Ni jambo lisilopingika kuwa jiko la umeme la shinikizo (pressure cooker) ni mkombozi wa masuala ya mapishi kutokana na uwezo wake wa kupika vyakula zaidi ya 50 ndani ya muda mfupi.
Uwezo huo huwasaidia wapishi kupika haraka kwa ufanisi jambo linalotajwa kuokoa muda na gharama.
Llicha ya faida zake lukuki, ili kuhakikisha kifaa hiki kinadumu na kuendelea kufanya kazi kwa ubora wa hali ya juu, ni muhimu kufahamu kwamba kuna baadhi ya mapishi ambayo huwezi kuyapika kwa kutumia kifaa hicho kutokana na sababu mbalimbali.
Kashata ni kitafunwa kitamu kinachotengenezwa kwa sukari na kuchanganywa na nazi, karanga au ufuta. Upishi wake huhitaji joto la moja kwa moja na udhibiti makini ili sukari iyeyuke vizuri bila kuungua.
Iwapo itapikwa kwenye pressure cooker iliyofungwa, sukari huyeyuka na kuenea hadi sehemu za juu za sufuria na mfuniko. Hali hii husababisha kushikamana vibaya, kuunguza pishi lote na hata kuharibu kifaa.
Hata bila kufunga mfuniko, tatizo hubaki pale pale. Sukari inapoanza kuganda hujishikiza kwa nguvu kwenye sufuria na inalazimisha kukwanguliwa kwa nguvu, jambo linaloharibu uso wa ndani wa sufuria na jiko lake. Kwa sababu hii, pressure cooker haifai kwa maandalizi ya kashata.
Chapati
Ni kitafunwa kinachopendwa sana asubuhi kwa supu au chai.
Chapati hutengenezwa kwa unga wa ngano, chumvi,sukari na mahitaji mengine kisha kukaangwa kwa joto la wastani.
Endapo itapikwa kwenye pressure cooker yenye shinikizo, mvuke mkali hukusanyika na kufanya isiive vizuri na kuwa laini.
Hata bila kufunga mfuniko, pressure cooker bado haiwezi kutoa muonekano uliozoeleka wa chapati hivyo kupoteza mvuto wake na kuifanya ikakamae.
Bisi za sukari hutengenezwa kwa nafaka za mahindi zinazopasuka kisha kuchanganywa na sukari iliyoyeyuka. Mapishi haya huhitaji nafasi ya wazi ili nafaka zipasuke vizuri na sukari isigande vibaya.
Iwapo zikipikwa kwenye pressure cooker yenye shinikizo, nafaka hazipati nafasi ya kupasuka kwa uhuru. Baadhi hubaki ngumu, zingine huungua, huku sukari ikishikamana vibaya bila kukauka jambo ambalo huenda likapoteza ladha.
Hata bila kufunga mfuniko tatizo hubaki. Sukari huyeyuka vizuri lakini haiwezi kukauka vizuri , jambo linalosababisha ‘popcorn’ kutoshika vizuri sukari kwa sababu hiyo pressure cooker si chombo sahihi kwa maandalizi ya bisi za sukari.
Kwa kuzingatia maelekezo haya, utaweza kutumia pressure cooker yako kwa usahihi ili kudumisha ubora wake kwa muda mrefu, na kuendelea kufurahia urahisi wake wa kupika aina mbalimbali za vyakula bila usumbufu.