Jinsi ya kufanya blenda yao idumu muda mrefu

Na Rodgers George
3 Mar 2022
Ni kwa kuzingatia matumizi ya blenda yako na kuepuka kuifanyisha kazi isyoendana na uwezo wake.
article
  • Unashauriwa kukata vyakula unavyosaga viwe katika vipande vidogo vidogo.
  • Unaposaga vitu vyako anza na kasi ya chini kuelekea juu.
  • Ikichemka, ipumzishe.

Ule usemi wa kwamba kila kitu kinadumu kulingana na matumizi, unaweza kuwa umeusikia ukaupuuzia lakini unaweza kuwa ni kweli.

Wewe na jirani yako mnaweza kununua blenda sawa lakini huenda yako ikaharibika mapema na ya jirani yako ikaendelea kupeta tu. Hiyo yote ni kutokana na matumizi yako.

Haya ndiyo mambo ambayo wataalamu wanashauri kuzingatia unapokuwa unatumia blenda yako iwe nyumbani au hata katika biashara ikiwemo ya kuuza juisi:

Zingatia saizi ya vitu unavyovisaga

Blenda kubwa inaweza kusaga kila kitu kinachowekwa ndani ya jagi lake, haimaanisha haihitaji msaada wako katika kupunguza saizi ya vitu hivyo.

Mfano kama unasaga juisi, kukata matunda katika vipande vidogo vidogo vitairahisishia kazi blenda yako na pia kutokutumia muda mrefu kufanya kazi.

Mtaalamu wa mapishi, Jessica Gavin kupitia tovuti yake ameandika kuwa, kama unasaga kitu ambacho siyo kimiminika, ni vyema ukakitaka kwenye vipande vidogo vidogo.

Hakikisha unavikata vitu unavyotaka kuvisaga katika maumbo madogo madogo. Picha| Simply Recipes.

Kutoka moto mdogo hadi mkubwa

Unavyosaga vitu kwenye blenda huwa unawashaje swichi yako? Wapo ambao huipeleka swichi ya kuongezea kasi moja kwa moja kwenye namba ya juu mfano namba tatu au nne au kasi ya mwisho kabisa.

Hiyo siyo sahihi kwani mota ya blenda inatakiwa kufanya kazi kwa hatua. Unapowasha mashine yako, hakikisha kiwango cha kasi kipo chini kabisa na kisha anza kupandisha taratibu kadri unavyosaga vitu vyako.

Pia usiiache blenda ikaunguruma kwa muda mrefu. Hakikisha inafanya kazi kwa walau sekunde 30 na unaipumzisha kabla ya kuendelea tena.

Usijaze blenda yako kupitiliza

Wapo ambao huweka vitu vingi kwenye blenda kiasi cha kwamba inajaa hadi alipoishia fundi. Jambo hilo siyo sahihi kwenye matumizi ya blenda.

Inashauriwa kuacha nafasi kidogo kwa ajili ya kuruhusu blenda ichanganye matunda au chochote unachosaga vizuri.

Nafasi hiyo itatumika kama eneo la kuzungukia vitu hivyo wakati unasaga.

Unapokuwa unatumia blenda na ukaona imeanza kuchemka, ipumzishe. Picha| vitamix.

Ikichemka iache

Huenda unasaga kitu kizito na benda ikatumia nguvu nyingi zaidi. Katika hali kama hiyo, huenda ukaanza kuhisi joto la mashine linapanda. 

Kwa wengine husema “aluta continua” lakini kitaalam, inashauriwa uonapo joto la mashine linaongezeka, izime na ukiweza chomoa kabisa waya. Ipatie nafasi ipumue kwa muda na utaendelea baadaye.

Unaweza kuchagua kupunguza kiasi cha kimiminika unachotengeneza (kukigawa mara mbili) ili blenda yako ifanye kazi kwa ufanisi.

Natumaini baada ya hapa, ukinunua blenda yako itadumu muda mrefu.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa