Vifaa hivi visikose katika jiko lako

Na Fatuma Hussein
3 Dec 2024
Vifaa hivi ni muhimu zaidi kuwa navyo katika jiko ili kurahisisha mapishi.
article

Vifaa hivi visikose katika jiko lako

  • Vifaa hivi ni muhimu zaidi kuwa navyo katika jiko ili kurahisisha mapishi.
  • Nunua vifaa vyenye uwezo wa kufanya kazi zaidi ya moja.
  • Mwiko na sufuria ni muhimu zaidi kuwa navyo kwa wingi.

Dar es Salaam. Kila mtu ana vifaa ambavyo huwezi kuvikosa katika jiko lake ili kurahisa mapishi ya kila siku.

Ni vyema kufahamu kuwa uchaguzi wa vifaa una nafasi kubwa ya kufanikisha shughuli za jikoni hasa zinahusu mapishi. 

Vipo vifaa ambavyo havitakiwi kukosa katika jiko lako kwa sababu uwepo hukumalisha kazi nyingi kwa wakati mmoja. Ni vifaa gani hivyo? 

Jokofu (fridge)

Jokofu ni kifaa muhimu kwa ajili ya kuhifadhi vyakula vinavyoharibika haraka kama maziwa, mayai na nyama.. Ili kuhakikisha chakula kipo salama, inashauriwa kuwa na hali joto ya wastani ambayo itazuia chakula kisiharibike. 

Ili kuongeza ufanisi wa jokofu lako, panga kuhifadhi vyakula vinavyohitaji kutumika mapema kwenye rafu ya juu, huku vyakula vinavyoweza kudumu muda mrefu vikihifadhiwa kwenye rafu za chini ambazo zina baridi kali. 

Kagua jokofu lako mara kwa mara ili kuhakikisha vyakula vyote viko safi na salama kwa matumizi. 

Jokofu si tu kwamba linasaidia kuhifadhi chakula kikiwa safi, lakini pia linawezesha kuhifadhi vyakula kama jamu, michuzi na achali ambavyo vinaweza kudumu muda mrefu zaidi. 

Jokofu lililopangwa vizuri na la mtindo ambalo litaweka vyakula na vinywaji safi kwa muda mrefu zaidi.Picha / Appliances online.

Microwave (Kipashia chakula)

Microwave hutumika kwa ajili ya kupashia chakula. .

Kazi nyingine ya microwave ni kupika, kuoka, kuchoma, kuchemsha na kuanika vyakula bila hitaji la vifaa vingine jikoni, kusafisha vifaa vya jikoni, kuongeza maji kwenye matunda, kuyeyesha baadhi asali iliyoganda na  kufanya hamira imuuke kwa haraka.

Ukiwa na kifaa hiki katika jiko lako kitakupata faida lukuki za mapishi. Kama mfuko unaruhusu, nunua microwave. 

Muonekano wa chakula katika kipashia chakula ,pia unaweza kupasha chakula aina yoyote . Picha / Appliances online.

Kisu

Kisu ni kifaa muhimu katika jiko ambacho hutumika kukata na kuandaa vyakula mbalimbali. 

Kisu sio tu katika upishi pia hutumika katika kurahisha kazi mbalimbali kama kuchonga mbao, kufungulia mifuniko migumu ya madumu ama kukata kamba na vitu vingine.

Kisu hutumika kukata viamba upishi mbalimbali kama nyanya, pilipili mboga, vitunguu, kukata nyama mkate na hata kupaka ‘jam’ (vyakula ambavyo hutengenezwa maalumu kwa lengo la kupaka vitafunwa) kwenye vyakula.

Ukiachia matumizi yake pia kuna aina za visu zaidi ya 15 ambazo hutumika jikoni kulingana na matumizi mbalimbali.

Kuna kisu cha Mpishi (Chef knife), kisu cha matumizi (Utility knife) kisu cha kukata nyama (Cleaver), kisu cha kukatia mkate (Bread knife) pamoja na kisu cha mchinjaji ambacho mara nyingi hutumika katika mabucha ya nyama.

Kuna aina zaidi ya 15 ya visu ambavyo hutumika kuanda vyakula , matunda na mbogamboga . Picha / Epicurious.

Sufuria

Sufuria ni chombo ambacho kinatumika kila siku katika mapishi mbalimbali hivyo ni vyema kununua sufuria bora ambazo zinadumu kwa muda mrefu, nzito haziunguzi kwa urahisi na ziwe za kuvutia. 

Matumizi makubwa ya sufuria jikoni ni kupika chakula, kuchemsha vitu kama vile maziwa, chai au maji, pamoja na kuhifadhi vyakula vikiwa jikoni kabla ya kuliwa.

Kuna aina nyingi za masufuria: Nyepesi na nzito, vioo pamoja na sufuria zisizoshika chakula.

Hivyo, wakati unazitumia sufuria hakikisha ukimaliza unaziosha vizuri kisha unazitunza. 

Sufuria hizi ni nzuri na haziitaji matunzo makubwa kama sufuria za kawaida . Picha / Granite sufuria set.

Kikaango (frying pan)

Hiki ni kifaa ambacho ukiwa mpishi huwezi kukwepa kuwa nacho. Kifaa hiki hutumika kwa kukaanga maandazi, chapati, samaki, vibanzi (chips) na vyakula vingine. 

Pia, unapotaka kukaanga kwa kutumia mafuta, kupika mayai au hata kupika vyakula vingine ni vyema ukawa na kikaango zaidi ya kimoja huku ukihakisha matumizi ya kifaa hicho kuwa safi na salama.

Unaweza kuwa na zote au moja kulingana na aina ya chakula mtu anachopendelea kupika. Picha / de Buyer.

Vijiko vya kupikia

Hivi ni vijiko vikubwa maalumu kwa kupikia vyakula na kupakulia.  

Vijiko vya kupikia vipo vya aina tofauti kama vile vya plastiki ngumu na vya aluminiamu, na mara nyingi huwa vinakuwa vijiko sita.Vipo vya kupakulia supu, vijiko vya kupakulia tambi, vijiko vya kutolea vitu kama chipsi, ndizi na nyama kwenye mafuta, vijiko vya kupakulia wali, vijiko vya kukaangia chapati, na maandazi.

Vijiko hivi ni imara na hudumu kwa muda mrefu, vinaweza kutumika jikoni au wakati wa kupakua chakula mezani kwa wale wanaopenda kula kila mtu na sahani yake. Picha / Vyombo vya kupikia.

Blenda

Hii ni vyema ukawa nayo na itakusaidia katika mambo mengi. Unaweza ukawa na blenda pekee na kama uchumi unaruhusu unaweza kununua ‘food processor’ ( Kichakata matini)  kabisa.

Blenda itakusaidia kutengeneza vitu mbalimbali na ukinunua ambazo hufanya kazi zaid ya moja ni vyema zaidi.

Blenda hutumika kusaga nyanya, nyama, mchanganyiko wa vitu mbalimbali kama vile unga wa kupikia keki,  karanga au korosho kwa ajili ya juisi na sharubati mbalimbali.

Blenda sio tu ni muhimu jikoni lakini pia ina rahisisha kazi na kuokoa muda kwa mpishi. 

Blenda ya kusagia matunda na vyakula mbalimbali husaidia kuokoa muda wa maandalizi ya chakula jikoni. Picha / Amazon.

Mwiko/upawa

Ni dhahiri kuwa hakuna kitu mpishi anaweza fanya jikoni bila ya kuwa na mwiko au upawa. Iwe anapika ugali, mboga, wali au mchuzi wa aina yoyote ni lazima awe na mwiko.

Kuna aina tofauti tofauti za miiko: mwiko wa plastikia na mbao ingawa hutofautiana katika ubora na matumizi yake.

Na kazi kubwa ya mwiko au upawa ni kumrahisishia mpishi kazi ya kugeuza chakula, kuchanganya vitu kwenye sufuria vikiwa bado vipo jikoni pamoja na kukoroga chumvi kwenye chakula.

Kitu cha kuzingatia wakati wa kununua mwiko, ni vyema kuchagua unaoendana na  matumizi yako.

Miko hii hutumika kugeuzia mboga na vyakula mbalimbali. Picha / Indian Mart.

Vibao vya Silikoni

Vibao vya silikoni haviwezi kuonekana kuwa vya kipekee lakini ni lazima ziwepo jikoni. Vibao hivi vinasaidia kuepua chakula kutoka katika jiko lako na hivyo kukinga na madhara ya kuungua. 

Vifaa hivi vinafaa kwa kazi za kila siku za jikoni, kuchoma mahindi, kugeuza baga, samaki, kukata nyama choma, au kutumika kugeuza mishikaki. Picha / Amazon.

Hivi ni baadhi tu ya vifaa vya jikoni usikose sehemu ya pili ya vifaa vya jikoni na matumizi yake.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa