Sh25.8 bilioni kusambaza nishati safi ya kupikia taasisi 453 Tanzania Bara

Na Kelvin Makwinya
18 Feb 2026
Makamba atoa wito kwa sekta binafsi katika kuzalisha na kusambaza wa nishati safi ya kupikia ili kuongeza upatikanaji na kupunguza gharama.
article
  • Ni kwa lengo la kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, kulinda mazingira na kuboresha afya ya jamii.
  • Makamba atoa wito kwa sekta binafsi kuchangamkia fursa katika uzalishaji na usambazaji wa nishati safi ya kupikia ili kuongeza upatikanaji na kupunguza gharama kwa wananchi.

Dar es Salaam. Serikali imezindua awamu ya kwanza ya mradi wa kusambaza nishati safi ya kupikia katika taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100, unaolenga kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, kulinda mazingira na kuboresha afya ya jamii.

Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba aliyekuwa akizungumza wakati wa uzinduzi huo Februari 17, 2026 jijini Dodoma, amesema awamu hiyo inahusisha shule 52 za sekondari pamoja na chuo kimoja cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika mikoa 18 iliyopo Tanzania Bara.

“Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata nishati safi, salama, nafuu na rafiki kwa mazingira sambamba na kutimiza malengo ya maendeleo endelevu,” amesema Makamba.

Makamba amesema utekelezaji wa mradi huo unajumuisha usimikaji wa mifumo ya gesi ya LPG, ufungaji wa majiko banifu na usambazaji wa mkaa mbadala katika taasisi 453. 

Ameeleza kuwa gharama zote za utekelezaji zitagharamiwa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), huku mradi huo ukiwa na thamani ya Sh25.8 bilioni.

Mradi huu ulianzishwa kwa lengo la kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, kulinda mazingira na kuboresha afya ya jamii. Picha | Wizara ya Nishati

Kuanzishwa kwa mradi huo ni hatua muhimu katika kupunguza gharama za nishati kwa taasisi za umma, huku ukisaidia kuongeza idadi ya watumaji wa nishati hiyo nchini.

Mwaka 2024 Tanzania ilizindua Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya nishati safi ya Kupikia uliuolenga kuongeza matumizi ya nishati safi nchini hadi asilimia 80 ifikapo mwaka 2034.

Ili kutekeleza mpango huo Serikali ilipiga marufu taasisi za Serikali na binafsi zinazolisha kuanzia watu 100 kutumia nishati zisizo salama kupikia na kuhamia katika nishati safi za kupikia ikiwemo gesi na umeme.

Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati, mpaka kufikia Machi 2025, jumla ya taasisi 762 zilikuwa zimeanza kutumia nishati safi ya kupikia ambapo kati ya hizo taaisisi za umma ni 495 na taasisi binafsi ni 267.

Makamba atoa wito kwa sekta binafsi kuchangamkia fursa katika uzalishaji na usambazaji wa nishati safi ya kupikia ili kuongeza upatikanaji na kupunguza gharama kwa wananchi. Picha | Wizara ya Nishati.

Akisisitiza umuhimu wa uendelevu wa mradi, Makamba amebainisha kuwa awamu ya pili ya mradi huo inatarajiwa kuhusisha taasisi 400 katika mikoa yote nchini, akizitaka ofisi za Serikali kusimamia kikamilifu mifumo hiyo ili ifanye kazi kwa muda mrefu.

“Nitoe wito kwa Serikali za Mitaa, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Tamisemi kusimamia mifumo iliyofungwa ili iwe endelevu suala litakalohamasisha jamii kuiga mfano wa taasisi za umma kuhamia katika nishati safi ya kupikia.” amesema Makamba. 

Aidha, ameitaka sekta binafsi kuona na kuchangamkia fursa iliyopo katika uzalishaji na usambazaji wa nishati safi ya kupikia ili kuongeza upatikanaji na kupunguza gharama kwa wananchi.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa