Ni kweli jokofu limetengenezwa kwa ajili ya kuhifadhi vyakula ili visiharibike na ni kweli kifaa cha kupashia vyakula (Microwave) kimenunuliwa kikiwa na nafasi ya kupasha mlo mmoja kwa wakati mmoja.
Lakini, mambo haya yanahitaji ubunifu ili kuhakikisha umeme wako haupotei na kukuongezea gharama zisizo za lazima. Haya ni mambo machache unayoweza kuyafanya ili kurahisisha maisha yako wakati ukitumia friji na “microwave”:
Huenda wewe ni kati ya wadau ambao wakienda sokoni kununua mahitaji ya nyumbani, wakirudi huhifadhi vitu hivyo kwenye friji bila hata kuviosha.
Ni kwanini upate tabu ya kuloweka mboga zako baada ya kuzitoa kwenye jokofu la kugandisha? Ni busara kuziandaa mboga zako kabla ya kuzihifadhi kwenye jokofu ili ukizitoa kwenye safari inakuwa ni moja tu ya kuweka kwenye sufuria na kupika.
Kwa kufanya hivi, utarahisisha kazi yako jikoni hasa kwa mikono kupata ganzi wakati wa kushika barafu na mboga zilizoganda.
Watumiaji wengi wa majokofu hawafuatilii kiasi cha ubaridi kinachofaa kwenye chakula fulani. Wengi hujikuta wakigandisha hadi matikiti maji wakidhani yatakua sawa baada ya kuyatoa kwenye jokofu.
Kwanini uhangaike, baadhi ya vyakula hupoteza ladha vikigandishwa na endapo utavitumia baadaye, hautafurahia ladha yake.
Vyakula kama matikiti na matunda mengine yenye maji mengi havifai kugandishwa badala yake vinahitaji ubaridi wa wastani tu. Kama huna utaalamu wa kiasi cha ubaridi na chakula, unaweza kumuomba kijana wako au mtaalamu mwingine akusaidie kuweka ubaridi utakaofaa kwa vyakula vyako kwenye jokofu.
3. Pasha milo miwili kwa wakati mmoja kwenye “Microwave” yako
Ndiyo! inawezekana. Wakati wengi wakishindwa kupasha milo miwili kwa wakati mmoja kwenye kifaa hiki, jambo ambalo linasababisha chakula ambacho kimepashwa mara ya kwanza kupoa wakati kingine kinaendelea kupashwa, fahamu kuwa unaweza kupasha milo miwili kwa mkupuo.
Unachohitaji ni bakuli moja, sahani moja na kikombe. Tanguliza bakuli yenye chakula na kisha weka kikombe ambacho juu yake utaweka sahani yenye chakula kingine. Ni rahisi namna hiyo.
Sasa unaweza kupasha chakula chako na cha mgeni wako kwa wakati mmoja.
Umewahi kununua viungo “fresh” kama gilihiliani, vitunguu maji na vinginevyo ambavyo huharibika haraka hata kabla hujavifaidi? Kama ndiyo, basi sahau kupoteza fedha yako kwani unaweza ukatumia vigandishio vya barafu kugandisha viungo vyako.
Chukua viungo vyako na vikate kufikia kiasi utakacho, weka viungo vyako kwenye vigandishio vya barafu (Ice trays) na kisha weka mafuta ya kupikia kiasi ili vigande.
Kwa kufanya hivyo, hautahitaji kutumia mafuta endapo utavitumia kwani mafuta uliyoyagandisha na viungo yatakutosheleza. Sasa unaweza kuepuka kutupa viungo vyako kwa kisingizio ya kuharibika. Hata hivyo, mbinu hii siyo rafiki kwa vitunguu saumu.
Baki nasi katika tovuti yetu ya jikopoint.co.tz uzidi kuzifaidi dondoo muhimu za jikoni.