Vyakula vinavyoongeza maziwa kwa mama anayenyonyesha

Na Esau Ng'umbi
22 Sept 2022
Njia mojawapo ya mama kuzalisha maziwa ya kutosha ni kupitia kula vyakula vyenye lishe katika milo mitatu kamili ya kila siku pamoja na asusa.
article
  • Ni pamoja na nyama, matunda na mbogamboga. 
  • Kula zaidi ya milo mitatu pamoja na asusa kunashauriwa.

Dar es salaam. Maziwa ya mama ni chakula muhimu na cha msingi kabisa kwa watoto waliopo kwenye umri wa kunyonya. Wataalamu wa afya wanashauri mtoto apewe maziwa ya mama peke yake kwa muda wa miezi sita ndipo aanze kupewa vyakula vingine laini.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Chakula na Lishe Nchini Tanzania (TFNC) asilimia 98 ya wanawake huwanyonyesha watoto wao na asilimia 58 ya watoto wananyonyeshwa maziwa ya mama pekee ndani ya miezi sita ya mwanzo. 

Pamoja na asilimia 98 ya wanawake kuchagua kuwanyonyesha watoto bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazowafanya kushindwa kutekeleza kwa usahihi zoezi la unyonyeshaji ikiwemo mama kukosa maziwa ya kutosha.

TFNC wanabainisha kuwa mama anayenyonyesha anatakiwa kuwa na lishe bora kutokana na kuwa na mahitaji makubwa ya virutubishi mwilini kwa ajili ya afya yake na kwa ajili ya kutengeneza maziwa ya mtoto.

Njia mojawapo ya mama kuzalisha maziwa ya kutosha ni kupitia kula vyakula vyenye lishe katika milo mitatu kamili ya kila siku pamoja na asusa. Makala haya yanaangazia vyakula vitakavyomsaidia mama anayenyonyesha kuzalisha maziwa mengi.

Matunda na mboga mboga

Mboga zina vitamin A, C, E na K  pamoja na viwango vya chini vya kalori pia huwa na nyuzi nyuzi  au ‘fiber’ pamoja na kemikali zinazozuia chakula kuoza kinaposagwa. Inashauriwa mama kula angalau mboga na matunda tofauti  katika kila mlo.

Nyama 

Mama anayenyonyesha anahitaji madini ya zinki pamoja na madini chuma kwa wingi. Nyama nyekundu huwa na madini hayo. pIA nyama ya samaki pamoja na nguruwe huwa na vitamini B ambayo husaidia kuupa mwili nguvu pamoja na kuongeza damu.

Maji

Maji ni muhimu katika kuongeza kiwango cha maziwa ya mama anayenyonyesha kwani yanahusika pakubwa katika utengenezaji wa maziwa. TFNC  wanashauri mama anayenyonyesha atumie angalau bilauri nane za maji kwa siku au lita moja na nusu.

Mama anayenyonyesha anashauriwa kunywa maji mara kwa mara. Picha | Esau Ng’umbi.

Kwa mujibu wa mtandao wa elimu ya malezi wa Africaparent mama anayenyonyesha anapaswa kuepuka vinywaji vilivyoongezwa sukari au kafeini na kutumia kwa wingi vimiminika kama supu au maji ya matunda.

Nafaka 

Vyakula vinavyotokana na nafaka isiyokobolewa kama vile ulezi, mtama, mchele wa ‘brown’  vinashauriwa zaidi kwa mama anayenyonyesha kwani vinaathari kidogo katika kiwango cha sukari mwilini na utengenezaji wa insulini kuliko vyakula vinavyotokana na nafaka iliyokobolewa.

Protini 

Vyakula kama samaki, kuku, maharagwe, njugu, mayai ni vyakula vinavyoleta afya kwa mama anayenyonyesha kutokana na protini ambayo husaidia kuupa mwili virutubisho pamoja na vitamini muhimu.

Pamoja na kula zaidi ya milo mitatu kamili ya chakula mama anayenyonyesha anashauriwa na TFNC kula asusa kati ya mlo na mlo.

Asusa ni nini?

Hiki ni kiasi kidogo cha chakula ambacho si mlo kamili, kinachoweza kuliwa bila matayarisho makubwa na huliwa kati ya mlo mmoja hadi mwingine.

Kwa mujibu wa TFNC, mama anayenyonyesha anashauriwa kuchagua asusa  zenye virutubisho muhimu kama  matunda, vyakula vilivyochemshwa au kuchomwa na kuepuka asusa zilizokaangwa, zenye sukari au chumvi nyingi.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa