Mapishi ya ugali ya mwiko mkubwa

Na Adeladius Makwega
22 Jun 2022
Ugali wangu ninaopika kwa mwiko mkubwa huwa una sifa kubwa tano: lazima uive, huwa hauna mabonge mabonge, chungu chake ninachopikia hakiungui na mwisho atayeuonja tu lazima ale tangu tonge la kwanza hadi mwisho.
article
  • Mwiko huwa na ufanisi mzuri wa kusonga ugali.
  • Mwiko huo hutumika wakati shughuli za watu ikiwemo misiba na harusi.
  • Kila nyumba inashauri kuwa nao.

Siku moja nilibanwa sana na njaa, kwa hiyo nilitafuta mboga yangu na kuichemsha haraka haraka jikoni, ilipoiva sikuiunga, niliichukua kama ilivyo nakuiweka kando ya jiko langu. 

Nikachukua sufuria na kuiweka maji jikoni, mara baada ya dakika kadhaa, maji haya yalichemka nakuweka unga katika sufuria hiyo iliyokuwa jikoni ili niusonge ugali.

Wakati nimeshaweka unga kwenye maji yalichemka nikaangalia mwiko wa kupikia ugali sikuuona kabisa, tafuta huku na kule mwiko siuoni, nikasema leo ninapika kwa kutumia nini? Kijiko na upawa wa chuma lakini vinashika moto na pia haviwezi kuukamata ugali vizuri.

Ninafanyaje? 

Akili yangu ilijiuliza mno, gafla mbele yangu kwenye kona na pahala ninapopika nikauona mwiko mkubwa, huku chini yake kukiwa na sufuria kubwa kadhaa za mapishi katika shughuli.

Nikauvuta huku ukipiga kelele,

Kwaaaaaaaaa!

 Nilipoutoa tu nikauosha haraka haraka na kuanza kuusonga ugali wangu.

Kwa kuwa mwiko huu ulikuwa mkubwa na ugali ulikuwa wangu mwenyewe basi mwiko huu wa kupikia sufuri la watu kama 100 uliukamata ugali vizuri na kuugeuza bila tabu na hata nilipokuwa nautumia kuusagasaga ugali ili kuondoa mabonge yenye unga ulifanya kazi hiyo vizuri sana.

Wakati naendelea kuusonga ugali huu, nikawa ninajiuliza huu mwiko wangu mdogo umekwenda wapi? Huu mwiko mkubwa ulifikajefikaje hapa?

Nilipata majibu kuwa mwiko mdogo pengine nimeutupa na uchafu. Mwiko mkubwa kuwepo hapa nyumbani kwangu nikakumbuka nikiwa kijana, bibi yangu mzaa baba anayeitwa Hedwiki Omari Binti Mkomangi aliniambia kuwa katika nyumba yako yoyote ile hakikisha unakuwa na mikeka mingi, sufuria kubwa na mifuniko yake na miko mikubwa kwa maana msiba, sherehe, ugonjwa na hata ugeni mkubwa nyumbani kwako ni dharura, 

Kimoyomoyo nikasema hapa akija mtu akanikuta ninavyousonga ugali wa mtu mmoja kwa mwiko wakupikia watu 100 atasema, “Katekista Makwega mbona unafanya israfu?”

Kwa hiyo ili somo la dharura la Binti Omari lilisababisha ninunue mwiko huo. Kumbuka nipo napika ugali msomaji wangu. Nikautenga ugali wangu nakuula polepole, bila tabu na ulikuwa ugali mtamu sana. Kwa hiyo tangu siku hiyo nikawa napikia ugali wangu kwa mwiko mkubwa hadi leo hii.

Ugali wangu ninaopika kwa mwiko mkubwa huwa una sifa kubwa tano kwanza lazima uive, pili huwa hauna mabonge mabonge, tatu chungu chake ninachopikia hakiungui hata wale mabingwa wa kula ukoko wanajinoma na tano na mwisho atayeuonja tu lazima ale tangu tonge la kwanza hadi mwisho.

Huo ndiyo ugali wangu, ninaopika kwa kutumia mwiko mkubwa. Je yupo anayediriki kushindana na mimi kupika kwa kutumia mwiko wake mdogo?

Ha ha ha ha ha ha ha, nicheke mwanakwetu, hayupo.

Labda mwanafunzi wangu hodari ambaye darasa hili la leo atafuzu, anaweza kushindana nami. Hata hivyo, huyo mwanafunzi wangu hodari (yeye) atabaki kuwa mwanafunzi tu na mimi kubaki kuwa mwalimu wake.

Mwanakwetu upo?

Mwandishi wa makala haya anapatikana mkoani Mwanza. Kwa mawasiliano unaweza kumpata kwa namba: 0717649257 au barua pepe: [email protected]

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa