Vitumbua kuku: Pishi maalum la siku ya wapendanao 

Na Lucy Samson
14 Feb 2023
Usilolijua ni kwamba unaweza kuandaa chakula cha tofauti nyumbani na ukawafurahisha uwapendao bila kuingia gharama kubwa.
article
 • Pishi hili linaweza kuwa mbadala wa mtoko wa siku ya wapendanao.
 • Utakachohitaji ni mazingira mazuri na kinywaji baridi cha kusindikiza mlo huo.

Sikukuu ya wapendanao maarufu kama “Valentine Day” huwa na shamra shamra nyingi kwa wapendanao ikiwemo kutoka ‘out’ kwa ajili ya kupata chakula chenye ladha ya tofauti na vile tulivyovizoea.

Wengine hupendelea kutembelea migahawa maarufu yenye chakula kizuri ambapo hutoboa mifuko yao zaidi ili kuweza kufurahia vyakula hivyo.

Usilolijua ni kwamba unaweza kuandaa chakula cha tofauti nyumbani na ukawafurahisha uwapendao bila kuingia gharama kubwa.

JikoPoint (www.nukta.co.tz)  tumekuandalia maujanja ya kuandaa vitumbua vya kuku unavyoweza kuvipika ukiwa nyumbani na kunogesha upendo mtu wako wa karibu.

Cha kufanya ili kujipatia ujuzi huu ni  kufuatana nasi mpaka mwisho.

Tomato au chachandu ya aina yoyote ile inaweza kunogesha pishi hili la vitumbua vya kuku na kukupa ladha ya kihistoria. Picha |Eating the World

Mahitaji

 • Nyama ya kuku robo
 • Pilipilimanga robo kijiko
 • Binzari ya unga nusu kijiko
 • Giligiliani robo kijiko
 • Chumvi robo kijiko
 • Maji ya ndimu kijiko kimoja
 • kitunguu maji
 • Kitunguu swaumu
 • Karoti na Hoho.

Maandalizi

Hatua ya kwanza kabisa ya kupika pishi hili ni kuandaa kuku. Hakikisha unatumia nyama ya steki isiyo na mifupa kisha osha vizuri na ukatekate kwa saizi ndogo.

Baada ya hapo washa jiko, bandika sufuria yenye maji kiasi na uweke vipande vya kuku, pilipili manga nusu kijiko, binzari ya unga nusu kijiko, giligiliani  ya unga nusu kijiko, chumvi nusu kijiko na maji ya ndimu kijiko kimoja kisha ufunike na uache iive.

Nyama ya kuku ikiiva hatua inayofuata ni kutengeneza mchanganyiko mzito kwa ajili ya kuchoma vitumbua. Hapa utahitaji blenda au food processor ( ili kusaga nyama ya kuku na kuchanganya viungo.

Andaa blenda kisha weka vipande vya kuku na mayai matatu na usage kwa dakika tatu au zaidi mpaka uhakikishe nyama imesagika vizuri na kutengeneza mchanganyiko mzito.

Ikiwa bado unaona nyama ni kavu unaweza kuongeza yai moja, hakikisha mchanganyiko hauwi mwepesi sana.

Baada ya kujiridhisha weka mchanganyiko wako kwenye bakuli, ongeza hoho, karoti, vitunguu maji, na ‘baking powder’ kisha ukoroge vizuri.

Ukimaliza bandika kichomeo cha cha vitumbua  jikoni kisha uchome kwa moto mdogo mdogo mpaka upande mmoja uive.

Upande mmoja ukiiva geuza na upande mwingine, kisha uepue tayari kwa kuliwa.

Utakachohitaji ili kuifanya siku hii iwe maalum na mlo huu ni kutafuta eneo zuri na tulivu na kinywaji kitakachosindikiza mlo huu.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa