Umeshawahi kualikwa katika chakula cha usiku sehemu na ukalazimika kutumia kisu na umma?
Baadhi ya watu wakikutana na vifaa hivyo vya jikoni hupuuzia matumizi yake huku wengine wakijilazimisha kutumia licha ya kutofahamu kanuni zake na kujikuta wanakosea.
Ikiwa umewahi kukutana na changamoto hiyo, usijali hizi hapa kanuni sita zitakazokupa ujasiri wa kuonyesha ustadi wako popote unapotumia vifaa hivi.
Weka kisu upande wa kulia wa sahani na uma upande wa kushoto.
Hakikisha vyombo hivi vimepangwa nje ya chakula, ili kuepusha kuonekana bila mpangilio.
Mpangilio huu unaashiria kuwa uko tayari kuanza mlo, jambo linalosaidia mhudumu kuelewa unachohitaji.
Unapohitaji kupumzika kidogo, panga kisu na uma ndani ya sahani kwa umbo la pembe, vikielekea kama saa 4:20.
Pembe hii ina maana maalum ya kimataifa inayotumiwa kueleza kuwa hujamaliza chakula.
Hii pia inasaidia kuhifadhi mazingira ya utulivu mezani bila mhudumu kukurupuka kuondoa sahani yako.
Ukimaliza kula, panga kisu na uma sambamba ndani ya sahani, vikielekea saa 4.
Ishara hii ni ya heshima na inarahisisha kazi ya mhudumu wa chakula.
Inazuia mkanganyiko wa kuacha vyombo visivyoeleweka au vyenye mpangilio mbaya.
Kama umefurahia chakula, weka uma na kisu sambamba ndani ya sahani, lakini ncha zake ziguse sehemu ya juu ya sahani.
Ishara hii inaonyesha shukrani yako kwa mpishi na huduma nzuri uliyopokea.
Inakufanya kuwa mteja anayejali mawasiliano ya heshima na timu ya wahudumu.
Unapohitaji kuongeza chakula, panga kisu na uma ndani ya sahani kwa umbo la jumlisha (“+”).
Mpangilio huu ni mawasiliano ya moja kwa moja na mhudumu kuwa bado unaendelea kufurahia chakula na unatarajia zaidi.
Inapunguza usumbufu wa kuzungumza au kupiga kelele kuwaita wahudumu.
Ikiwa chakula hakikuridhisha, panga kisu na uma kwa umbo la msalaba ndani ya sahani.
Ncha za vyombo ziwe zikivuka katikati ya sahani, ikionyesha kuwa chakula hakikukufurahisha.
Ishara hii ni njia ya kistaarabu ya kuonyesha kutoridhika badala ya kutoa maneno ya lawama waziwazi.
Unapokuwa na watu wengine, iwe ni marafiki, familia, au washirika wa kibiashara, ni muhimu kuonyesha ustadi wako wa kutumia kisu na uma.
Weka kisu mkono wa kulia kwa kukata, na uma mkono wa kushoto kwa kushikilia unapokata au kupeleka chakula mdomoni.
Kwa kufuata kanuni hizi, utaongeza heshima na kujihisi ujasiri zaidi wakati wa kula katika mazingira yoyote.