Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewahimiza wake wa marais barani Afrika kuongeza juhudi katika kupigia chapuo matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza athari zinazowakabili wanawake na mazingira kutokana na matumizi ya nishati chafu ikiwemo mkaa na kuni.
Kwa muda sasa Rais Samia amejipambanua katika majukwaa ya kitaifa na kimataifa kubeba ajenda ya matumizi ya nishati safi akihimiza uwekezaji nanuwezeshaji wa upatikanaji wa nishati safi ya kupikia ili kuhakikisha watu wanapika katika mazingira salama kiafya na kimazingira.
Itakumbukwa Juni 5, 2024 Rais Samia alipokuwa akihutubia katika mkutano wa wakuu na serikali kati ya Korea na Afrika katika mji wa Goyang, Seoul Korea, aliwataka wakuu wa nchi za Afrika kuunga mkono ajenda ya nishati safi ya kupikia itakayotatua changamoto za kiafya kwa wanawake na kupunguza uharibifu wa mazingira katika kufikia lengo 7(1) la Malengo ya Milenia.
Lengo namba saba la Milenia linazungumzia nishati ya bei nafuu na safi ifikapo 2030 huku Tanzania ikiweka mkakati wa kufikisha nishati safi ya kupikia kwa zaidi ya asilimia 80 ya wanawake ifikapo 2034.
Rais Samia aliyekuwa mgeni rasmi katika mkutano wa 11 wa taasisi ya hisani ya Merck Foundation leo Oktoba 29,2024 jijini Dar es Salaam amesema wake wa marais wana nafasi muhimu ya kushawishi na kuchochea mabadiliko ya matumizi ya nishati safi katika jamii zao.
“Natamani kuwakumbusha dada zangu wake za maraisi, ninyi kama wake za maraisi pia mna nafasi muhimu katika jamii zenu mbalimbali…
… kwa kusema hivyo nina waomba dada zangu kuchukua mjadala huu wa wa nishati safi ya kupikia kwa uzito na kujali ili maraisi wenzangu wachukulie kama agenda ya kuwasaidia wanawake,” amesema Rais Samia.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na wake wa wakuu wa nchi mbalimbali Barani Afrika mara baada ya ufunguzi wa mkutano wa 11 wa Merck Foundation Africa Asia Luminary. Picha Ikulu Mawasiliano.
Matumizi ya nishati safi ya kupikia ni agenda mahususi ambayo imechukua nafasi kubwa katika Sera, Mipango na Mikakati ya Serikali mbalimbali duniani.
Umuhimu wa agenda hii unasukumwa na ongezeko la uharibifu wa mazingira, athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na athari za kiafya zinazotokana na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia.
Serikali ya Tanzania imeandaa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambao unatoa una lengo la kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Hata hivyo, baadhi ya wadau wa maendeleo wameishauri Serikali ili kufikia malengo ya mkakati huo inapaswa kuzidisha kasi ya uelimishaji wa jamii pamoja na kupunguza gharama ya nishati safi ikiwemo gesi ili iwafikie watu wengi kwa urahisi.
Nini maana ya nishati safi ya kupikia?
Kwa mujibu wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, nishati safi ya kupikia ni dhana inayotumika kuelezea na kubainisha nishati na teknolojia sahihi ambapo kwa pamoja hutoa moshi wenye kiwango kidogo cha sumu pale zinapotumika kwa usahihi.