Mbinu za kupika chapati laini za kusukuma

Na Lucy Samson
19 Oct 2022
Mbinu ya kwanza ni ya kuchagua aina bora ya unga wa ngano kwa sababu kuna aina nyingi za unga wa ngano.
article
  • Kupika chapati laini ni moja kati ya changamoto inayowakumba wapishi wengi.
  • Jambo la kufurahisha ni kwamba zipo mbinu zinazoweza kusaidia mapishi ya chapati hizo.

Moja kati ya sifa kubwa ya chapati ya kusukuma ni muonekeno mzuri (umbo la duara) ladha na ulaini wa kitafunwa hicho.

Sifa hizo zina uwezo wa kukufanya uwe mpishi bora wa chapati mtaani au nyumbani au ukaendelea kupoteza walaji wa kitafunwa hicho usipotilia mkazo sifa hizo.

Hata hivyo, kupika chapati laini ni moja kati ya changamoto kubwa  inayowakumba wapishi wengi wa kitafunwa hicho.

Jambo la kufurahisha ni kwamba zipo mbinu zinazoweza kusaidia mapishi ya chapati laini, mchambuko zitakazopendwa na kusifiwa na kila mtu.

Upishi wa chapati laini hautofautiani sana na ule wa chapati za kawaida, cha kufanya ni kuongeza ujuzi kidogo.

Mbinu ya kwanza ni ya kuchagua aina bora ya unga wa ngano kwa sababu kuna aina nyingi za unga wa ngano. Ili kufanikisha chapati laini hakikisha unapata unga wa ngano wa  chapati wengine wanaita ngano ya chapati.

Ukishanunua aina hiyo ya unga, mbinu ya pili ya kupata chapati laini ipo kwenye kuchanganya ngano na kukanda.

Wakati wa kuchanganya unga tumia siagi au mafuta ya kupikia pamoja na vitu vingine kama chumvi, sukari kiasi kwa wanaopendelea na maji ya vuguvugu  kiasi kisha uanze kukanda.

Kwenye hatua ya ukandaji kanda mpaka unga uwe laini kisha funika kwa muda wa dakika 30 mpaka saa moja kisha ukate madonge kwa ajili ya kusukuma.

Kuacha unga wa  ngano uliokandwa kwa muda mrefu kabla ya kusukuma hufanya mafuta kuchanganyika na ngano vizuri hivyo kufanya unga kuwa   laini.

Kwa wale wanaotaka chapati mchambuko basi ukishakata madonge yako usisukume moja kwa moja na kuanza kuchoma. Zisukume upake mafuta na uzitengenezee duara kama inavyoonekana hapo chini.

Wakati wa kutengeneza madonge hakikisha unapaka mafuta au siagi ya kutosha kisha unaacha kwa dakika tano hadi 10 kabla ya kuzisukuma na kuchoma. Picha | Jinsi ya kupika/Facebook.

Mpaka hapo sasa unaweza kuanza kusukuma taratibu huku kutengeneza shepu ya duara kisha choma chapati zako  kwa moto mdogo.

Rudia hatua hii kwa ngano iliyobaki  na chapati zako itakuwa tayari. 

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa