Namna ya kupunguza chumvi iliyozidi kwenye chakula

Na Esau Ng'umbi
26 Sept 2022
Unaweza kutumia kiazi mviringo, maziwa au limao, maji.
article
  • Unaweza kutumia kiazi mviringo, maziwa au limao.
  • Wataalamu wa afya waonya chumvi ikizidi inaweza kusababisha magonjwa ya moyo.

Chumvi ni kiungo pendwa kwa mapishi. Hukifanya chakula kiwe na ladha zaidi na cha kuvutia. Asilimia kubwa ya vyakula vya kupikwa huwekwa chumvi moja kwa moja ingawa vipo baadhi ya vyakula ambavyo si lazima chumvi iwekwe wakati wa kupika.

Pata picha umezidisha chumvi wakati ukipika pishi lako ambalo limekugharimu muda, pesa pamoja na ubunifu wako mwingi. Usihofu kwa sababu hakuna lisilowezekana. 

Tumia njia hizi  kupunguza kupunguza chumvi iliyozidi wakati unapika chakula:

Kiazi  Mviringo

Ndiyo! inapotokea umezidisha chumvi basi fikiria kuhusu kiazi mviringo kwa sababu kina uwezo wa kunyonya  kiasi cha chumvi kinapowekwa kwenye chakula.

Unachotakiwa kufanya ni kukata vipande vidogo na kuacha vichemke pamoja na chakula chenye chumvi iliyozidi kwa muda wa dakika 15 hadi 20.

Kiazi mviringo hunyonya maji pia kwa hiyo unatakiwa kuwa mwangalifu kama unahitaji chakula chako kiwe na mchuzi basi unaweza kuongeza maji kidogo.

Maziwa

Maziwa ni mojawapo ya njia nzuri ya kupunguza chumvi iliyozidi. Ingawa kwa kiasi fulani yanaweza kuathiri baadhi ya viungo lakini ni chaguo zuri kwani pamoja na kupunguza chumvi unapata virutubisho vya ziada.

Unaweza pia kutumia tui la nazi au mtindi wa maziwa kama mbadala wa maziwa.

Maji

Hii ndiyo njia rahisi zaidi na ya haraka ya kupunguza chumvi iliyozidi kwenye chakula. Unaweza kuongeza kiasi cha maji kulingana na wingi wa chumvi iliyopo na kuacha chakula chako kichemke kwa muda, ingawa tarajia kupungua kwa ladha ya baadhi ya viungo.

Limao

Maji ya limao yana kiwango kikubwa cha asidi ambayo inaweza kusaidia kupunguza kiwango cha chumvi iliyozidi. 

Hata hivyo, njia hii  haishauriwi katika chakula ambacho kiwango cha chumvi kilichozidi ni kikubwa.

Maji ya limao yana uwezo mkubwa wa kuweka uwiano wa chumvi sawa kutokana na wingi wa asidi. Picha | Wikipedia.

Kwa mujibu wa jarida la vyakula la Fsr la nchini Marekani, watafiti wake  wamebaini kuwa maji ya limao yanaweza kupunguza kiwango cha chumvi iliyozidi kwa asilimia 75.

Kuongeza kiwango cha viungo au chakula

Ikiwa mazingira yana ruhusu kuongeza kiwango cha chakula au viungo unaweza kufanya hivyo ili kupata uwiano wa chumvi ya wastani unaotakiwa kwenye chakula.

Mathalan, unaweza kuongeza mbogamboga kwenye chakula kama wali, ambazo zitasaidia kufyonza chumvi iliyozidi na kuongeza ladha kwenye chakula.

Pamoja na mbinu hizo wataalamu wa afya wanashauri kwamba ni muhimu kuwa makini na kiwango cha chumvi tunachoingiza mwilini kwani kinapozidi husababisha magonjwa ya moyo pamoja na shinikizo la damu.

Kwa  Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mtu mzima anatakiwa kutumia kiwango cha chumvi kisichozidi gramu tano kwa siku ili kupunguza shinikizo la damu na hatari ya kupata magonjwa ya moyo.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa