Jinsi ya kuhifadhi vitunguu kwa muda mrefu

Na Fatuma Hussein
26 Nov 2025
Ni pamoja na kuepuka kuviweka karibu na kuta za nyumba au kubebanisha vitunguu wakati wa kuhifadhi.
article
  • Ni pamoja na kuepuka kuviweka karibu na kuta za nyumba au kubebanisha vitunguu wakati wa kuhifadhi.

Kama ilivyo umuhimu wa chakula katika mwili wa binadamu ndivyo ulivyo umuhimu wa vitunguu maji katika mapishi.

Kwa wazoefu wa masuala ya jikoni, wanafahamu umuhimu wa kiungo hicho chenye uwezo wa kuongeza harufu na ladha nzuri katika aina mbali mbali za vyakula.

Licha ya umuhimu na urahisi wa upatikanaji wake, wapishi wengi hukumbana na changamoto ya kuhifadhi hususani vinaponunuliwa kwa wingi kwa ajili ya matumizi ya muda mrefu.

Changamoto hiyo huvifanya vitunguu hivyo kuoza na kuwanyima uhuru wanunuzi au wapishi kutunza viungo hicho muhimu.

Makala hii inaenda kukupa mbinu rahisi na za uhakika za kuhifadhi vitunguu nyumbani kwa kutumia vifaa vya kawaida, ili kuzuia upotevu na kuhakikisha una vitunguu safi kila wakati.

Beba kwa uangalifu
Kwa mujibu wa tovuti ya National Onion Association ,ubora na usalama wa vitunguu unategemea jinsi vinavyoshughulikiwa na kuhifadhiwa ipasavyo.

Hivyo, ni muhimu kubeba vitunguu kwa uangalifu ili kuzuia kujeruhi ngozi yake ya nje kunakotokana na kubanwa sana au kudondoshwa.

Uharibifu huu wa ndani husababisha harufu mbaya na hupunguza muda wa maisha ya kitunguu hivyo hakikisha unabeba kwa uangalifu kwa mikono miwili au mfuko.

Mwanga wa jua huunguza vitunguu na kubifanya kutengeneza unyevu ambao baadae huozesha vitunguu.Picha/inkitchen.


Hifadhi sehemu baridi, kavu na yenye hewa ya kutosha
Sehemu bora ya kuhifadhi vitunguu ni ile yenye hewa safi inayopita vizuri, bila unyevunyevu wala joto kali. hii huzuia ukungu na bakteria wanaosababisha kuoza.

unaweza kuhifadhi sehemu ya chini ya jiko, au katika ghala lenye madirisha madogo ni maeneo mazuri ya kuhifadhia.Usiviweke karibu na sinki au sehemu zinazopata unyevu mara kwa mara, kwa kuwa unyevu ni adui mkubwa wa vitunguu.
Hewa safi na mazingira kavu huwezesha vitunguu kudumu muda mrefu zaidi.


Epuka kuhifadhi katika mifuko ya plastiki
Mifuko ya plastiki huzuia hewa kupita, hivyo unyevu unaojikusanya ndani husababisha vitunguu kuoza haraka.

Hali hii pia huchochea kuota kwa mapema, jambo linalopunguza ubora wake. Badala yake, tumia mifuko ya karatasi au ya vikapu vya asili ambayo huruhusu hewa kupita.

Ikiwa unahitaji kubeba, unaweza kutumia plastiki kwa muda mfupi tu, lakini kwa uhifadhi wa muda mrefu, chagua mifuko inayopitisha hewa.Hii itasaidia kudhibiti unyevunyevu na kudumisha uthabiti wa vitunguu.

Mifuko ya wavu inasaidia kupitisha hewa hivyo kuepusha vitunguu kuoza.Picha/India Mart.

Chagua vitunguu vikavu
Wakati wa kununua au kuvuna, hakikisha unachagua vitunguu vikavu na vilivyokomaa. Epuka kuchagua vitunguu vyenye madoa, ukungu au vilivyoanza kuota.

Vitunguu vizuri huwa na ngozi ya nje kavu, na rangi ya kuvutia bila alama nyeusi au kijivu.
Kuchagua vitunguu bora tangu mwanzo hupunguza hatari ya vitunguu vyenye shida kuambukizwa vitunguu vizuri wakati wa kuhifadhi.

Hata kitunguu kimoja kilichoharibika kinaweza kuambukiza vingine haraka ndani ya gunia moja.

Usiviweke karibu na viazi
Viazi hutoa gesi na unyevu wakati vinapohifadhiwa, hali inayoweka vitunguu vilivyokaribu na viazi hatarini kuharibika.

Weka viazi na vitunguu katika sehemu tofauti kabisa, ikiwezekana vyumba tofauti au chombo maalum kila kimoja ili kudhibiti unyevu na kupunguza uwezekano wa kuoza mapema.

Viazi hutoa gesi inayosababisha viazi kuoza kwa urahisi hivyyo hawiwezi kukaa karibu kwa muda mrefu.Picha inkitchen

Epuka mwanga wa jua na joto la moja kwa moja
Mwanga wa moja kwa moja wa jua huongeza joto, jambo linalosababisha vitunguu kuota au kukauka.

Hifadhi vitunguu kwenye eneo lenye kivuli na baridi kwani mwanga unapogonga moja kwa moja, unaharibu ngozi ya nje na kupunguza muda wake wa kuhifadhiwa.

Zaidi ya hayo, joto la juu husababisha maji ya ndani ya kitunguu kuyeyuka haraka, na kufanya kitunguu kuwa chepesi na kisicho na ladha. Sehemu yenye kivuli na ubaridi wa wastani ndiyo salama zaidi.

Kuhifadhi vitunguu kwa muda mrefu hakuhitaji teknolojia ya gharama kubwa. Kwa kufuata hatua hizi rahisi utaweza kupunguza upotevu na kuhakikisha una viungo safi kila wakati jikoni.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa