unaweza kusafisha kwa kitambaa au nguo kavu ikishapoa.
4.Maji na sabuni
Hii ni mbinu inayotumiwa na wengi lakini ni wachache wanaofanikiwa kuondoa uchafu wote unaokuwepo katika microwave.
Ili kupata matokeo bora kwanza changanya maji na sabuni ya maji katika bakuli kubwa kisha uwashe microwave kwa dakika 10 ili mchanganyiko huo upate moto na kutoa mvuke utaorahishia madoa kutoka.
Hatua hiyo ikimalizika subiri kifaa chako kipoe kisha unaweza kutumia maji hayo hayo kuendelea kusafisha kama kawaida.
Uchafu ni hatari
Kwa mujibu wa tovuti ya The Maids, uchafu unapokaa kwa muda mrefu kwenye microwave unaweza kuzalisha harufu mbaya, bakteria, na vijidudu ambavyo vinaweza kusababisha magonjwa.
“Mbali na hatari za kiafya, ‘microwave’ chafu inaweza pia kutoa harufu mbaya na hata kuwaka moto,” imebainisha tovuti hiyo.