Serikali kutoa ruzuku kupunguza makali ya bei ya gesi mijini, vijijini

Na Lucy Samson
8 Jan 2025
Wakazi wa vijijini watanunua gesi kwa ruzuku ya asilimia 50 na mijini kwa asilimia 20.
article
  • Wakazi wa vijijini watanunua gesi kwa ruzuku ya asilimia 50 na mijini kwa asilimia 20.
  • Msigwa asema matumizi ya gesi hupunguza gharama za maisha.

Serikali ya Tanzania imesema imetenga ruzuku itakayowezesha wananchi wa mijini na vijijini kununua gesi kwa bei rahisi hatua inayotajwa kuongeza matumizi ya nishati hiyo nchini

Gerson Msigwa, Msemaji Mkuu wa Serikali aliyekuwa akizungumza na wanahabari January 5, 2025 amesema katika mwaka wa fedha 2024/25 Serikali imetenga ruzuku ya asilimia 50 vijijini na asilimia 20 itakayowezesha wananchi kununua gesi ya kupikia kwa gharama nafuu.

“Katika bajeti yetu ya safari hii tumetenga fedha na tumeweka ruzuku katika bei ya gesi…Tunasambaza kila wilaya mitungi zaidi ya 3000 tutakwenda awamu kwa awamu,” amesema Msigwa.

Kauli hiyo ya Serikali kuhusu kutoa ruzuku katika bei ya gesi inakuja wakati ambao wadau na wananchi wamekuwa wakilalamikia bei ya nishati hiyo kuwa juu jambo linalowafanya baadhi yao kushindwa kumudu na kutumia nishati nyingine zisizo salama.

Mwaka 2024 Serikali ilizindua mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya kupikia wa miaka 10 kuanzia mwaka 2024 hadi mwaka 2024 ukilenga kuongeza matumizi ya nishati hiyo nchini.

Kabla ya mkakati huo, Ripoti ya Utafii wa Athari za Upatikanaji wa Nishati Endelevu kwa mwaka 2021/2022 inayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ilibainisha kuwa asilimia 67 ya kaya zote Tanzania Bara hutumia kuni kama chanzo kikuu cha nishati kwa ajili ya kupikia.

Gerson Msigwa, Msemaji Mkuu wa Serikali, akizungumza na wanahabari katika Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere, Dar es Salaam. Picha|Gerson Msigwa/X.

Hiyo ni sawa na kusema zaidi ya nusu au kaya sita kati ya10 zinatumia nishati hiyo kwa ajili ya mapishi huku asilimia 25 wakitumia majiko ya mkaa na asilimia 8.1 majiko mengine.

Ili kufikia malengo yaliyowekwa na mkakati huo ambayo pia ni miongoni mwa malengo endelevu (SDG) Serikali iliahidi kutoa ruzuku hiyo pamoja na  kuboresha miundombinu ya upokeaji wa gesi bandarini itakayosaidia kupunguza gharama za gesi kwa walaji.

“Kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania(TPDC) tunayo mikakati ya kuboresha miundombinu ya upokeaji wa gesi bandarini tunaamini tukipokea gesi kwa kiasi kikubwa zaidi tutakuwa na mahusiano ya moja kwa mlaji,” amesema Judith Kapinga, Naibu Waziri wa Nishati Mei 17, 2024.

Aidha, Msigwa amesema kuwa ruzuku hiyo itawasaidia Watanzania kupunguza gharama za maisha hususani kwa wakazi wa mijini ikiwemo Dar es Salaam.

“Watu wengi hawajui kuwa ukiwa Dar es Salaam hapa ni gharama zaidi  kununua  kuni na mkaa kupikia ni gharama zaidi kuliko kutumia gesi…tumefanya utafiti tumeona watu wote wanaoanza kutumia gesi hawarudi kutumia mkaaa,” amesema Msigwa.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa