Hakuna ambaye hufurahia harufu mbaya iwe ni kwenye mavazi, jikoni au kwenye vifaa vya nyumbani kama friji kama wengine wanavyopenda kuliita.
Fikiria tu umerudi zako nyumbani una hamu na kinywaji baridi au matunda alafu unafungua friji unakutana na harufu mbaya ikitoka kwenye kifaa hicho kinachosifika kwa kuhifadhi mahitaji ya nyumbani. Utajisikia vibaya!
Kwa baadhi ya watu tatizo hili limekuwa sugu kiasi kwamba hata wakiosha friji kwa zaidi ya mara moja, ndani ya saa chache harufu mbaya hurudi na kusababisha hata vyakula vilivyohifadhiwa humo kukosa harufu halisi na kupoteza ladha.
Ikiwa wewe ni mmoja wa wanaosumbuliwa na harufu mbaya inayotoka kwenye friji mbinu zifuatazo zinaweza kukusadia:
Viazi mviringo
Kwa wataalamu wa mapishi wanafahamu umuhimu wa viazi mviringo nyumbani. Mbali na kufanya pishi kuwa zito na kupunguza chumvi, viazi mviringo vinaweza kupunguza harufu mbaya kwenye friji lako na kuliacha likiwa na harufu nzuri.
Unachotakiwa kufanya ni kumenya viazi viwili au vitatu, kata saizi ndogo ndogo na uweke kwenye sahani au bakuli lililo wazi kwa muda wa saa 24.
Badilisha viazi kila siku ili kupata matokeo bora.
Baking soda
Matumizi ya baking soda ni mbinu nyingine inayoweza kukuepushia aibu ya friji kutoa harufu mbaya. Cha kufanya ni kumimina kiasi kidogo cha kiungo hiki kwenye sahani au chombo kilicho wazi na kuweka kwenye friji lako kwa saa 24 au zaidi.
Ukipenda unaweza kuongeza matone kadhaa ya mafuta ya kunukia au sabuni ya manukato ambayo yataondoa harufu mbaya ya kufanya friji lako inukie wakati wote.
Limao na chumvi
Mbali na kuongeza ladha kwenye chakula limao linaweza kuondoa tatizo la friji kutoa harufu mbaya ikiwa litachanganywa na kiasi kidogo cha chumvi na kwa matokeo zaidi unaweza kuongeza kiasi kidogo cha baking soda pia.
Osha limao au ndimu kata vipande vidogo vidogo, weka chumvi kiasi na baking soda kiasi kisha uweke kwenye friji kwa siku moja au zaidi, baada ya muda huo kupita harufu mbaya ya friji utaisikia kwa jirani tu.
Majani ya chai yaliyotumika
Baada ya kutumia majani ya chai, usiyatupe yahifadhi kwa ajili ya kunusuru friji yako na harufu mbaya.
Majani ya chai tunayoyazungumzia hapa ni yale yanayouzwa yakiwa kwenye vifuko vidogo maalum pamoja na kamba inayo muwezesha mtumiaji kutumia na kuyatoa au jina lingine (tea bags).
Majani haya yakiwa kwenye chombo cha wazi ndani ya friji lako kwa muda wa saa 24 au zaidi yanaweza kuondoa kabisa harufu mbaya na kuacha friji yako ikiwa na harufu nzuri.
Hakikisha unabadilisha majani kila baada ya siku nne mpaka tano.
Vanila
Kwa wale wanaotengeneza keki, mikate na vitafunwa vingine wanafahamu namna ambavyo vanila huongeza harufu nzuri ya kunukia kwenye mapishi yao. Basi hata kwenye friji vanila ina uwezo wa kuondoa harufu mbaya ya kuifanya friji yako inukie muda wote.
Utakachotakiwa kufanya ni kutengeneza viduara vidogo vya pamba na kuchovya kwenye vanila kisha kuweka kwenye chombo kilichowazi kwenye friji.
Wakati ukiendelea kutumia mbinu hizo kumbuka kusafisha friji lako angalau mara moja kwa wiki huku ukihakikisha mboga na michuzi haimwagiki hovyo hovyo kwenye friji.