Mahundi: Matumizi ya nishati safi ya kupikia si anasa

Na Lucy Samson
1 Oct 2024
Kiongozi huyo amesema nishati hiyo ina faida nyingi zaidi kuliko wengi wanavyofikiri.
article
  • Matumizi ya nishati safi ya kupikia hulinda afya za watumiaji na mazingira.

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mary Prisca Mahundi amesema kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwemo gesi na umeme si anasa kama ilivyozoeleka kwa baadhi ya watu.

Mahundi aliyekuwa akihamasisha wananchi kuhusu matumizi ya nishati hiyo jijini Dodoma hivi karibuni amesema kuwa matumizi ya nishati zisizo safi husababisha uharibifu mkubwa wa mazingira ikiwemo ukataji miti.

“Tunaposema tutunze mazingira, tunaweza kuona takriban hekta 469,000 za misitu zinateketea kwa mwaka  sababu ya shughuli mbalimbali za binadamu ikiwemo matumizi ya nishati zisizo safi za kupikia (kuni na mkaa) hivyo tunapotumia nishati safi kupikia tunaenda kutunza mazingira yetu,” amesema Mahundi.

Kiongozi huyo ameeeleza kuwa mbali na uharibifu wa mazingira matumizi ya nishati zisizo safi huathiri afya za watumiaji na kusababisha vifo vya zaidi vya watanzania 33,000 kila mwaka.

Ili kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2033 Serikali ya Tanzania ilizindua Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia Mei 8 mwaka huu.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika uzinduzi wa mkakati huo alisema ili kupunguza matumizi ya nishati zisizo salama nchini juhudi za pamoja zinahitajika ikiwemo kuelimisha wananchi juu ya faida ya nishati safi.

“Tatizo la matumizi madogo ya nishati safi ya kupikia ni mtambuka na ni suala linalohitaji nguvu za pamoja, hivyo mkakati huu unatoa mwongozo wa kitaifa kwa watu wote kufikia lengo tulilojiwekea la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034,” amesema Rais Samia.

Miongoni mwa masuala yaliyoangaziwa katika mkakati huo ni kuhamasisha taasisi zinazolisha watu 100 na kuendelea ikiwemo shule, magereza na polisi kutumia nishati safi ya kupikia.

Mbali na hatua hiyo, Serikali pia imeanza mchakato wa kuangalia upya bei ya nishati hizo ikiwemo gesi ili kuwezesha wananchi wengi kumudu hususan waishio vijijini.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa