Kutengeneza keki ni sanaa inayohitaji ustadi, uvumilivu na zaidi ya yote vifaa sahihi ili kuandaa keki nzuri yenye vipimo sahihi itakayovutia walaji
Ukizungumza na wapishi wengi wazoefu ni lazima watakwambia kuwa siri ya upishi wa keki ni vipimo sahihi pamoja na vifaa bora hivyo ikiwa wewe ni mwanafunzi au mpishi mpya wa keki vifaa vifuatavyo vitakurahishia safari yako ya maandalizi ya kitafunwa hicho kinachopendwa na wengi.
Mapishi mengi ya keki yanahitaji kuchanganya siagi na sukari ambayo inahitaji nguvu zaidi kuliko kuchanganya kwa mkono.
Katika hatua hiyo ni lazima kutumia mchapio unaoweza kuwa wa umeme au mkono, kutegemea kiwango cha keki unayoandaa.
Yanaweza kukuchosha na kukufanya utumie muda mwingi tofauti na anayetumia mashine ya umeme.
Usahihi wa vipimo ni ni muhimu sana wakati wa kuandaa keki ili uweze kupata matokeo unayotarajia.
Hivyo wakati wa kununua mahitaji usisahau vipimo ambavyo ni seti ya vijiko vya kupimia, hakikisha ina angalau 1/4 kijiko, 1/2 kijiko, 1 kijiko cha chai na kijiko kimoja cha chakula kwa vipimo, na unaweza kutengeneza karibu sahani yoyote kwa hizi nne.
Vile vile kwa seti yako ya vikombe vya kupimia, 1/4 kikombe, 1/3 kikombe, na kikombe kimoja kinahitajika .
Sinia na tray za kuokea
Keki hutengenezwa katika maumbo na ukubwa tofauti, hivyo kuwa na sinia au sufuria sahihi za kuokea ni muhimu.
Hakikisha unatumia zile zinazostahili aina ya keki unayotengeneza, iwe ni keki ya duara, mraba, au cupcakes.
Oven/ jiko la gesi
Oveni ni moyo wa utengenezaji wa keki. Hakikisha una oveni inayopasha joto kwa usahihi na kufuatilia muda wa kuoka ili kuhakikisha keki yako inawiva sawasawa.
Ikiwa hauna oveni njia mbadala unaweza kutumia jiko la gesi, au vifaa vya kisasa ikiwemo ‘pressure cooker’ ili kuandaa keki nzuri na ya kuvutia jambo la msingi ni kuelewa namna ya kukadiria moto ili usiunguze keki.
Mizani
Kupima kwa mizani ni sahihi zaidi kuliko kukadiria kwa kiasi, na kwa hivyo mapishi yote ya kitaaluma yanafanywa kwa kuzingatia wingi.
Mizani nzuri ya jikoni ni muhimu zaidi kwa wanaofanya biashara ya keki kwani wengi huwa wanauza kwa kilo hivyo ili uendane na mahitaji ya wateja ni lazima kuwa na mzani.
Bakuli kubwa
Hili ni mojawapo ya vifaa vya msingi ambavyo haviwezi kukosekana jikoni. Bakuli hizi hutumika kuchanganya viungo kwa urahisi, iwe ni unga, mayai, sukari, au siagi.
Ni vyema kuwa na bakuli za ukubwa tofauti ili kukidhi mahitaji mbalimbali ya mapishi yako.Hauhitaji bakuli za gharama ama kubwa sana, kinachohitajika ni ukubwa na umbo la bakuli.
Sahani tatu au nne za mviringo na za mstatili au mraba zitakuwa za kutosha.
Na urefu wa sentimita mbili kwa kila upande ni bora.
Kijiko cha mbao (Wooden spoon)
Kijiko kimoja cha mbao kinatosha, lakini chombo hiki cha kupikia ni muhimu sana, kwa hivyo inaweza kusaidia kuwa na vijiko kadhaa.
Vijiko vya mbao ni vigumu na huvumilia hekaheka za jikoni, hivyo vinaweza kutumika kwa aina mbalimbali za kuchanganya.
Unaweza kuvitumia hata kwa ungo mzito na mgumu zaidi.
Chujio
Unaweza kutumia chujio kwa njia nyingi tofauti, kwa wanaoka keki chujio ni muhimu zaidi kwa kuchuja viungo vikavu kama sukari au unga.
Chombo hiki pia kinaweza kusaidia kwa kuchuja viungo vilivyo na maji ama maziwa ambavyo vingeweza kupita kwenye kichujio la kawaida.
Kumbuka kuwa hivi ni vifaa vinavyohitajika wakati wa kupika keki na sio wakati wa kupamba keki. Endelea kufutilia Jiko Point kwa makala nyingine.