Jiko la umeme linaloivisha chakula kwa gharama ya Sh200

Na Rodgers George
13 Oct 2021
Jiko la presha la Sescom linapika vyakula vya kuchemsha na kuroast ikiwemo wali, ugali na maharage.
article

  • Linapika vyakula vyote vinavyohusisha maji.
  • Linaivisha maharage ndani ya dakika 45 kwa gharama chini ya Sh200
  • Haliwezi kupika vyakula vya kuchoma na kukaanga.

Dar es Salaam. Hofu ya baadhi ya watu  kutumia umeme kama nishati  ya kupikia ni gharama. Kuna uwepo wa kasumba ya kuwa kutumia jiko la umeme ni gharama hivyo wengi huchagua kuendelea na matumizi ya kuni na mkaa.

Hata hivyo, kitu ambacho kasumba hiyo haizungumzii ni uwepo wa baadhi ya vifaa vya umeme ambavyo vinarahisisha upishi jikoni huku matumizi yake ya umeme ni ya kawaida. 

Vipo vingi lakini kwa leo, nakusogezea jiko la umeme aina ya Sescom ambalo unapikia chakula kwa kwa presha ambalo lina uwezo wa kuivisha maharage kwa muda usiozidi saa 1.

Jiko la Sescom limetengenezwa nchini China na kwa Tanzania, linasambazwa na Shirika la Nishati Endelevu Tanzania (Tatedo). Jiko hilo ni muunganiko wa teknolojia tatu ambazo ni jiko la umeme, kilinda joto na sufuria la presha.

Kwenye jiko hili unaweza kupika vyakula mbaimbali ikiwemo wali, kusonga ugali, rosti ya nyama na hata pilau au makande.

Hata hivyo, jiko la Sescom haliwezi kuchoma nyama au kukaanga chisi au nyama.

Kwa ufupi, linafaa kutumika kwa mapishi yanayohusisha maji.

Afisa Masoko kutoka Tatedo, Katarina Aloyce akimuelekeza mmoja wa wateja kuhusu matumizi ya jiko la Sescom ambalo ni sehemu ya nishati safi na salama ya kupikia. Picha| Rodgers George.

Utofauti na nishati nyingine

Tatedo ilifanya utafiti mwaka 2017 na 2018 ambao ulihusisha majaribio ya kupika nusu kilo ya maharage kwenye nishati mbalimbali ikiwemo mafuta ya taa, mkaa na gesi.

Kwa mujibu wa Tatedo, ilihitajika mkaa wa zaidi ya Sh1,000 kuivisha mboga hiyo huku gesi ikigharimu ShSh800 na jiko la umeme la kawaida likigharimu uniti za Sh700.

Kwa jiko la mafuta ya taa, ilihitajika Sh600 lakini kwa upande wa jiko la Sescom, lilitumia unitiza umeme zenye gharama chini ya Sh200.

Tatedo imeainisha kuwa, mballi na kutumia gharama ndogo, jiko hilo liliivisha maharage hayo kwa dakika 45. 

Jiko hilo lina ufanisi mkubwa wakati wa kupika kwa sababu linatumia umeme kidogo. Picha| Secom.

Kutoboa mifuko

Kizuri sharti kiwe na gharama lakini ni ajabu vile jiko laSescom linaweza kukuokolea gharama kwa kipindi cha muda mrefu.

Jiko hili la kisasa linaloweza kupika vyakula vyote vyenye mchuzi linauzwa kwa Sh180,000 kama bei ya rejareja.

Na unaweza kulipata kwenye kiunganishi hiki.

Unahitaji kujua kifaa gani kinaweza kufanya yale jiko la Sescom imeshindwa kufanya, endelea kufuatilia habari za Jiko News.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa