Kwa nini jiko la gesi ni chaguo bora kwa mama lishe Tanzania?

Na Nyendo Mwaja
6 Jan 2026
Baadhi ya mama lishe wanadai kuwa vipato vyao ni vidogo kuwawezesha kununua majiko na gesi huku wengine wakikosa elimu sahihi ya faida za nishati hiyo. 
article
  • Matumizi ya gesi yanaokoa muda na yanatunza mazingira na afya pia.
  • Wengi hutamani kutumia lakini hukwama kutokana na kushindwa kumudu gharama.
Jiko hili lamfaa mama lishe kwaajili ya kuokoa muda na kupika chakula chake kwa haraka na kwa wakati, Picha/ Habari Leo.

Miezi mitatu iliyopita alisema ‘inatosha” kutumia mkaa katika mgahawa wake.  

Huyu ni Shija Nyanda, mama lishe ambaye anatumia jiko la gesi ya majumbani (LPG) kupikia chakula katika mgahawa wake uliopo Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam. 

Shija, mama wa watoto watatu anasema aliamua kugeukia matumizi ya gesi ya majumbani ili kuokoa muda wa kupika chakula na kuwahudumia wateja wake kwa wakati. 

“Nina miezi kama mitatu natumia jiko la gesi na kwa kweli nalifurahia maana linanipa urahisi katika shughuli zangu za mapishi, ninatumia ule mtungi mkubwa wa Sh54,000 na ninatumia muda mfupi kupika kuliko nilivyokua natumia jiko la mkaa,” anasema Shija.  

Kabla ya kuanza kutumia jiko la gesi alikuwa akisumbuliwa na magonjwa ya mara kwa mara ya upumuaji na maumivu ya kichwa yaliyotokana na moshi wa mkaa. 

Jiko hili husaidia kujikinga na magonjwa ya kupumua na maumivu ya kichwa. Picha/ Mwangwi wa Blogu ya Taifa.

“Nilikuwa nikipumua kwa shida sana ule moshi niikuwa nauvuta na unapoingia puani naanza kukohoa na kusikia maumivu makali ya kifua, lakini pia baada ya muda naanza kusikia maumivu makali ya kichwa,” anasema Shija.

Tangu aanze kutumia nishati hiyo safi na salama ya kupikia, Shija (40) anakiri faida imeongezeka ambapo kwa sasa anapata wastani wa Sh35,000  hadi Sh40,000 kwa siku.

Wakati Shija akifaidika na matumizi ya jiko la gesi, elimu inahitajika zaidi kwa mama lishe wengine ambao wanaendelea kutumia kuni na mkaa kupikia chakula, jambo linalohatarisha afya zao.

Wataalam wa afya wanaeleza kuwa moshi unaotokana na kuni na mkaa unaweza kuathiri mapafu, moyo, mishipa ya damu, macho, ngozi na mfumo wa uzazi, na kusababisha magonjwa sugu na kifo. 

Baadhi ya mama lishe wanadai kuwa vipato vyao ni vidogo kuwawezesha kununua majiko na gesi huku wengine wakikosa elimu sahihi ya faida za nishati hiyo. 

“Kutokana na kipato changu kuwa kidogo na biashara hii ninayoifanya sijaweza kufanikiwa kununua jiko la gesi na kulitumia,” anasema Maria Mollel, mama lishe wa jijini Dar es Salaam. 

Maria anasema akiwezeshwa kifedha yuko tayari kutumia gesi ya kupikia badala ya mkaa na kuni ambao umekuwa siyo rafiki kwa afya yake. 

Majiko haya hutumika zaidi mijini kuliko vijijini kutoka na urahisi wa gharama na upatikanaji wake. Picha/ Jiko Point.

Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira inakadiria kuwa watu 22,000 hufariki dunia kila mwaka nchini Tanzania kutokana  na matumizi ya kuni na mkaa. 

Kwa mujibu wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati safi ya Kupikia (2024-2034) iliyotolewa Mei 2024, inaeleza kuwa  LPG inatumika zaidi mijini kuliko vijijini kwa sababu ya urahisi wa upatikanaji wa nishati hiyo.

Pia uwezo wa kumudu gharama kutokana na vipato vya watumiaji na kuongezeka kwa uelewa kuhusu matumizi salama ya LPG majumbani.

Gharama za awali za kununua mtungi wa kilo 15 ni takribani Sh110,000, jiko la LPG la sahani mbili ni takribani Sh50,000 na mtungi wa kilo 6 pamoja na jiko lake ni takribani Shilingi 58,000.

Gharama hizi za awali zinaweza kubadilika kulingana na eneo analoishi mtu na gharama za usafiri.

Serikali, wadau wanavyohimiza majiko ya gesi kupikia

Mtaalamu wa nishati safi ya kupikia wa kampuni ya Saddy Gas Point ya mkoani Tanga, Saad Salim Mgeni anaeleza kuwa moja kati ya faida atakazozipata mama lishe pale atakapotumia jiko la gesi ni usalama wa afya yake. 

“Jiko la gesi litamuepusha mama lishe na kuvuta hewa ya kabonimonokside inayotoka kama moshi kwenye mkaa na kuni ambayo ikivutwa kwa muda mrefu husababisha changamoto ya upumuaji na macho,” anasema Mgeni.

Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya kupikia wa 2024-2034 ambao utasaidia kuongeza idadi ya Watanzania wanaotumia nishati safi ikiwemo majiko ya gesi ili kulinda mazingira na afya za watumiaji. 

“Lengo la mkakati huo ni kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034,” alisema aliyewahi kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2025/26 bungeni jijini Dodoma. 

Pia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika programu ya usambazaji wa mitungi 452,445 nchini ambapo kila wilaya itapata mitungi 3,255 na kuigawa kwa wananchi.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa