Faida za kutumia chungu katika mapishi

Na Herimina Mkude
6 Jan 2022
Kwa wale mliozoea sufuria, habari za matumizi ya vyungu zinaonekana kama mambo ya kale. Hata hivyo, ukweli ni kwamba vifaa hivyo vya kupikia bado ni dili mjini na vijijini. 
article

  • Husaidia kutunza virutubisho vya chakula wakati wa mapishi
  • Chakula hakipoi haraka
  • Bei yake ni ‘chee’

Huenda umezoea kutumia sufuria katika mapishi yako lakini leo, nakutambulisha chombo kingine ambacho huenda ulihisi wakati wake umepita. 

Kwa wale mliozoea sufuria, habari za matumizi ya vyungu zinaonekana kama mambo ya kale. Hata hivyo, ukweli ni kwamba vifaa hivyo vya kupikia bado ni dili mjini na vijijini. 

Hii ndiyo inanifanya niandike makala hii angalau iwafikie na hata kuwapa mwanga watoto wetu juu ya umuhimu wa vifaa hivyo vyenye jicho la kiutamaduni. 

Vyungu ni sehemu ya tamaduni za Kiafrika. Picha| Alexandra’s Africa.

Undani kuhusu chungu

Chungu ni chombo kinachotengenezwa na udongo wa mfinyanzi. Matengenzo yake huhusisha udongo na zana za upambaji huku moto ukitumika mwishoni kukipatia ukakamavu. 

Matumizi ya chungu yanabeba dhana ya utamaduni wa asili ya Kiafrika na ni moja ya urithi kutoka kwa wazee wetu wa kali. 

Hata hivyo, matumizi hayo kwa sasa yanapungua kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujio wa vifaa vya kisasa vya kupikia ikiwemo sufuria za chuma.

Mbali na utamaduni unaoambatana na chombo hicho, chungu kina faida lukuki katika mapishi na afya.

Chungu husaidia kuhifadhi virutubisho vya chakula wakati wa mapishi kuwa kuwa huivisha chakula taratibu na kwa nafasi tofauti na vyombo vingine kama sufuria, hivyo kufanya pishi lako kuwa la kiafya zaidi huku ukiwa na uhakika wa kuivisha vyema chakula chako. 

Pamoja na kuiivisha chakula taratibu, wakati chakula chako kikikaribia kuiva unaweza kuzima jiko lako kutunza nishati na kitaendelea kuchemka kwa dakika kadhaa au kuiva kwa joto la chungu hicho. 

Pia, chungu kina sifa ya kutopooza chakula mapema. Waliowahi kutumia vyungu wanafahamu hili. 

Chakula kilichopikwa kwa chungu cha ufinyanzi hupata mvuke wa madini mbalimbali ikiwemo ya chuma, ‘magnesium’ na ‘calcium’ kutokana na udongo wa mfinyanzi kuwa na utajiri wa madini hayo ambayo ni muhimu katika mwili wa binadamu.

Unaweza kupikia chakula chochote kwenye chungu. Picha| Urithi wetu Wachagga.

Gharama yake ni “Chee”

Nafahamu kuwa katika mapishi bajeti ni kitu muhimu na kwa chombo hiki, hapo ndipo mahala pake.

Tofauti na vyombo vya kupikia vya kisasa kama masufuria, chungu kinauzwa kwa bei rahisi zaidi ambapo katika baadhi ya maeneo ya mijini huanzia Sh2,000 hadi Sh3,500 inategemeana na ukubwa. Vyungu vikubwa zaidi bei yake.

Licha ya kuwa na faida nyingi chombo hiki kinahitaji umakini wakati wa kukitumia kwa kuwa ni rahisi kuvunjika.

Ni wakati wako sasa kuanza kutumia chungu katika mapishi yako ili ujionee utofauti, na ukiniuliza mimi nitakwambia chungu ni ‘mkali wao’ katika mapishi ya mboga hasa za majani.

Unaweza kuanza kujaribu kutumia chungu kwenye mapishi rahisi kama mboga za majani ya maboga yenye mchanganyiko wa karanga, halafu utupe maoni yako ni kitu gani cha utofauti umekiona na utuambie pishi gani lililopikwa kwa chungu unatamani ulionje.

Panapo majaaliwa, siku moja nitawafunza jinsi ya kupika kwa kutumia chungu.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa