Sababu zinazochangia watoto wadogo kupoteza hamu ya kula 

Na Lucy Samson
8 Mar 2023
Mtoto akila mlo mmoja kwa muda mrefu ni rahisi kuuchoka na kusababisha kupoteza kabisa hamu ya kula.
article
  • Wataalamu wa lishe wasema kula mlo mmoja kwa muda mrefuna ulishaji usiofaa  huchangia hamu ya kula kupotea
  • Mbinu shirikishi wakati wa kula zitasaidia kuondoa tatizo hilo

Ukikaa na wazazi au walezi wa watoto wadogo hutaacha kusikia habari na malalamiko juu ya watoto wao kusumbua kula.

Wengine watoto wao hupoteza kabisa hamu ya kula, jambo linalochangia kupungua uzito na kushambuliwa na magonjwa.

Wataalamu wa lishe wanashauri mtoto kuanza kupewa chakula cha ziada anapofikisha miezi sita, na kuendelea kuongezewa kipimo kadri anavyozidi kukua.

Katika kipindi hicho wazazi na walezi hutafuta njia mbadala kuhakikisha mtoto wao wanakula vizuri ikiwemo kuongeza ndimu au barafu kwenye chakula, kuwatisha na kuwalazimisha kula.

Wakati mwingine njia hizo zinakuwa hazileti matokeo mazuri na hapo ndipo wazazi hupata msongo wa mawazo na wasijue nini cha kufanya.

Kwa mujibu wa mwongozo wa utoaji huduma ya lishe kwa watoto wadogo ulioandaliwa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), zipo sababu mbalimbali zinazoweza kusababisha mtoto kupoteza hamu ya kula ikiwa ni pamoja na kupewa vinywaji vingi.

Mwongozo huo unasema ikiwa mtoto kuanzia umri wa miezi sita mpaka miaka mitano atapewa kiasi kikubwa cha kinywaji chenye asili ya  maji maji ni rahisi tumbo lake kujaa gesi hivyo kijikuta anapoteza kabisa uwezo wa kula.

Kwa watoto wenye umriwa miaka miwili mpaka mitano wataalamu wa lishe wananshauri kuwaruhusu wale wenyewe cni ya uangalizi wa wazazi au walezi.Picha|Gettyimage.

Kutokubadilishwa kwa mlo 

Mtaalamu wa lishe kutoka TFNC, Dorice Kitana anasema mtoto akila mlo mmoja kwa muda mrefu ni rahisi kuuchoka na kusababisha kupoteza kabisa hamu ya kula.

Ni kawaida kuona wazazi au walezi wakitengeneza unga wa lishe kwa ajili ya kuandaa uji ambao kwa jamii nyingi ndiyo chakula kikuu cha watoto kuanzia miezi sita na kuendelea ambacho hupewa kwa muda mrefu bila kubadilishwa.

“Kama tulivyo watu wazima kila siku tunatamani kula kitu kipya, hata watoto ni hivyo hivyo wanachoka kula aina moja ya chakula,” anasema Kitana

Mbinu za ulishaji sizizofaa

Mwongozo wa TFNC, unasema ni vyema wazazi kutumia mbinu shirikishi wakati wa kuwalisha watoto, kitendo cha mzazi kumkaba mtoto, kumlazimisha kula kunamfanya mtoto achukie muda wa kula, hivyo kijikuta akipoteza hamu ya kula.

“Ulishaji shirikishi ni ule ambao mtoto anasaidiwa na kuhimizwa kula katika mazingira ya furaha na upendo. Pia wazazi na walezi watengene muda wa kutosha kwa ajili ya kuwalisha watoto,” unasema mwongozo huo.

Tumia mbinu hizi kumsaidia mtoto kupata hamu ya kula

Ikiwa mtoto wako anasumbuliwa na tatizo la kupoteza hamu ya kula na hujui namna ya kuzuia tatizo hilo, usijali hizi hapa ni mbinu zinazoweza kukusaidia.

Mbinu shirikishi ya ulishaji wa mtoto inahusisha pia mchango wa wazazi au walezi wote wawili.Picha|istock.

Badilisha mlo wa mtoto mara kwa mara

Mwongozo wa lishe wa TFNC unasema mtoto anatakiwa apate angalau makundi mawili ya chakula kwenye kila mlo.

 Makundi  hayo ni pamoja na Vyakula vya nafaka, mizizi na ndizi vinavyohusisha mahindi, mchele, mtama, ulezi, ngano, uwele, viazi vikuu.

Vyakula vya jamii ya kunde na vyenye asili ya wanyamaikiwemo kunde, karanga, soya,nyama, samaki, dagaa, maziwa, na maayai.

Makundi mengine yanayoshauriwa  ni pamoja na mbogamboga na matunda ambayo ni chanzo cha vitamini ikiwemo vitamini C.

Dorice Kitana anasema kubadilisha mlo wa chakula kutafanya mtoto awe na hamu ya kula akijua kwenye kila mlo kuna ladha mpya inaongezeka.

Tumia mbinu shirikishi wakati wa kumlisha mtoto

Mbinu shirikishi za kumlisha mtoto  zinahusisha kumlisha mtoto akiwa mwenye furaha, kumhimiza kula kwa upendo.

Pia kaa naye karibu wakati wote wa kula, zungumza  naye  na tenga muda wa kutosha wakati anapata chakula.

“Watoto wasilazimishwe kula haraka wala kutishiwa hiyo itawafanya wachukie muda wa kula na kupoteza kabisa hamu yao ya kula,” ameongeza Katana.

Ikiwa tatizo la kupoteza hamu ya kula litakuwa sugu, Katana anashauri ni vyema kumfikisha mtoto kituo cha afya achunguzwe afya yake.

“Wakati mwingine  watoto hupata mikwaruzo kinywani, mashambulizi ya bakteria au magonjwa mengine kwa hiyo ni  vyema apelekwe hospitali,” ameongeza mtaalam huyo wa lishe.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa