Epuka makosa haya unapotumia Pressure cooker

Na Fatuma Hussein
22 Apr 2025
Ni pamoja na kutosafisha pressure cooker baada ya matumizi na kufuata muongozo sahihi.
article
  • Ni pamoja na kutosafisha pressure cooker baada ya matumizi na kufuata muongozo sahihi.

Ukuaji wa teknolojia hasa ya vifaa vya kielektroniki umerahisisha na kuyafanya maisha kuwa bora zaidi. Nyakati za sasa, siyo lazima utumie kuni au mkaa kupika chakula. Nishati safi na salama ndio suluhisho. 

Miongoni mwa teknolojia za kisasa za kupikia ni matumizi ya jiko la umeme lenye presha (Pressure Cooker). Kwa jiko hili linalotumia umeme kidogo unaweza kupika chakula kwa haraka na kuokoa muda. 

Kutokana na matumizi ya pressure cooker kuongezeka, baadhi ya watu wamekuwa wakifanya makosa ambayo yamekuwa yakipunguza uhai wa vifaa hivyo. 

Makosa hayo yamekuwa yakichangia vifaa hivyo kuharibika mapema na kumuongezea mmiliki gharama za kununua lingine.

Makala haya yanaangazia kwa undani makosa ya kuepuka wakati unatumia pressure cooker ili usiwe miongoni mwa watu watakaojutia uamuzi wa mzuri wa kupikia kwa kifaa hicho cha umeme. 

Kutokutumia mwongozo sahihi wa pressure cooker

Unaponunua pressure cooker hakikisha unazingatia kusoma muongozo kabla ya kutumia hii itakusaidia kukielewa vizuri kifaa unachohitaji kutumia. Picha/ Goodluck Gustaph/ Jiko Point.

Kosa moja kubwa linalofanywa na baadhi ya watu ni kupuuza kusoma mwongozo wa matumizi unaotolewa wakati unanunua kifaa chao. 

Kila pressure cooker lina maelekezo tofauti kuhusu matumizi yake. Hii ni pamoja na muda wa kupika, kiwango cha mvuke kinachohitajika, na hata namna ya kuifunga au kuisafisha.

Kutumia kifaa bila kuelewa mwongozo wake kunaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo ajali ndogo ndogo jikoni au chakula kutokupikwa vizuri.

Ni muhimu kufahamu kuwa ukubwa na uwezo wa pressure cooker hutofautiana kati ya chapa moja hadi nyingine. Hii ina maana kuwa kiwango cha chakula au maji kinachohitajika kinaweza kutofautiana kulingana na kifaa unachotumia. 

Kabla ya kuanza kupika hakikisha umesoma na kuelewa mwongozo wa matumizi ya kifaa chako ili kupata matokeo bora na kuepuka hatari zisizotarajiwa.

Kutosafisha pressure cooker baada ya matumizi

Ili kuongeza ufanishi kwenye kifaa chako ni muhimu kuisafisha vizuri hasa pale unapomaliza kupika. Picha/ Goodluck Gustaph/ Jiko Point.

Baada ya kutumia pressure cooker, baadhi ya watu husahau au hupuuzia hatua muhimu ya kuisafisha. Usafi ni miongoni mwa mambo yatakayoimarisha utendaji wake na kuifanya idumu kwa muda mrefu. 

Pressure cooker isiposafishwa vizuri hasa sehemu kama valvu za mvuke inaweza kuanza kunuka vibaya au kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi.

Sufuria ya ndani, mfuniko na valvu zinahitaji usafi wa kina baada ya kila matumizi. 

Ikiwa sehemu hizi zitaachwa bila kusafishwa zinaweza kukusanya mabaki ya chakula au mafuta na kuziba mfumo wa mvuke, jambo linaloweza kupunguza ufanisi wa kifaa hicho.

Kutotumia kipimo sahihi cha maji

Unapotumia kipimo ambacho sio sahihi kuna uwezekano mkubwa wa kuzidisha maji au kupunguza maji jambo ambalo linaweza kuchochea kupata chakula kibaya. Picha/ Goodluck Gustaph/ Jiko Point.

Kiwango cha maji ni mojawapo ya mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kutumia pressure cooker. Tofauti na njia za kawaida za kupika, pressure cooker haina njia nyingi za kutoa mvuke na hivyo maji hayapotei kwa urahisi.

Ikiwa utaweka maji mengi kupita kiasi, unaweza kusababisha chakula kuwa na ladha isiyo nzuri au hata kukifanya kifaa hicho kishindwe kufanya kazi ipasavyo.

Wakati wa kupika vyakula kama nyama, samaki au supu ya karoti usitumie maji mengi kwani vyakula hivi hutoa maji yao ya asili wakati wa kupikwa. Fuata kipimo kinachopendekezwa kwenye mwongozo au mapishi husika ili kupata matokeo bora.

Kupika vyakula visivyofaa 

Si kila chakula kinafaa kupikwa kwa kutumia pressure cooker. Kila pressure cooker utakalonunua limeainisha aina ya chakula unachotakiwa kupika. Ukipika chakula tofauti na maelekezo, unaweza kupata matokeo yasiyo mazuri ikiwemo chakula kutokuiva vizuri. 

Kutumia pressure cooker kwa chakula ambacho hakiendani nayo ni kupoteza muda na malighafi. Zingatia malekezo ili kifaa chako kifanye kazi kwa ufanisi mzuri na kudumu muda mrefu.

Kupika chakula kingi kwa wakati mmoja

Kupika chakula kupita kiasi kunaweza kusababisha kutokuiva na badala yake ukawa unapoteza muda. Picha/ Adobe stock.

Kila pressure cooker lina sufuria yake maalum ambayo imetengenezwa kubeba ujazo fulani wa chakula. Ukizidisha, chakula hakitaiva wala kifaa hicho hakitafanya kazi na ukilazimisha kinaweza kuharibika mara moja. 

Pia, mvuke hauwezi kusambaa sawasawa kama sufuria imejaa kupita kiasi ni muhimu kuheshimu viwango vilivyowekwa. 

Kabla ya kupika chakula, angalia vipimo unavyotakiwa kuweka. Siyo vibaya kupika mara mbili kwa sababu kifaa hicho kinatumia umeme mdogo na kinapika kwa haraka.

Kutotumia mfuniko kwa usahihi

Soma mwongozo vizuri ili kujua njia sahihi ya namna ya kufunga mfuniko wa jiko hasa wakati wa upishi. Picha/ Goodluck Gustaph/ Jiko Point.

Mfuniko wa pressure cooker ni sehemu muhimu ya ufanisi wa kifaa hiki. Ikiwa hautafungwa kwa usahihi, presha haitajikusanya ndani na hivyo chakula kinaweza kisiive vizuri. Pia mfuniko usipofunikwa vizuri, unaweza kusababisha madhara kwa mtumiaji kwa sababu presha inaweza kutoka kwa ghafla.

Soma mwongozo namna ya kufunga mfuniko wa jiko. Ujuzi huu ni muhimu kwa usalama na mafanikio ya kila mlo unaopikwa kwa kutumia pressure cooker.

Kwa kuepuka makosa haya ya kawaida utajihakikishia upishi wa haraka, salama na wenye ladha ya kipekee huku ukizingatia kila hatua kusoma mwongozo.

Kama bado hujaanza kutumia pressure cooker, bado hujachelewa, JikoSokoni, duka la mtandaoni la JikoPoint linauza kifaa hicho kwa bei nafuu. Tembelee hapa kufahamu zaidi. 

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa