Ndizi mbivu ni miongoni mwa matunda pendwa yasiyokuwa na msimu yanayofaa kutumiwa na watu wa rika zote.
Rangi ya njano iliyokolea ni miongoni mwa sifa adhimu zinazoitambulisha ndizi iliyoiva vizuri ambayo ipo tayari kuliwa.
Lakini utafanyaje ikiwa ndizi zako ulizozinunua kwa wingi zitaiva kupitiliza kiasi cha kushindwa kulika.
Najua jibu la haraka haraka linaweza kuwa kuzitupa, lahasha zipo aina nyingi za vinywaji au viburudisho unavyoweza kuandaa kwa kutumia ndizi hizo ikiwemo ice cream
Ndio! Ndizi zilioziva zinaweza kutengeneza ‘ice cream’ tamu ikiwa utachangamya na mahitaji mengine ikiwemo vanila na maziwa.
Kufahamu namna rahisi ya kutengeneza kiburudisho hiki hususani wakati huu wa jua kali fuatana nami mpaka mwisho wa makala hii.
Maandalizi
Hatua ya kwanza ni kumenya ndizi na kuzikata vipande vidogo vidogo ili kurahisha mchakato wa kuandisha pale utakapohamishai katika friji.
Hakikisha ndizi unazozitumia zimeiva sana kiasi cha rangi ya maganda kuanza kubadilika rangi kutoka kuwa njanpo angavu kuwa njano iliyoiva sana.
Baada ya kukakata gandisha ndizi kwa msaa 4 au zaidi kutegemea na uwezo wa friji yako. Wakati unasubiri zigande chemsha maziwa kiasi chako kulingana na wingi wa ndizi au ice cream unayotaka kuandaa kisha uache yapoe,
Zikiganda endelea na hatua nyingine ambayo ni kuandaa blenda kisha mimina ndizi zilizoganda, maziwa kiasi (yasizidi kiwango cha ndizi) pamoja na vanila kijiko kimoja au zaidi.
Saga vitu mahitaji yote mpaka upate mchanganyiko mzito (kama zilivyo ice cream nyingine) na ikiwa mchanganyiko wako ni mwepesi ongeza vipande vya ndizi vilivyoganda.
Baada ya kusaga itoe kwenye bleda na uweke katika chombo chenye mfuniko na urudishe katika friji kwa saa 1 au zaidi na itakuwa tayari kwa kuliwa.
Hakuna haja ya kuongeza sukari kwani ndizi za kuiva zina kiwango kikubwa cha sukari kinachotosheleza mahitaji.