Jinsi ya kuchoma mishkaki kwenye jiko la umeme

Na Rodgers George
15 Mar 2022
Majiko haya yanapatikana kwa gharama kuanzia Sh70,000 hadi Sh100,000.
article
  • Unatakiwa kuwa na jiko la kuchomea nyama linalotumia umeme.
  • Jiko hilo linaweza kuchoma vyakula vyote na siyo nyama tuu.
  • Gharama yake ni kuanzia Sh70,000 hadi Sh100,000.

Kati ya sababu ambazo watu huzitumia kuendela kutumia mkaa ni mapishi ya nyama ya kuchoma, ni kutokufahamu njia nyingine za kuchoma nyama kwa kutumia nishati mbadala.

Utasikia mtu akisema “unachomaje mishkaki kwenye jiko la gesi?” Jibu linaweza lisiwe rahisi kulipata kama hujui nishati mbalimbali za kupikia.

Jiko Point hatuongelei nadharia, tunaongelea mambo ambayo yanashikika na baadhi ya watu tayari wanayatumia.

Katika pita pita zangu mjini Instagram hivi karibuni, nilikutana na ukurasa wa bidhaa za jikoni na mdau huyo (vadeeonline) alikuwa akionyesha namna jiko la kuchoma mishikaki linavyofanya kazi.

Kati ya vitu vilivyonivutia zaidi ni kuwa, unachohitaji kutumia jiko hilo, ni umeme tu. Siyo mkaa wala kuni, ni umeme.

Kwenye jiko hilo unaweza kuchoma nyama pamoja na vyakula vingine kama mahindi. Picha| Daraz.

Linafanyaje kazi?

Unachotakiwa ni kuandaa mishikaki yako kwa kuikata na kuiweka kwenye vijiti vyake. Katika uchomaji wa mishikaki, inashauriwa kuunga nyama na viungo vya kulainisha nyama kama tangawizi na kitunguu swaumu.

Baada ya kuandaa mishkaki, andaa jiko lako la kuchomea vyakula kwa ajili ya kuchoma nyama. Maandalizi ya jiko hilo ni pamoja na kuweka trei ya kunasia mafuta.

Washa jiko lako na acha moto ukolee. Utajua kuwa moto umekolea kwa kuona koili za jiko lako zimeanza kuwa rangi ya machungwa. Bada ya hapo anza kuchoma mishkaki uliyoiandaa.

Hakikisha unasafisha jiko lako maa baada ya kutumia kuepuka uharibifu na mafuta kugandiana.

Mbali na nyama, kwa kutumia jiko hili unaweza kuchomea mahindi, viazi na chakula chochote kinachofaa kuchomwa.

Kwa wadau wa bidhaa za jikoni, jiko hili linapatikana kwa Sh70,000 hadi Sh100,000 na zaidi.

Kisingizo chako cha kuendelea kutumia mkaa ni nini? Tueleze tukuletee suluhu.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa