Jinsi ya kuosha vizuri vyombo vyenye mafuta

Na Herimina Mkude
5 Feb 2022
Kutokuosha vizuri kwa vyombo sio tu kunafanya vyombo vyako kuwa na muonekano mbaya bali kunavutia wadudu kama nzi na mende.
article
  • Unashauriwa kutumia maji ya moto kuosha vyombo hivyo kwa ufanisi.
  • Uoshaji vizuri wa vyombo hivyo husaidia kupunguza nzi na mende jikoni kwako.

Jambo ambalo huleta maumivu ya kichwa baada ya kula ni kuosha vyombo. Shughuli hii kwa baadhi hufanya wahisi uvivu kupika.

Kimbembe zaidi kinakuja pale vyombo hivyo vinapokuwa vimetumika kwenye vyakula vyenye mafuta au shombo, kama dagaa, mchuzi na supu ya nyama.

Mara nyingi vyombo hivyo vimekuwa havioshwi vizuri kiasi cha kufanya kubaki na harufu au shombo ya pishi husika.

Sidhani kama utafurahia kutumia chombo kilicho na hali hiyo, hivyo soma kwa umakini hatua zifuatazo zitakupa mwongozo wa kuosha vizuri vyombo vyenye mafuta.

Shughuli ianze.

  1. Ondoa mabaki ya chakula kweye vyombo.
  2. Chemsha maji yakutosha.
  3. Mimina maji ya moto kwenye sinki au dishi lenye vyombo vyenye mafuta.
  4. Baada ya mafuta kuyayuka, mwaga maji hayo kama unatumia dishi au fungua “drainer” kama ni sinki.
  5. Changanya maji mengine ya moto na ya baridi kupata maji vugu vugu.
  6. Anza kuosha vyombo vyako.
Unashauriwa kuondoa uchafu wa mifupa na vyakula kabla ya kuanza kuosha. Picha| The Kitchn.

Kwa upande wa sabuni ninashauri usitumie sabuni ya kipande kwenye kuoshea vyombo vyenye mafuta, kwani sabuni hizo mara nyingi huwa na mafuta pia, hivyo inakuwa vigumu kuondoa shombo au mafuta kwenye vyombo.

Unaweza kutumia sabuni maalum za kuoshea vyombo, au sabuni ya unga isiyo na harufu kali.

Kwa wanaotumia dishi kuoshea vyombo, usiviweke vyombo vyote ndani ya dishi wakati unaosha, weka chombo kimoja kwenye dishi, ukishakiosha kiweke pembeni ndipo uweke kingine.

Kufanya hivyo kunasaidia kuosha chombo kwa nafasi, na kuepusha chombo unachoosha kubeba mafuta au shombo ya vyombo vingine.

Ukimaliza kuviosha, weka maji mengine ya uvuguvugu kwa ajili ya kusuuzia. Unaposuuza hakikisha chombo chako hakina utelezi wa mafuta wala harufu ya chakula.

Hadi hapo unaweza kuvikausha vyombo vyako na kuviweka mahala husika.

Kutokuosha vizuri kwa vyombo sio tu kunafanya vyombo vyako kuwa na muonekano mbaya bali kunavutia wadudu kama nzi na mende.

Wadudu hao wanasambaza bakteria ambao wanasababisha magonjwa ikiwemo kuumwa tumbo na kuharisha.

Jiepushe na madhira hayo kwa kuosha vizuri vyombo vyako. Usiache kufatilia Jikopoint  YouTube kwani nitakuwekea video ya hatua hizi ili uweze kuelewa zaidi.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa