Dar es salaam. Maziwa ya mama ni chakula muhimu na cha msingi kabisa kwa watoto waliopo kwenye umri wa kunyonya. Wataalamu wa afya wanashauri mtoto apewe maziwa ya mama peke yake kwa muda wa miezi sita ndipo aanze kupewa vyakula vingine laini.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Chakula na Lishe Nchini Tanzania (TFNC) asilimia 98 ya wanawake huwanyonyesha watoto wao na asilimia 58 ya watoto wananyonyeshwa maziwa ya mama pekee ndani ya miezi sita ya mwanzo.
Pamoja na asilimia 98 ya wanawake kuchagua kuwanyonyesha watoto bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazowafanya kushindwa kutekeleza kwa usahihi zoezi la unyonyeshaji ikiwemo mama kukosa maziwa ya kutosha.
TFNC wanabainisha kuwa mama anayenyonyesha anatakiwa kuwa na lishe bora kutokana na kuwa na mahitaji makubwa ya virutubishi mwilini kwa ajili ya afya yake na kwa ajili ya kutengeneza maziwa ya mtoto.
Njia mojawapo ya mama kuzalisha maziwa ya kutosha ni kupitia kula vyakula vyenye lishe katika milo mitatu kamili ya kila siku pamoja na asusa. Makala haya yanaangazia vyakula vitakavyomsaidia mama anayenyonyesha kuzalisha maziwa mengi.
Matunda na mboga mboga
Mboga zina vitamin A, C, E na K pamoja na viwango vya chini vya kalori pia huwa na nyuzi nyuzi au ‘fiber’ pamoja na kemikali zinazozuia chakula kuoza kinaposagwa. Inashauriwa mama kula angalau mboga na matunda tofauti katika kila mlo.
Nyama
Mama anayenyonyesha anahitaji madini ya zinki pamoja na madini chuma kwa wingi. Nyama nyekundu huwa na madini hayo. pIA nyama ya samaki pamoja na nguruwe huwa na vitamini B ambayo husaidia kuupa mwili nguvu pamoja na kuongeza damu.
Maji
Maji ni muhimu katika kuongeza kiwango cha maziwa ya mama anayenyonyesha kwani yanahusika pakubwa katika utengenezaji wa maziwa. TFNC wanashauri mama anayenyonyesha atumie angalau bilauri nane za maji kwa siku au lita moja na nusu.
Kwa mujibu wa mtandao wa elimu ya malezi wa Africaparent mama anayenyonyesha anapaswa kuepuka vinywaji vilivyoongezwa sukari au kafeini na kutumia kwa wingi vimiminika kama supu au maji ya matunda.
Nafaka
Vyakula vinavyotokana na nafaka isiyokobolewa kama vile ulezi, mtama, mchele wa ‘brown’ vinashauriwa zaidi kwa mama anayenyonyesha kwani vinaathari kidogo katika kiwango cha sukari mwilini na utengenezaji wa insulini kuliko vyakula vinavyotokana na nafaka iliyokobolewa.
Protini
Vyakula kama samaki, kuku, maharagwe, njugu, mayai ni vyakula vinavyoleta afya kwa mama anayenyonyesha kutokana na protini ambayo husaidia kuupa mwili virutubisho pamoja na vitamini muhimu.
Pamoja na kula zaidi ya milo mitatu kamili ya chakula mama anayenyonyesha anashauriwa na TFNC kula asusa kati ya mlo na mlo.
Asusa ni nini?
Hiki ni kiasi kidogo cha chakula ambacho si mlo kamili, kinachoweza kuliwa bila matayarisho makubwa na huliwa kati ya mlo mmoja hadi mwingine.
Kwa mujibu wa TFNC, mama anayenyonyesha anashauriwa kuchagua asusa zenye virutubisho muhimu kama matunda, vyakula vilivyochemshwa au kuchomwa na kuepuka asusa zilizokaangwa, zenye sukari au chumvi nyingi.