Microwave: Mbinu mbadala ya kukaanga karanga

Na Herimina Mkude
2 Feb 2022
Unachohitaji kupika karanga kwa njia hii ni microwave, sahani ya kuhimili joto la microwave, karanga, maji na chumvi.
article
  • Unachohitaji ni microwave, sahani, karanga, maji na chumvi.
  • Hakikisha unaiseti microwave yako kwenye joto la wastani.
  • Gawa dakika tano kwa awamu yaani mbili, mbili moja.

Dar es Salaam. Yawezekana umezoea kutumia microwave kwenye shughuli za kupasha tu chakula na vinywaji kama chai au kahawa. Leo nitakupa moja ya maujanja ambayo unaweza ukayafanya kwa kutumia kifaa hicho kinachotumia umeme.

Ujanja huu utakusaidia hasa ‘bachela mwenzangu ‘kusave’ zile pesa unazozitumia kila siku kununua karanga. Iwe ni mia mbili na hata jero.

Zingatia kuwa, hapa nazungumzia karanga zile za kawaida, tuziache zile zenye ‘mbwembwe’ nyingi kama zile za mayai na unga wa ngano. Hizo tutaziangalia siku nyingine.

Unachotakiwa kufanya ni kununua karanga mbichi, na hazina gharama sana, kwa Dar es Salaam zinauzwa hadi shilingi 2,600 kwa kilo (bei inaweza tofautiana kulingana na aina ya karanga na soko unalonunulia).

Sio lazima ukaange kilo nzima kwa siku moja, unaweza ukakaanga robo, na nyingine ukatumia siku nyingine.

Kama una wageni, hapo itabidi tu upambane kulingana na mahitaji yao.

Karanga zinapatikana kwa gharama ya Sh 2,600 kwa kilo moja. Picha| Rodgers George.

Tuingie ujanjani

Uandaaji wa karanga hauna mambo mengi, vitu muhimu vinavyohitajika ni chumvi, maji pamoja na sahani ambayo inahimili joto la microwave hadi karanga zitakapoiva.

Vyombo vingi vya udongo vinafaa kutumika kwenye microwave lakini kwa vyombo vya plastiki, chonde! hakikisha kina nembo ya kuidhinisha matumizi yake kwenye microwave (microwave safe).

Hatua ya kwanza, Chambua karanga zako kutoa maganda na karanga zingine ambazo zinaweza kuwa zimeoza au kuharibika, Kisha chukua karanga na uziweke kwenye chombo ambacho utakitumia kwenye microwave.

Baada ya hapo, chukua maji kidogo na chumvi kiasi upendacho na uvikoroge kwenye kikombe.

Chumvi ikiyeyuka, chukua mchangayiko huo na unyunyize kwenye chombo chenye karanga, kisha changanya  ili karanga zipate chumvi vizuri. 

Hatua inayofuata ni kuziweka karanga kwenye microwave, kwenye hatua hii hakikisha ‘hauset’ muda mrefu ili karanga zisiungue.

Kwa kawaida inaweza kuchukua dakika tano za joto la wastani (medium heat) hadi karanga kuiva.

Unapoweka karanga kwenye microwave, usizipike kwa dakika tano mfurulizo. Gawa dakika hizo. Picha Rodgers george.

Unachotakiwa kufanya ni ‘kuset’ dakika mbili mara ya kwanza, zikiisha angalia karanga zina hali gani. Namaanisha uonje na uchanganye.

Kama  hazijaiva, ‘set’ tena dakika mbili, nazo zikipita onja kama karanga zimeiva vile unataka.

Unaweza ‘ukaset’ tena dakika moja kama unapenda karanga zako ziwe zimeiva  vizuri. Hadi hapo karanga zako zipo tayari kwa kurushwa ‘pangoni’.

Usijibane sana, jimiminie hata juisi glass moja ya kushushia karanga zako.

Faida ya kutumia ujanja huu ni pamoja na kutokukulazimu kukaanga karanga kwa kutumia mchanga kwenye majiko ya nishati zisizo safi kama mkaa na kuni.

Uwe kwenye getto lako, unachohitaji ni microwave tu kutengeneza kichangamsha meno cha aina hii.

Vilevile, itakusaidia kutokuunguza karanga, kwa sababu sio wote tunaweza kaanga vizuri karanga kwenye majiko ya gesi lakini nnitakuja na mbinu hiyo pia siku za usoni. 

Mimi maujanja nimeshakupa kazi kwako unaemiliki microwave.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa