Kutana na majiko banifu yanayotumia umemejua Tanzania

Na Mariam John
8 Oct 2021
Majiko yake hutumia mawe ya volcano na udongo wa mfinyanzi badala ya mkaa na huendeshwa kwa umemejua.
article
  • Umemejua hutumika kufua upepo kukoleza moto.
  • Yanatumia mawe ya volkano na udongo mfinyanzi kama “mkaa”. 
  • Yanapunguza matumizi ya mkaa na kuni.

Mwanza. Baada ya kuhitimu elimu yake, Tagemeo Nzigo (32) alianza kujihusisha na shughuli ndogo ndogo za ujasiriamali wa utengenezaji wa majiko ya kupikia.

Safari ya Tegemeo, mzaliwa wa Kasulu mkoani Kigoma, ilianza kwa kutengeneza jiko linalotumia kuni lakini kutokana na kuzalisha moshi mwingi hasa kipindi cha mvua ilimlazimu kuongeza ubunifu mwingine wa kutengeneza jiko ambalo halitumii mkaa wala kuni katika upishi.

“Niliamua kubuni jiko hili ambalo halitumii mkaa kutokana na hali ya uchumi hususani wa kijijini ambao wengi hawana uwezo wa kununua mkaa kwa ajili ya kupikia,” anasema Tegemeo.

Tegemeo anasema alitamani kuja na jiko ambalo litasaidia katika utunzaji wa mazingira ambao wananchi wengi wanakata miti ovyo kwa ajili ya kupikia hivyo kusababisha janga.

Sasa amebuni jiko banifu la kisasa linalotumia chenga za mkaa na hivyo kupunguza matumizi ya mkaa ikiwa ni hatua kuanza kutumia nishati safi na salama za kupikia.

‘Mkaa’ wake ni mawe na udongo wa mfinyanzi

Jiko hili linalotumia mawe ambayo ni mabaki ya volkano maarufu kwa wengi kama mawe ya kusugulia miguu. 

Likiwa katika umbo la namba nane, jiko hilo lina mfumo wa upepo unaotumia umemejua, betri za simu, power bank (kitunza chaji)  na umeme wa gridi wa kawaida ambao umepunguzwa nguvu kupitia vifaa vya kielektroniki kama adapta na kuwa na mkondo mnyoofu (DC).

Jiko hilo linahitaji umeme mdogo sana ili kuwaka na likiunganishwa kwenye umeme mkubwa haliwaki na linaharibika muda huo huo.

Ili mawe haya yaweze kuwaka baada ya kuwekwa jikoni lazima yachanganywe na chenga au vumbi kidogo la mkaa ili kuyasaidia yashike moto.

Baada ya hapo huendelea kuwaka yenyewe yakitegemea zaidi hewa ya oksijeni inayofuliwa na feni iliyopo upande wa chini wa jiko kwenye kiboksi maalumu.

Tegemeo akiendelea na utengenezaji wa jiko banifu linalotumia mawe ya volkano ili kuokoa mazingira.

Fungu moja la mawe, miezi sita

Kwa mujibu wa Tegemeo, fungu moja la mawe au tofali za udongo wa mfinyanzi zinaweza kutumika kwa kipindi cha miezi sita bila kuisha hata kama mtumiaji akifululiza kupika vyakula vinavyochukua muda mrefu kama maharage na makande.

Fungu la mawe hayo huuzwa kati ya Sh2,000 na S4,000. Ikiwa mtu akishindwa kuyapata anaweza kutumia udongo mfinyanzi ambao unapatikana katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania. Jiko moja lina uwezo wa kubeba mawe matatu hadi sita kutegemeana na ukubwa wa jiko.

Nini kilimsukuma kutengeneza jiko hili?

Kwa mara ya kwanza mwaka 2016, Tegemeo anasema alianza kutegeneza jiko linalotumia mkaa na kuunganishwa na umemejua lakini matokeo yake mkaa ulikuwa unaisha kwa kasi.

“Nikabadilisha badala ya kuweka mkaa nikawa naweka misumari lakini pia nikaona misumari inayeyuka kwa haraka na ni hatari kwa mtumiaji,” anasema Tegemeo.

Katika kipindi hicho, jiko hilo halikupata wateja kwa sababu ufanisi na ubora wake haukukubalika sokoni. 

“Wengi hawakuja kwa nia ya kununua bali walikuja kwa ajili ya kushuhudia namna linavyofanya kazi, baadaye nikaona ni njia ya kujipatia kipato ili mtu aje kumwonyesha namna nilivyotengeneza na linavyofanya kazi alilazimika kulipa Sh500 hadi Sh1,000, fedha ambazo zilinisaidia katika kununua vifaa vya kutengenezea jiko jipya,” amesema kijana huyo.

Aina mbalimbali za majiko banifu yaliyotengenezwa na kijana Tegemeo yakiwa tayari soko kwa ajili ya wateja.

Hatua zaidi mbele

Baada ya jiko la kwanza kukosa wateja aliamua kupiga hatua ya ubunifu na kuliboresha zaidi. Sasa ametengeneza jiko ambalo halina tofauti na majiko mengine.

Tofauti ya jiko hili hutengenezewa mfumo unaotumia umeme pamoja na sehemu ya feni ambayo hutumiwa na mpishi katika kuongeza na kupunguza moto kutegemea na kiwango cha moto anachotaka kukitumia kwa wakati huo.

“Kwa namna jiko langu nilivyotengeneza ukiliwekea mkaa na kuliwasha kawaida haliwezi kuwaka na ukilichomeka kwenye soketi ya umeme linaharibika hapo hapo kwa kuwa linahitaji umeme mdogo kama unaotumika kwenye simu,” anasema.

Majiko yaanza kukubalika sokoni

Baada ya kufanikiwa kudhibiti mfumo wa umeme na kuanza kutumia mawe ya volkano na umemejua, ndipo jiko hilo likakubalika sokoni na wateja wake.

Katika kipindi cha miaka minne tangu mwaka 2018 biashara yake ilianza kupamba moto, jamii inayomzunguka na watu kutoka maeneo tofauti walielewa ubunifu wake ambao ulisababisha kujiongezea umaarufu katika wilaya ya Kasulu.

Kwa sasa anamiliki nyumba kubwa yenye vyumba vinne na ameajiri watumishi watano wanaomsaidia katika kuunda majiko hayo katika ukubwa tofauti tofauti.

Kupitia majiko hayo, pia amekuwa akipigiwa simu kila kona ya nchi watu wakihitaji kupata majiko hayo.

Tegemo anasema wakati anaanza alikuwa na uwezo wa kutengeneza majiko mawili kwa wiki moja lakini baada ya wateja kuongeza ameajiri watu ambao humsaidia kutengeneza majiko ambapo kwa wiki moja hutengeneza majiko zaidi ya 20.

Tegemeo anabainisha kuwa toka majiko hayo yalipoanza kununuliwa na watu mwaka 2018, tayari majiko zaidi ya 800 ya size tofauti tofauti yalishanunuliwa.

Gharama ya chini ya jiko moja size ya kati huuzwa Sh75,000 lakini pia yapo majiko makubwa yanayouzwa kati ya Sh100,000 hadi Sh290, 000.

Majiko ambayo hutengenezwa yapo yenye sehemu mbili hadi tatu za kupikia (plate) na kwamba  wateja wake wakuu ni mama wa nyumbani, mama lishe na hoteli.

Changamoto anayopitia

Pamoja na majiko hayo kusaidia katika kuhifadhi mazingira, baadhi ya wateja wake kushindwa kuzingatia maelekezo ya jinsi ya kutumia na hivyo huharibika mapema baada ya kuunganisha kwenye umeme wenye nguvu kubwa.

“Wengi wanapofika nyumbani hujisahau na kuchomeka kwenye soketi za umeme hivyo huwalazimu jiko hilo kulirudisha tena kwa ajili ya kutengenezwa upya hivyo kumlazimu mteja kutumia gharama mara mbili,” anasema Tegemeo.

Tegemeo akionyesha chenga za mkaa ambazo huchanganywa na mawe ya volkano ili kuwasha moto kwenye jiko banifu. Betri za kawaida zinaweza pia kuendesha feni ya jiko. Picha zote| Mariam John.

Wateja wanasemaje?

Katika duka la Tegemeo jijini Mwanza, Jiko Point (jikopoint.co.tz) ilishuhudia watu mbalimbali wakiwa wanajitokeza kuangalia bidhaa hizo na wengine wakirudisha majiko kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho.

Joyce Gerald, mmoja wa wateja ambao walinunua jiko kwa Tegemeo toka mwezi wa sita,anasema jiko hilo ni zuri na linahitaji matunzo na uangalizi kama mtoto mdogo.

“Ni zuri linafaa kwa utunzaji wa mazingira na linapunguza gharama za matumizi ya mkaa lakini changamoto yake ni uangalizi linahitaji umakini wa kiwango cha juu,” anasema Joyce.

Ukosefu wa malighafi ni changamoto kuu

Mama huyo anaeleza kuwa changamoto nyingine ni uhaba wa wa matofali yanayotokana na udongo wa mfinyanzi na volkano na ana wasiwasi kama malighafi hizo zinaweza kutumika kwa muda wa miezi sita.

“Nimelipenda linarahisisha kwenye upikaji hakuhitajiki jiko lingine la ziada hata kama una haraka ila linasababisha sufuria nyepesi kutoboka mapema  kwa kuwa moto wake ni mkali,” anasema Joyce.

Pamoja na changamoto hizo, Joyce anawataka vijana kuendelea kuwa wabunifu wa teknolojia na nishati rafiki kwa mazingira ili kupunguza ukataji wa miti unaosababisha mabadiliko ya tabianchi.

Ili kuweza  majiko hayo kutoa huduma zaidi, Tegemeo na wenzie watalazimika kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha uwepo wa malighafi na kutoa maelekezo bora namna ya vyombo vinavyoweza kutumika katika majiko hayo. 

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa