Tumia vyakula hivi kupunguza ukavu ukeni

Na Lucy Samson
16 May 2024
Tatizo hili linapompata mwanamke huwa linampa maumivu na kumfanya apoteze hamu ya tendo la ndoa jambo linaloleta mgogoro katika mahusiano.
article
  • Ni pamoja na parachichi, mafuta ya samaki na mboga mboga.
  • Wataalamu wa afya waeleza sababu, wasema tatizo hili linatibika.

Ukavu ukeni ni miongoni mwa matatizo ya kiafya yanayotajwa kugharimu afya na furaha za wanawake hususani  wanaposhiriki tendo la ndoa.

Tatizo hili linapompata mwanamke huwa linampa maumivu na kumfanya apoteze hamu ya tendo la ndoa jambo linaloleta mgogoro katika mahusiano.

Baadhi ya wanawake hukimbilia kutumia njia mbadala ambazo zinaweza kuhatarisha afya ya uke ambayo mara nyingi bidhaa zinazotumika kulainisha uke huharibu bakteria wanaolinda uke na kusababisha magonjwa mengine kama fangasi.

Chanzo ni nini? 

Mtaalamu wa Lishe wa kujitegemea Sophia Lugome kutoka jijini Mwanza anasema kuwa mara nyingi ukavu ukeni husababishwa na mabadiliko ya vichocheo mwilini hususani kwa wanawake waliokoma kuona siku zao (Menopause).

Nayo tovuti ya masuala ya afya ya Medical News Today ya nchini Marekani inabainisha kuwa tatizo hilo pia linaweza kuwapata wanawake wa rika zote hata mabinti ambao wameshavunja ungo huku ikitaja upungufu wa homoni ya estojeni kama chanzo.

“Ukavu ukeni unasababishwa na kiwango kidog ocha homoni ya estojeni ambayo inahusika na kulainisha uke na kuufanya uwe nyumbufu,” imesema tovuti hiyo.

Wakati baadhi ya watu wakikimbilia kutumia vilainishi, Daktari Zabron Mbatiya kutoka Hospitali ya Kairuki ya jijini Dar es Salaam anasema kuwa tatizo hilo linalweza kutibika kwa vyakula na matunda ambayo yataongeza kinga mwilni na kuzalisha bakteria walinzi ukeni.

Kwa mujibu wake, baketria hao walinzi hufanya kazi ya kulinda uke na mashambulizi ya bakteria wageni pamoja na kuzalisha unyevu unyevu unaotakiwa.

Ikiwa wewe ni miongoni mwa wanokutana na tatizo hili nukta habari imekuandalia vyakula vinayoweza kuwa suluhu ya ukavu ukeni.

Mboga na matunda huupa mwili virutubisho vya kutosha vinavyoweza kukusaidia kutibu ukavu ukeni.PichaFichuo.
  1. Parachichi

Miongoni mwa matunda yanayoweza kutumiwa kuongeza ute ute ukeni ni parachichi ambapo tovuti ya masuala ya afya ya Bonafide inabainisha kuwa tunda hili lina utajiri wa mafuta na vitamini  muhimu kwa ngozi, kama vile vitamini E, vitamini B6, beta-carotene, ambavyo husaidia kulainisha uke na kudhibiti viwango vya estrojeni.

  1. Mafuta ya samaki

Wataalamu wa afya wanasema kuwa mafuta ya samaki ikiwemo salmoni, ambayo ni chanzo kikuu cha mafuta omega-3, ambayo huongeza unyevu wa ngozi na maeneo mengine mwilini. 

“Utafiti mmoja uligundua kuwa wanawake baada ya kumaliza hedhi ambao waliongezea 3.5 gramu za asidi ya mafuta omega-3 kila siku walipata maboresho katika ukavu wa uke kwa miezi sita,” imesmea tovuti Bonafide.

Matumiz ya vyakula hivi hayatofautiani na yale ya kawaida.Picha|Daudi Mbapani
  1. Viazi vitamu

Mbali na utamu wa chakula hiki, kinaweza pia kutumika kutibu tatizo la ukavu ukeni. Tovuti ya Bonafide inabainisha kuwa chakula hiki kina beta-carotene, kichocheo cha vitamini A  kwa wingi ambayo inahitajika kwa wingi mwilini.

 “Kiazi kitamu kimoja kilichopikwa bila kumenya maganda huatoa mara sita ya beta-carotene zaidi ya ile inayohitajika kwa siku. Hii inaweza kuwa njia nzuri ya kuondoa ukavu wa ukeni,” imesema tovuti hiyo,

  1. Mboga mboga

Daktari Mbatiya ameiambia Nukta habari kuwa mboga mboga ikiwemo brokoli na koli flawa, pilipili hoho zina virutubisho vingi ambavyo huongeza kinga ya mwili ambayo huwapa nguvu bakteria wazuri waliopo ukeni kupambana na vimelea vya magonjwa vinavyosababisha ukavu.

“Vyakula au mboga za majani kama koli flawa wanawawezesha wale bakteria ambao tunawaita ‘normal flora’ waweze kuwepo ili kuhakikisha unyevu unyevu wa ukeni unakuwepo,” amesema Dk. Mbatiya.

Aidha, Daktari Mbatiya amesema kuwa endapo utahisi ukavu usio wa kawaida unaoambatana na maumivu makali ni vyema kutembelea kituo cha afya kwa ajili ya matibabu zaidi.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa