Kisukari ni miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza yanayoongoza kwa kugharimu uhai wa watu kila mwaka.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mwaka 2019 watu milioni 1.5 walifariki kwa matatizo ya kisukari huku Wizara ya Afya ya Tanzania ikibainisha kuwa Watanzania milioni 2.8 wenye umri kati ya miaka 20 na 79 wanaishi na ugonjwa huo.
Hiyo ni sawa na wastani wa silimia 10.3 ya wananchi wote wa Taifa hili la Afrika Mashariki.
Katika kudhibiti ugonjwa huo, WHO inapendekeza watu kula chakula kwa mpangilio, kufanya mazoezi, kuwa na uzito wa kawaida wa mwili na kujizuia na matumizi ya pombe na bidhaa za tumbaku ikiwemo sigara.
Hata hivyo, baadhi ya watu wanafikiri ukishakuwa na kisukari basi huruhusiwi kula kila kitu jambo ambalo siyo kweli. Suala ni unakulaje vyakula hivyo?, Vifuatavyo ni vyakula ambavyo wataalamu wa afya wanashauri mtu mwenye kisukari avitumie:
Nafaka zisizokobolewa
Kwa mujibu wa jarida la afya la Hesperian, unga unaotokana na vyakula vya nafaka ambazo hazijakobolewa ni wenye afya kwa sababu nafaka hizo zinapokobolewa huondoa kiini tete na ganda la juu ambalo huwa limesheheni virutubishi.
Vyakula vya nafaka zilizokobolewa humeng’enywa kwa urahisi hivyo hutengeneza sukari haraka mwilini na vinaweza kusababisha sukari kupanda kwa haraka mpaka kufikia viwango vya hatari.
Mfano wa vyakula vya nafaka isiyokobolewa ni pamoja na ugali wa dona, ugali wa ngano, mchele na mkate wa kahawia (brown bread and rice).
Mboga za majani, matunda na vyakula vyenye nyuzi nyuzi
Mtaalam wa afya wa Zahanati ya Misigalo ya jijini Mwanza, Dk Fradius Christian anaeleza kuwa vyakula vya nyuzi nyuzi hupunguza kasi ya ufyonzaji wa sukari
“Vyakula vyenye nyuzi nyuzi ni muhimu kwa sababu husababisha mmeng’enyo wa chakula kwenda taratibu na hiyo husaidia kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu,” amesema Dk Christian.
Nyuzi nyuzi huwa ni sehemu ngumu ya mimea kama vile majani, mashina na mizizi na hupatikana katika vyakula vifuatavyo:
Unywaji mzuri wa maji
Kwa mujibu wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), zaidi ya asilimia 60 ya uzito wa mwili wa binadamu ni maji.
Maji husaidia mwili kufanya kazi mbalimbali kwa ufasaha ikiwa ni pamoja na kusaidia katika uyeyushwaji wa chakula, usafirishaji na ufyonzwaji wa virutubishi mwilini. Maji husaidia kuondoa uchafu na mabaki ya uchafu mwilini kwa njia ya jasho na mkojo.
Mzima mwenye kisukari anashauriwa kunywa maji safi na salama kiasi cha lita moja na nusu kwa siku au glasi nane kwa siku. Pia mtu mzima anaweza kuongeza kiasi cha maji kwa kunywa vitu vya maji maji kama vile supu, juisi ya matunda halisi na madafu.
Vyakula vyenye protini
Wataalamu kutoka kituo cha afya cha Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), kituo cha Afya wanasema vyakula vyenye protini husaidia kujenga mwili.
Aina hii ya vyakula ni pamoja na maharage, kunde, mbaazi, soya, karanga, njegere, njugu mawe, dengu, choroko na nyama.
Vyakula vingine ni mayai, samaki, dagaa, kumbikumbi, senene, maziwa na nzige. Vyakula hivi haviongezi sukari mwilini lakini unatakiwa kutumia kwa kiasi ili kuepuka madhara mengine ya kiafya.
Epuka vyakula vilivyochakatwa sana
Dk Christian anabainisha kuwa vyakula vilivyochakatwa viwandani huwekwa sukari nyingi au chumvi nyingi. Pia huongezwa viambata ambavyo siyo rafiki kwa afya yako hivyo ni muhimu kutumia kwa kiasi.
Vyakula hivyo ni pamoja na keki, biskuti, chokuleti, pipi, chipsi, vyakula vya kukaangwa na vinywaji kama soda, pombe na juisi kwani huongeza sukari mwilini kwa kasi.