Jinsi ya kuandaa mafuta ya nazi nyumbani

Na Mlelwa Kiwale
8 Oct 2024
Mafuta ya nazi husaidia kuongeza unyevu katika ngozi huku ikisadia kupambana na chunusi na kuponya ngozi iliyoungua.
article
  • Mafuta ya nazi husaidia kuongeza unyevu katika ngozi huku ikisadia kupambana na chunusi na kuponya ngozi iliyoungua.

Nazi ni miongoni mwa viungo maarufu vinavyotumika katika mapishi mbalimbali ikiwemo wali, maharage na aina nyingine za mboga.

Umaarufu wa kiungo hiki unazidi kuongezeka siku za hivi karibuni ambapo hupatikana kiurahisi madukani zikiwa tayari zimeshachujwa na kupakiwa katika pakti maalum.

Mbali na kutumika katika mapishi kiungo hicho hutumika kuandaa mafuta ambayo hung’arisha na kuimarisha ngozi.

Tovuti ya masuala ya afya ya Healthline inaeleza kuwa mafuta ya nazi husaidia kuongeza unyevu katika ngozi huku ikisadia kupambana na chunusi na kuponya ngozi iliyoungua.

Ili kupata faida hizo, unaweza kuandaa mafuta ya nazi nyumbani na kuepukana na gharama ya kuyanunua kila mara.

Utakachohitaji ni nazi (kiasi chako), maji safi,chujio na chombo cha kupikia(sufuria).

Jinsi ya kuandaa

Anza kwa kuandaa nazi, kwa kuzikuna  kwa kutumia kibao au kuzisaga kwa blenda mpaka zitakapokuwa laini.

Endelea kwa kuchuja nazi kwa maji masafi ili kuhakikisha unapata tui zito la kutosha ambalo utaweza kupata mafuta kwa wingi zaidi.

Baada ya kuchuja weka tui katika chombo kisafi na uliache kwa masaa 12 au zaidi. Unaweza kuweka katika friji au sehemu yoyote yenye joto la wastani.

Ili kufahamu kama tui lipo tayari kwa hatua inayofuata utaona limejitenga kwa kutengeneza matabaka mawili la juu likiwa limeganda au kushikana kiasi na chini likiwa maji matupu.

Ukifikia hapo tumia chujio kuondoa maji na ubaki na tui zito lililoganda  kwa ajili ya kuendelea na hatua nyingine.

Endelea kwa kuwasha jiko na kubandika sufuria yenye tui jikoni kisha uache lichemke hadi litakapoanza kutoa mafuta.

Baada ya hapo chuja mafuta kwa chujio au kitambaa kisafi kuondoa makapi yaliyopatikana kisha utayahifadhi katika chombo kisafi kwa ajili ya matumizi.

Mapaka hapo utakuwa tayari umetengeneza mafuta mazuri ya nazi, unaweza kuongeza viungo kama majani au mafuta ya ‘rosemary’ ili kuongeza harufu nzuri.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa