Jinsi ya kujikinga na madhara ya matumizi yasio sahihi ya gesi ya kupikia nyumbani

Na Nyendo Mwaja
2 Jan 2026
Ni pamoja na kuwa karibu na gesi wakati wa kupika na kuitumia sehemu yenye hewa kubwa.
article
  • Ni pamoja na kuwa karibu na gesi wakati wa kupika na kuitumia sehemu yenye hewa kubwa.

Wakati Serikali na wadau wa nishati wakiendelea kuhamasisha matumizi ya gesi ya kupikia nyumbani (LPG), watumiaji wanashauriwa kuchukua tahadhari ili kujikinga na madhara ya kiafya ya matumizi yasiyo sahihi ya nishati hiyo ikiwemo kutumia vifaa vyenye ubora. 

Tafiti zinaonyesha kuwa nishati hiyo safi na salama mbadala wa kuni na mkaa imekuwa ikisababisha matatizo ya kiafya kwa watumiaji wake kutokana na kutozingatia maelekezo ya utumiaji wake.  

Matumizi mabaya ya nishati safi ya gesi husababisha mlipuko kutokea, Picha/Nukta Habari

Ripoti ya utafiti kuhusu majeraha ya moto yanayotokana na shughuli za kupikia kwa wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ya mwaka 2024 inatoa picha halisi ya chanzo cha ajali za moto zinazotokana na shughuli za kupikia. 

Utafiti huo ulifanywa na watafiti madaktari wa MNH na kuchapishwa katika jarida la Science Direct ulichambua wagonjwa wa majeraha ya moto waliolazwa hospitalini hapo kati ya Februari 2022 na Januari 2023, 

Katika kipindi hicho, jumla ya wagonjwa 377 wa majeraha ya moto walilazwa MNH. Kati yao, wagonjwa 100 walipata majeraha yanayohusiana moja kwa moja na upishi. 

Kukosa umakini wa kukagua vifaa vya vyenye gesi huweza kusababisha mlipuko, Picha/ Ujue moto

Utafiti unaonesha kuwa mkaa ulihusika kwa kiwango kikubwa zaidi, ukichangia zaidi ya nusu ya majeraha hayo. Hata hivyo, gesi ya kupikia ilihusishwa na zaidi ya theluthi moja (35%) ya ajali hizo, ikifuatiwa na kuni, huku umeme ukiwa na asilimia moja. 

Licha ya mkaa kuongoza, watafiti walielekeza umakini wao kwenye gesi ya kupikia kutokana na kuongezeka kwa matumizi yake kama mbadala wa nishati chafu. 

Kwa wagonjwa 35 waliopata majeraha yanayohusiana na LPG, sababu kuu zilikuwa uvujaji wa gesi, hali iliyochangia idadi kubwa ya ajali hizo, pamoja na uzembe katika matumizi ya majiko. 

Kwa mujibu wa utafiti huo, sehemu kubwa ya ajali hizi zingeweza kuzuilika endapo tahadhari za msingi zingezingatiwa.

Kipengele kilichozua wasiwasi zaidi ni ukosefu wa elimu ya usalama kwa watumiaji. 

Ukosefu wa elimu ya usalama kwa watumiaji husababisha athari kwa watumiaji kutokana na mlipuko kama huu, Picha/Swahili Times

Asilimia 85.7 ya waathirika wa ajali za gesi ya kupikia walieleza kuwa hawakupata maelekezo yoyote ya usalama kutoka kwa wauzaji wa mitungi ya gesi wakati wa kununua au kujaza gesi. Hali hii inaweka hatarini zaidi watumiaji wapya au wale wasio na uzoefu wa matumizi ya LPG.

Wakati Taifa likihimiza matumizi ya LPG ili kupunguza ukataji miti, uchafuzi wa hewa majumbani na madhara ya kiafya yatokanayo na kuni na mkaa, watafiti katika ripoti hiyo wanaonya kuwa ukosefu wa usimamizi thabiti na elimu kwa umma unaweza kugeuza suluhisho kuwa chanzo kipya cha matatizo.

Wanapendekeza kuimarishwa kwa udhibiti wa wauzaji wa gesi, utoaji wa elimu ya lazima ya usalama kwa wateja kabla ya kuuza au kujaza mitungi, pamoja na kampeni za kitaifa za uhamasishaji kuhusu matumizi salama ya gesi. 

Pia wanasisitiza umuhimu wa kuwepo kwa miongozo ya wazi ya kitaifa kuhusu matumizi na matengenezo ya mitungi ya gesi.

Chukua hatua hizi kujilinda na madhara ya kulipukiwa na gesi nyumbani

Ukifuata mambo haya unaweza kujilinda na madhara ya kiafya ikiwemo majeraha na kifo wakati ukitumia gesi ya kupikia nyumbani: 

Washa gesi yako kwa umakini

Mtaalamu wa nishati safi Saad Salim Mgeni kutoka kampuni ya Saady Gas point iliyopo mkoani Tanga anasema unapotaka kutumia gesi hakikisha unawasha kwa kiberiti au kitufe cha jiko lako na usiache itoke kwa muda mrefu kwani unapochelewa inaweza ikalipuka kutokana na hewa ya kuenea kwa sehemu kubwa.

“Kwanza washa kiberiti kisha ufungulie gesi na unaweza kubalansi moto wako kuwa mwingi au kidogo kutokana na uhitaji wako na aina ya chakula unachopika na pia jiko lako linataikwa liwe sehemu yenye hewa ya kutosha,” anasema Mgeni.

Hakikisha ‘banner’ yako haina kutu na imekaza vizuri

Banner: Hiki ni kifaa kinachosaidia moto kuwaka na kwa nguvu inayohitajika kwa kutoa na kusambaza gesi ikichanganya na hewa. Banner ikiwa imeharibika au kutokukazwa vizuri huongeza hatari ya moto au kulipuka kwa gesi.

Hakikisha banner yako imekaza vizuri ili kuzuia gesi isivuje, Picha/ Ubuy Tanzania.

“Hakikisha banner yako haina kutu na imekaza ili moto wako uweze kuwaka vizuri na ni vyema kuibadilisha kila baada ya miezi mitatu,” anasema Mgeni.

Weka mtungi wa gesi penye hewa ya kutosha

Hii inasaidia kupunguza mkusanyiko wa gesi endapo itavuja hivyo haitasongamana kufikia kiwango cha kulipuka. Husaidia itawanyike haraka hewani, jambo litakalokukinga na madhara ya kiafya ikiwemo kuvuta hewa chafu. 

Pia mtungi wa gesi usimame wima usiweke karibu na moto au jua kali. Kabla ya kuwasha jiko, hakikisha hakuna harufu ya gesi. Ukihisi harufu, zima gesi mara moja na fungua madirisha.

Hakikisha unakagua mtungi wako wa gesi mara kwa mara

Ni muhimu kukagua mtungi wako ili kuhakikisha usalama wa nyumba na familia. Hakikisha mtungi, mpira na viungio vyote vipo katika hali nzuri.

Unashauriwa kubadilisha vifaa vilivyochakaa au kupasuka ili kuzuia uvujaji wa gesi utakaosababisha mlipuko. Hii inaongeza umakini wa kufuatilia jiko lako kwa usalama wako binafsi.

Tumia vifaa vya gesi vyenye ubora

Tumia mtungi, jiko na viungio vyenye alama zilizothibitishwa na mamlaka za viwango ikiwemo Shirika la Viwango Tanzania (TBS). Epuka vifaa bandia au vya bei rahisi visivyo na viwango. 

Hakikisha vifaa vya gesi yako sio vya mda mrefu na viwe na ubora, Picha/Oili na Gesi.

Kuwa karibu na jiko wakati wa kupika
Kuacha jiko la gesi likiwa linaendelea kuwaka bila mtu karibu huongeza hatari ya chakula kuchemka na kuzima moto, gesi kuvuja au moto kulipuka ghafla. Moto mkali unaweza pia kusababisha vyombo kushika moto au mafuta kulipuka, hivyo ni muhimu kuwa karibu na jiko muda wote unapopika.

Usitumie gesi wakati umelewa au umechoka
Ulevi au uchovu hupunguza umakini na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi. Katika hali hiyo, mtu anaweza kusahau kuzima gesi, kuchelewa kugundua uvujaji wa gesi au kushindwa kudhibiti moto, jambo linaloweza kusababisha ajali za kuungua au nyumba kuwaka moto.

Wafundishe watoto mapema kuwa gesi si kifaa cha kuchezea
Watoto ni wadadisi kwa asili na wanaweza kuwasha jiko bila kujua hatari zake. Kuwazuia kukaribia jiko kunapunguza hatari ya kuungua au kusababisha moto. 

Weka gesi yako mbali na watoto na uwaeleze jinsi hatari itakayotokea endapo wataichezea, Picha/ Mwangwi wa Blogu ya Taifa.

Wafundishe mapema kuhusu hatari za gesi ili kuwajengea tabia ya tahadhari hata wanapokua watu wazima. 

Wasiliana na fundi au muuzaji aliyeidhinishwa
Usijaribu kurekebisha jiko, kidhibiti au mtungi wa gesi bila utaalamu yanaweza kuongeza uvujaji wa gesi na hatari ya mlipuko. Muite fundi aliyeidhinishwa ana ujuzi na vifaa sahihi vya kubaini tatizo na kulitatua kwa usalama.

Mgeni anasema wanawasaida wateja wao kuchukua tahadhari ya athari hizo kwa kuwapa elimu ya kutumia gesi ya kupikia na vifaa vyake ili isiwaletee madhara.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa