Chalamila awahimiza wanawake kutumia nishati safi ya kupikia

Na Fatuma Hussein
22 Aug 2025
Luoga amesisitiza kuwa Serikali tayari imeanza kuunganisha kaya na taasisi katika mifumo ya gesi asilia, huku mitungi 452,000 ikiwa tayari imetolewa kwa wananchi. 
article
  • Matumizi ya nishati safi ya kupikia yaongezeka kufikia asilimia 20.3.
  • Takribani taasisi 400  tayari zimeunganishwa na huduma ya gesi asilia.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amewataka wanawake nchini kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na badala yake kutumia nishati safi ya kupikia kwa ajili ya kulinda afya, mazingira na ustawi wa familia zao.

Chalamila aliyekuwa mgeni rasmi katika kongamano la nishati safi kwa maendeleo endelevu lililofanyika jijini Dar es Salaam leo Agosti 22, 2025 amesema matumizi ya nishati chafu yamekuwa chanzo cha magonjwa ya mfumo wa hewa na pia yamechangia uharibifu mkubwa wa mazingira kupitia ukataji miti ovyo.

“Rais Samia Suluhu Hassan anapokutaka wewe utumie nishati safi anakuongezea thamani ya kubaki kama unavyostahili kuwa kwa hiyo ndio maana nimesema kila mmoja amwangalie mwenzie alafu amwambie inawezekana hii sio sura yako…

… Kwa hiyo kama mwanaume aliweza kukuona wewe ni mzuri ukiwa hivyo hivyo basi inawezekana ungekuwa unatumia nishati safi pengine ungeolewa hata na mtu mwingine Billgate,” amesema Chalamila. 

Mgeni rasmi wa Kongamano la Pika Kijanja msimu wa nne Albert Chalamila akisalimiana na wenyeji wake baada ya kuwasili eneo la tukio. Picha/ Bongo fm.

Kwa mujibu wa ripoti ya Utafii wa Athari za Upatikanaji wa Nishati Endelevu kwa mwaka 2021/2022 inayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inabainisha uwepo wa matumizi makubwa ya kuni na mkaa vijijini kuliko mijini.

Ripoti hiyo ya NBS  inaweka wazi kuwa asilimia 88 ya kaya zilizopo vijijini zinatumia kuni kama chanzo kikuu cha mapishi, kulinganisha na asilimia 6 ya kaya zinazotumia nishati hiyo mjini.

Aidha, Chalamila ameongeza kuwa ingawa mkaa mara nyingi huonekana kuwa nafuu, gharama zake za muda mrefu ni kubwa kutokana na madhara ya kiafya yanayojitokeza. 

Ametolea mfano familia inayotumia mkaa kwa mwaka huweza kuokoa fedha kidogo, lakini baada ya muda hujikuta ikitumia gharama kubwa kwa matibabu ya magonjwa ya mapafu na matatizo mengine ya kiafya.

Kwa upande wake Mhandisi Innocent Luoga, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, amebainisha kuwa juhudi za Serikali katika kusukuma matumizi ya nishati safi zimeanza kuleta mafanikio makubwa.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Albert Chalamila akifuatilia mjadala wa Nishati Safi ya Kupikia. Picha/ Bongo fm.

“Matumizi ya nishati safi yameongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021/22 hadi asilimia 20.3 mwaka huu. Hii ni hatua kubwa na tunalenga kufikia asilimia 80 ifikapo mwaka 2034, au hata mapema zaidi, kwa sababu mikakati ya Serikali na wadau inaendelea kutekelezwa kwa kasi,” amesema Luoga.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Albert Chalamila akishuhudia matumizi ya vifaa vinavyotumia nishati safi ya kupikia. Picha/ Bongo fm.

Luoga amesisitiza kuwa Serikali tayari imeanza kuunganisha kaya na taasisi katika mifumo ya gesi asilia, huku mitungi 452,000 ikiwa tayari imetolewa kwa wananchi. 

Kwa mujibu wa Luoga takribani taasisi 400 zikiwemo shule, magereza na makambi ya majeshi tayari zimeunganishwa na huduma hiyo.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa