Zifahamu sababu za tumbo kujaa gesi

Na Lucy Samson
20 Feb 2023
Mara kadhaa utasikia watu wakilalamika kuwa matumbo yao yamejaa gesi kiasi kinachowazuia kula vizuri au kufanya baadhi ya shughuli. Tatizo hili la kiafya linaloweza kuwapata watu wa rika zote, huambatana na dalili mbalimbali ikiwemo maumivu ya tumbo yasiyo ya kawaida, tumbo kujaa, maumivu ya kifua  pamoja na kukosa hamu ya kula. Kwa mujibu wa tovuti healthline gesi […]
article

Mara kadhaa utasikia watu wakilalamika kuwa matumbo yao yamejaa gesi kiasi kinachowazuia kula vizuri au kufanya baadhi ya shughuli.

Tatizo hili la kiafya linaloweza kuwapata watu wa rika zote, huambatana na dalili mbalimbali ikiwemo maumivu ya tumbo yasiyo ya kawaida, tumbo kujaa, maumivu ya kifua  pamoja na kukosa hamu ya kula.

Kwa mujibu wa tovuti healthline gesi hiyo inayozidi tumboni inaweza kutolewa kwa njia ya mdomo au kwa njia ya haja kubwa zaidi ya mara 20 kwa siku.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya,  zipo sababu mbalimbali zinazochangia tatizo la  gesi tumboni ikiwemo kuwepo kwa matatizo kwenye mmeng’enyo wa chakula.

“Mmeng’enyo wa chakula huweza kushambuliwa na magonjwa mbalimbali ikiwemo  Ulcerative colitis na celiac disease (magonjwa yanayoshambulia mfumo wa chakula) kusababisha kujaa gesi kwa tumbo,” anasema Meshack Mhalila, mtaalam wa afya wa kujitegemea kutoka Mkoani Mbeya.

Watu wa rika zote wapo kwenye hatari ya kupata tatizo la gesi tumboni ikiwa hawatazingatia ulaji mzuri kulingana na kanumi za afya. Picha |Lucy Samson

Kukosa choo au kupata choo kigumu (Constipation)

Kukosa choo kwa muda mrefu husababisha mlundikano wa uchafu tumboni ambao huzalisha backeria.

Mtaalamu huyo wa afya anaeleza kuwa bakteria hao wanaozalishwa huchochea mchakato wa uchachushwaji (fermentation) wa uchafu huo hali inayozalisha gesi zaidi.

Kukosa choo na choo kigumu husababishwa na ulaji wa vyakula vilivyokobolewa sana visivyo na kambakamba, matumizi kidogo ya maji, msongo wa mawazo na kuishi bila kufanya mazoezi.

Mwili kukosa maji (Dehydration)

Mwili unapokosa maji ya kutosha, chakula  kinachoingia tumboni hukosa uwezo wa kuvunjwa vunjwa vizuri na kutolewa nje kwa njia ya haja kubwa, hali inayochangia gesi kubaki tumboni kwa wingi

Mbali na hayo maji maji yalipo tumboni (Gastric juices) yanayorahisisha  mchakato wa mmeng’enyo wa chakula huzalisha gesi pale unapojikunja kusukuma chakula kwenye utumbo, hivyo upungufu wa maji mwilini huchochea uzalishaji wa gesi hizo.

“Hakikisha unakunywa maji mara nyingi zaidi kila siku ili kuepuka tumbo kujaa gesi,” ameongeza Mhalila.

Uchovu wa mara kwa mara ni moja ya dalili ya mwili kukosa maji.Picha|Lucy Samson

Mzio (alerg) ya baadhi ya vyakula

Mzio wa vyakula mbalimbali kama maziwa, mayai na ngano inaweza kuwa ni sababu ya kujaa gesi kwa tumbo lako. 

“Hapa tunatofautiana unaweza kukuta kwangu chakula fulani nikila sipati gesi na mwingine akila anapata gesi, cha kufanya ni kufuatisha mwili wako.

Kama mwili unakataa aina fulani ya vyakula na unapata mchafuko kama kupata gesi, kuvimba mwili, kuharisha au kutapika basi usitumie chakula hicho,” amesema Mhalila.

Maambukizi ya bakteria, virusi kwenye utumbo

Maambukizi ya hayo ya bakteria huweza kushambulia utumbo mwembamba na kuzuia mchakato wa mwili kufyonza virutubisho na hatimaye kuzalisha gesi ya ziada.

Kwa mujibu wa tovuti ya healthline,  bakteria hao  wanaweza pia kuharibu utando wa utumbo mwembamba na kusababisha dalili nyingine kama kutapika, kuharisha na maumivu ya tumbo.

Chukua tahadhari

Wataalam wa afya wanashauri mgonjwa kuchukua tahadhari endapo hali ya tumbo kujaa gesi itaendelea kwa muda mrefu.

“Tumbo kujaa gesi pia ni dalili ya magonjwa mengine kama saratni ya haja kubwa hivyo ni vyema kutembelea vituo vya afya,” amesema Mhalila.

Awali habari hii ilichapishwa kwenye tovuti ya Nukta Habari(www.nukta.co.tz).

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa