Pilipili ya nanasi: Maandalizi hadi kuitumia kwa chakula

Na Lucy Samson
21 Oct 2022
Pilipili ni kiungo muhimu chenye kuongeza ladha na hamu ya kula (appetite).
article

Pilipili ni kiungo muhimu chenye kuongeza ladha na hamu ya kula (appetite) kwenye chakula.

Kumekuwa na ubunifu mbalimbali unaofanyika kwenye kiungo hicho kuhakikisha kinakuwa na ladha tofauti tofauti kuendana na haja ya mlaji.

Aina ya pilipili inayozungumziwa hapa ni ile inazosagwa na kuwa katika hali ya kimiminika. Inaweza kuwa ya ladha ya embe, limao, ukwaju, ubuyu na nyingine nyingi.

Leo tujifunze jinsi ya kutengeneza pilipili yenye ladha ya nanasi.

Maandalizi

Hatua ya kwanza baada ya kununua mahitaji ya aina hii ya pilipili ni kuosha na kumenya nanasi. Kama unatengeneza kiasi kidogo cha pilipili unaweza kununua vipande vya nanasi vinavyouzwa vikiwa vimeshakatwa katwa.

Tutatumia vipande vichache vya nanasi ili utamu wa tunda hilo usizidi kiasi cha pilipili ulizonazo.

Mimi leo nimetumia vipande viwili vya nanasi huku kwetu vinauzwa Sh1,000.

Ukimaliza kuandaa nanasi osha, menya na ukatekate nyanya, kitunguu, karoti hoho kwa saizi kubwa kiasi. 

Washa jiko na uvichemshe kwa dakika tano kisha uache vipoe.

Vikipoa weka vipande vya nanasi, nyanya, karoti, hoho, kitunguu na pilipili kwenye blenda na usage mpaka vilainike.

Ukimaliza kusaga weka mchanganyiko kwenye sufuria yenye mafuta kiasi kulingana na wingi wa pilipili yako kisha uache uchemke.

Ukichemka mimina mchanganyiko wako kenye sufuria. Ongeza  maji kiasi ili mchanganyiko wako usiwe mzito sana.

Baada ya hapo ongeza chumvi, maji ya limao na kiungo cha mchuzi kama unapendelea.

Baada ya hapo pilipili yako itakuwa tayari unaweza kuiweka kwenye chupa za plastiki kwa ajili ya kuuza  au kwa matumizi ya nyumbani.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa