Jinsi ya kuandaa unga wa lishe kwa ajili ya mtoto

Na Fatuma Hussein
27 Nov 2025
Unga huu wa lishe unaweza kutumika kwa ajili ya watoto na familia lakini pia unaweza kutumika kama fursa ya biashara.
article
  • Ni muhimu kuzingatia mahitaji kulingana na muongozo wa wataalamu wa lishe.
  • Epuka kutumia nafaka nyingi ambazo zote hufanya kazi moja katika mwili.


Baada ya kujifunza kanuni za kuzingatia unapoandaa unga wa lishe kwa mtoto, leo tutaendelea mbele zaidi kujifunza namna ya kuutengeneza.

Kwa mujibu wa Afisa Lishe Mwamvua Zuberi kutoka mkoa wa Dar es Salaam, unga wa lishe wenye mchanganyiko maalum husaidia kuongeza madini na virutubisho muhimu katika ukuaji wa mtoto.

“Katika kuandaa uji tuache tabia ya kuchanganya nafaka nyingi kwa wakati mmoja kama vile ulezi, mtama, mchele na mahindi, kwa sababu kila nafaka ina tabia yake tofauti,” ameeleza Mwamvua.

Kwa mujibu wa tovuti ya Wema Herbal Clinic, uandaaji wa lishe kwa watoto unatakiwa kuzingatia umri na hatua ya ukuaji. Ili mtoto akue vizuri anahitaji virutubisho vya kutosha vinavyotokana na wanga, protini, vitamini na mafuta.

Unga huu wa lishe unaweza kutumika kwa ajili ya watoto na familia lakini pia unaweza kutumika kama fursa ya biashara kwa wajasiliamali.

Ndani ya JikoPoint leo tunaenda kujifunza hatua sahihi za kuandaa unga wa lishe wenye ubora kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu.

Hatua kwa hatua namna ya kuandaa

Hatua ya kwanza baada ya kunua mahitaji yote muhimu, chambua nafaka zote kwa kuondoa uchafu, mawe na mbegu zilizooza, kisha osha kwa maji safi ukitumia vyombo vya bati au chuma ambavyo hurahisisha kuona uchafu.

Picha hii imetengenezwa na akili unde kwa lengo la kuelimisha hatua ya uandaaji uji wa mtoto ikiwemo kuchambua soya.Picha/Gemin.

Baada ya kuosha, anika nafaka pamoja na mboga mboga kavu juani kwa siku mbili hadi tatu hadi zikauke vizuri.

Ni muhimu kuhakikisha kuwa umeanika mahitaji yote muhimu juani kabala ya kusaga. Picha/ Gemin.

Kwa upande wa soya, chemsha kwa dakika 10 ili iwe rahisi kuondoa maganda, menya kisha anika juani hadi zikauke kabisa.Ikiwa hutaweza kuchemsha, unaweza kuzikanga badala yake.

Hatua inayofuata ikiwa unatumia karanga au ufuta navyo vinapaswa kukaangwa kwa moto mdogo bila kuungua, au kuokwa kwenye oveni kwa nyuzi joto 60°C kwa dakika 15 hadi 20, kisha kuanikwa tena juani hadi vikauke.

 Baada ya hapo, chuja ufuta ili kuondoa makapi yaliyoungua au menya karanga na chagua zile zilizo bora zaidi.

Ukimaliza kuandaa mahitaji hayo ni vyema kukaanga nafaka moja baada ya nyingine kwenye sufuria kavu ili kuongeza ladha na kuongeza muda wa kuhifadhiwa. 

Baada ya kumaliza kuandaa mahitaji yote changanya nafaka pamoja na mboga mboga kavu kisha saga.

Wakati wa kusaga unaweza kupeleka katika mashine za kusagia vyakula, blender au kinu cha nyumbani, kisha chuja ili kupata unga laini.

Mara baada ya kuchuja, anika unga mahali pakavu hadi upoe, funika kwa kitambaa cha nyavu ili kuzuia wadudu na uchafu, kisha hifadhi kwenye chombo safi, kikavu na chenye mfuniko.

Unga wako wa lishe sasa utakuwa tayari kwa matumizi ya nyumbani au hata kufungwa kwa ajili ya biashara.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa