Mambo ya kuzingatia unapotumia  ‘rice cooker’

Na Lucy Samson
3 May 2023
Kama lilivyo jina lake, jiko hili la kisasa linalotumia umeme linaweza kuivisha wali ndani ya muda mfupi huku likikupunguzia hatari ya chakula chako kuungua.
article
  • Hakikisha hakuna maji maji yoyote kwenye sufuria kabla hujachomeka waya kwenye umeme.
  • Funika vizuri ili kutoruhusu mvuke kutoka ndani ya kifaa hicho wakati wa kupika. 
  • Hakikisha umeweka maji na viungo vinavyohitajika kabla ya kuanza kupika. 

Wabunifu mpaka jikoni. Hauhitaji kutumia muda mwingi kupika kwa sababu teknolojia inaweza kukufanyia kila kitu, shughuli inabaki kula na kufanya mambo mengine ya maendeleo.

“Rice cooker” ni miongoni mwa vifaa vya kielektroniki vinavyorahisisha shughuli ya mapishi. 

Kama lilivyo jina lake, jiko hili la kisasa linalotumia umeme linaweza kuivisha wali ndani ya muda mfupi huku likikupunguzia hatari ya chakula chako kuungua.

Ikiwa  haufahamu matumizi ya ‘rice cooker’ usijali, makala hii ni kwa ajili yako ambapo utajifunza hatua kwa hatua namna unavyoweza kuivisha pishi lako ndani ya dakika 15 tu.

Ndio! Dakika 15 zinatosha kabisa kuivisha wali kwa kutumia ‘rice cooker’ ingawa wauzaji wa vifaa hivyo wanasema inaweza kuchukua hadi dakika 20 kutokana na wingi wa mchele.

Aina nyingi za ‘rice cooker’ huwa na sufuria au mabakuli yenye matobo yanayowezesha kupika mboga mboga kwa kutumia mvuke. Picha | Ms lousware/Instagram.

“‘Rice cooker’ inakupunguzia muda wa kukaa jikoni. Mfano unapika chakula cha kilo moja au zaidi unaweza kutumia hadi dakika 20,” anasema  Patrick Daudi, muuzaji wa majiko hayo jijini Dar es Salaam.

Majiko haya huuzwa kwa muundo na ukubwa mbalimbali. Yapo yanayopika kilo moja, kilo moja na nusu mpaka kilo mbili na nusu kuwawezesha wenye familia kubwa kutumia kwa uhuru.

Aina nyingi za ‘rice cooker’ hutengenezwa kwa plastiki ngumu kwa nje na kwa ndani inakuwa na sufuria ambayo ndiyo hutumika kwa ajili ya kupikia.

Uzuri wa sufuria hii ni kwamba unaweza kuitoa na ukaiosha mara baada ya kumaliza kupika.

Hatua kwa hatua matumizi ya ‘Rice cooker’

Hatua ya kwanza kabisa unapoanza kutumia ‘rice cooker’ ni kuosha sufuria ya ndani na kuikausha kwa kitambaa kisafi. Hakikisha hakuna maji maji yoyote kabla hujachomeka waya kwenye umeme.

Baada ya hapo anza kwa kuchambua  mchele, osha na ukaushe maji tayari kwa ajili ya kupika.

Hatua uinayofuata ni kuweka mchele kwenye sufuria ya ‘rice cooker’ weka chumvi, mafuta pamoja na maji kiasi kisha ukoroge vizuri vichanganyike.

Unaweza pia kuongeza na viungo mbalimbali uvipendavyo kama nazi karoti, hoho au iriki.

“Katika hatua hii mimi napenda kuweka tui la nazi, nikishachanganya mchele na chumvi, tui la nazi nafanya kama ndiyo maji kisha napika,”  anasema Mwanaidi Shabani mkazi wa Mkorora, mkoani Tanga.

Moja kati ya jambo la kuzingatia kwenye matumizi ya ‘rice cooker’ ni kupima kiwango sahihi cha maji ili kuwezesha wali kuiva vizuri.Picha|Tsunex/instagram.

Ukijiridhisha na kiwango cha chumvi na viungo funika na uwashe ‘rice cooker’ kisha bonyeza sehemu iliyoandikwa ‘cook’ na uache chakula chako kiive.

Katika hatua hii ya kupika Daudi anasema  ‘rice cooker’ nyingi zina kitufe kinachoruhusu kifaa hicho kuanza kupika huku kikimbatana na taa nyekundu itakayowaka wakati jiko limeanza kupika.

“Ukishaona imewaka taa nyekundu unaweza kuendelea na mambo yako hapo litapika ikifika hatua maji yamekakuka litaanza kukausha ‘warm’ na likimaliza linajizima lenyewe,” amesema Daudi.

Wapo pia wanaopika pilau, dizi na aina nyingine ya vyakula kwa kutumia jiko hilo la kisasa, ila kwa leo tuishie hapa.

Pakua chakula chako na ule pamoja na uwapendao.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa