Fahamu aina za majiko na faida zake

Na Fatuma Hussein
2 Jan 2025
Kila jiko lina sifa za kipekee ikiwemo ubunifu wa kisasa na ufanisi wa nishati.
article
  • Ni pamoja na jiko la umeme na jiko la gesi yaliozoeleka kwa kila mtu.
  • Kila jiko lina sifa za kipekee ikiwemo ubunifu wa kisasa na ufanisi wa nishati.

Kuchagua jiko bora kwa ajili ya mapishi ni miongoni mwa kibarua wanachokutana nacho wapishi wengi hususani wasiofahamu faida na matumizi ya kila aina ya jiko.

Tofauti na ilivyokuwa miaka ya zamani ambapo wazee wetu walitumia aina zinazofanana za majiko ambayo ni majiko ya kuni au mkaa, siku hizi kuna aina nyingi za majiko zenye teknolojia rahisi zinazofaa kwa kila aina ya matumizi.

Jiko Point imekuandalia orodha ya aina za majiko ya kisasa yanayotumia nishati safi ya kupikia, faida na matumizi yake ili kukuruhusu kufanya maamuzi sahihi wakati mwingine utakapohitaji kununua jiko.

Jiko la induction (Induction cooktop)

Jiko lenye ufanisi wa hali ya juu, linapika kwa haraka huku likihifadhi nishati. Picha / Real simple.

Jiko hili hutumia teknolojia ya sumaku umeme kuleta joto moja kwa moja kwenye sufuria. 

Kwenye jiko hili, hakuna moto unaoonekana wala joto kwa uso unaozunguka hivyo linafaa zaidi kwa wapishi wanaopenda teknolojia ya kisasa na watu wanaopenda kubana matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.

Faida unazotarajia kuzipata ukitumia jiko hili ni pamoja na kupunguza muda wa kupika, kurekebisha joto mara moja pale unapohitaji, kupunguza athari za kupata majeraha ya moto na uso wa jiko kuwa na uwezo wa kutunza baridi.

Jiko la ‘Coil’

Jiko la coil linalodumu muda mrefu, linatoa joto thabiti kwa vyombo vyote vya kupikia.Picha / The sprunce.

Jiko la Coil hutumia umeme kuzalisha joto linalotumika kupika aina mbalimbali za chakula

Jiko hili limeundwa kwa chuma kigumu kilichozungushwa kwa juu mfanano wa dawa ya mbu ya kuchoma, chuma hicho kimeunganishwa na umeme na kikipata moto hubadilika na kuwa na rangi ya machungwa au nyekundu.

Aina hizi za jiko kwa kawaida ni za bei nafuu na zinapatikana kwa urahisi hii ni kutokana na kuwa na gharama nafuu.

Jiko la kioo la kauri (Ceramic glass cooktop)

Uso wa kioo laini unaoonekana maridadi, unaongeza mvuto wa jikoni hili. Picha / Ceramic Glass 

Jiko la kioo la kauri ni chaguo bora kwa wale wanaotafuta kifaa cha kisasa pia linatumia umeme na lina uso wa kioo.

Faida za kutumia jiko hili ni rahisi kusafisha, usambazaji sawa wa joto, na mvuto wa kisasa. Licha ya faida hizo pia jiko hili huathirika kirahisi kwa mikwaruzo.

Jiko la gesi (Gas stove)

Jiko la gesi linaloweza kutumika hata wakati wa kukatika kwa umeme. Picha / AEG South Africa.

Jiko la gesi ni maarufu na linatumia gesi asilia au propane. Jiko hili lina  vitufe vinavyoweza kudhibiti moto. 

Kulingana na uwezo wake wa kiufundi jiko hili linaweza kutumika nyumbani na katika migahawa mikubwa.

Miongoni mwa faida za kutumia jiko hili ni pamoja na kupunguza muda wa kupika, kutumika hata wakati umeme unapokuwa umekatika na uwezo wa kupasha vyombo vya joto kwa haraka 

 Jiko la umeme (Electric stove)

Jiko la umeme linalotumia nishati kwa ufanisi, bora kwa mazingira na familia yako.Picha /Alibaba.

Jiko la umeme hutumia umeme kubadili nishati kuwa joto. Lina sehemu ya kupasha joto juu ya uso wa kupikia, inayodhibitiwa kwa vitufe maalum.

Licha ya kufaa kwa wapishi wa aina zote jiko hili ni salama kwa familia zenye watoto, rahisi kusafisha pia husambaza moto sawia kwa vyombo vyote..

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa