Umuhimu wa kunywa maji ya moto asubuhi

Na Lucy Samson
24 Sept 2022
Mbali na kupunguza mafuta mwilini maji ya moto yanaweza kupunguza msongo wa mawazo, magonjwa ya moyo na choo kigumu.
article
  • Mbali na kupunguza mafuta mwilini maji ya moto yanaweza kupunguza msongo wa mawazo, magonjwa ya moyo na choo kigumu. 
  • Wataalamu wa afya wanashauri matumizi ya maji ya moto yaende sambamba na mazoezi.
  • Zingatia kiwango cha joto wakati wa kutumia kinywaji hicho.

Baadhi ya watu husema unywaji wa maji ya moto umewasaidia kupunguza vitambi na unene, huku wengine wakitibu maumivu ya viungo na uchovu kwa kutumia kinywaji hicho.

Kunywa maji ya moto asubuhi kunaweza kupunguza unene na vitambi, wengine wanasema si vema kula chakula kabla hujatanguliza  kitu cha moto tumboni wakati wa asubuhi.

Najua unajiuliza ukweli wa jambo hili ni upi?. Tiririka nami mpaka mwisho wa makala hii ujifunze umuhimu wa kinywaji hiki.

Daktari George Munisi, Mtaalamu wa Chakula na Lishe anasema unywaji wa maji ya moto wakati wa asubuhi unasaidia sana kuamsha mfumo wa mmeng’enyo wa chakula.

“Kuna vitu vinaitwa vichocheo vya mfumo wa chakula, unapokunywa maji ya moto wakati wa asubuhi unavisaidia kufanya kazi katika efficient (ufanisi),” anasema Dk Munisi.

Maji ya moto hupunguza mafuta mwilini

Wataalamu wa masuala ya chakula na lishe wanasema kuna uhusiano kati ya unywaji wa maji ya moto na kupungua kwa mafuta mwilini.

“Unapotumia maji ya moto wakati wa asubuhi yanaenda kuyeyusha mafuta yaliyojikusanya kwenye utumbo kwa kiasi fulani,” anasema Dk George.

Mbali na maoni ya mtalaam huyo, tovuti ya habari za afya ya Healthline imetaja manufaa mengine ambayo mtu anaweza kuyapata endapo akinywa maji ya moto wakati wa asubuhi mbali na kupunguza uzito na unene.

Kupunguza hatari ya kupata choo kigumu (Constipation)

Jarida hilo linafafanua kuwa upungufu  wa maji mwilini husababisha chakula kujikusanya kwenye utumbo mpana kabla ya kutoka nje kama haja kubwa.

Hivyo unywaji wa maji ya moto wakati wa asubuhi utakuweka kwenye nafasi nzuri ya kuepuka changamoto ya kupata choo kigumu.

Huimarisha mzunguko wa damu mwilini

Kuanza siku yako na maji ya moto huuakikishia mwili mzunguko mzuri wa damu ambao utakuweka kwenye nafasi nzuri ya kuepuka magonjwa ya moyo.

Kupunguza msongo wa mawazo

Kwa mujibu wa  tovuti ya habari za kitabibu Medical News Today, kunywa vinywaji vya moto asubuhi kama chai, kahawa na maji ya moto kunaweza kupunguza msongo wa mawazo na wasiwasi

“Kikombe kimoja cha maji ya moto asubuhi kinaweza kupunguza msongo wa mawazo,” inaeleza tovuti hiyo.

Maji ya moto huondoa sumu mwilini

Wataalamu wa afya wanasema maji ya moto huufanya mwili utokwe jasho hivyo kuna nafasi kubwa ya kupoteza sumu mwilini ambazo hutoka kwa njia ya jasho na mkojo.


Tangazo


Cha kuzingatia wakati wa kunywa maji ya moto

Japo kuna uhusiano kati ya kunywa maji ya moto na kupunguza mafuta mwilini, uhusiano huo sio wa moja kwa moja hivyo ni vyema mtu afanye shughuli nyingine ikiwemo mazoezi.

“Inabidi utumie maji ya moto na vitu vingine ambavyo vitaongeza matumizi ya nishati ya mwili kama mazoezi, au kufanya shughuli yoyote wakati wa asubuhi,” anasema Dk Munisi.

Angalizo lingine ambalo wataalamu wa afya wanalisisitiza ni unywaji wa maji ya moto yanayoweza kuunguza mdomo, ulimi na koromeo.

Tovuti ya Healthline inashauri maji yasiwe ya moto kiasi cha kumuunguza mnywaji.

“Onja kiwango cha joto cha maji yako kabla hujameza maji mengi kwa wakati mmoja,” inasema tovuti hiyo. 

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa