Vyakula rahisi kupika kwa kutumia pressure cooker 

Na Fatuma Hussein
27 May 2025
Unaweza kupika chakula kigumu kama maharage au nyama kwa dakika chache tu, bila kupoteza ladha au ubora.
article
  • Unaweza kupika vyakula mbalimbali ikiwemo maharage na makande
  • Ni rahisi na hutumia nishati kidogo.

Kuna nyakati muda ni hautoshi lakini unahitaji chakula kitamu, kilichoiva vizuri na chenye virutubisho kamili. Katika mazingira kama hayo, pressure cooker (jiko la umeme la presha) huwa ni mkombozi jikoni. 

Unaweza kupika chakula kigumu kama maharage au nyama kwa dakika chache tu, bila kupoteza ladha au ubora. Hii ni faida kubwa kwa watu wenye shughuli nyingi au familia zenye mahitaji ya mlo wa haraka.


Fahamu vyakula vitano unavyoweza kupika kwa pressure cooker kwa urahisi na haraka. Kama bado hujanunua pressure cooker, basi jikopoint.co.tz utajipatia zenye ubora wa hali ya juu kukidhi mahitaji yako.

Maharage

Maharage ni chakula cha kawaida kinachopendwa na familia nyingi, hasa Afrika Mashariki. Mara nyingi huchelewesha mlo kwa sababu huiva kwa muda mrefu. 

Kwa kutumia pressure cooker, unaweza kuyapika kwa dakika 25–30 badala ya saa nzima. Maharage huiva vizuri na kuwa laini kwa urahisi. Kama unatumia mkaa au kuni basi, kifaa hiki kinaweza kukufaa na kuokoa gharama na muda wako.

Hakuna asiyejua utamu wa maharage na hunoga zaidi iwapo nazi au karanga itakuwa moja ya kiungo. Picha/ Canva.

Pilau

Pilau ni chakula cha sherehe na hufurahisha wengi kutokana na harufu na ladha yake tamu. Kupika pilau kwa pressure cooker husaidia mchele na nyama kuiva sawasawa bila kuungua. Unaweza kupika pilau kwa dakika 10 hadi 12 pekee ukiwa na pressure cooker. 

Ukialikwa harusini au shughuli yoyote ukakosa pilau basi unahisia kama haupo shughulini n ahii ni kulingana na utamu wake.Picha/ Canva.

Viungo kama karafuu na pilipili mtama hutawanyika vizuri kutokana na mvuke wa juu. Hii huufanya mlo huu kuwa wa haraka lakini wa hadhi ya juu.

Viazi vya mchuzi

Viazi vya mchuzi ni rahisi kupika lakini huhitaji usahihi ili visivunjike au kubakia vibichi. 

Pressure cooker huviaacha vikijaa mchuzi ndani kwa ndani, hivyo ni chaguo bora kwa chakula cha jioni chenye haraka lakini kilichoiva vizuri.

Sio mpaka uweke nyama kwenye viazi unaweza kuweka samaki au dagaa nyama. Picha/ canva.

Kwa kutumia pressure cooker, viazi vinaiva ndani ya dakika 5 hadi 8 pekee. 

Supu ya nyama

Supu ni chakula chenye virutubisho vingi, hasa inapopikwa kwa mifupa na nyama. 

Pressure cooker huongeza kasi ya kupata virutubisho kutoka kwenye mifupa huku ikisaidia  nyama kuwa laini kwa bila kuchemka kwa muda mrefu.

Utamu wa supu ya nyama huonekana hasa unapoitumia na chapati pembeni. Picha/canva.

Kwa dakika 30 hadi 40, unaweza kupata supu nzito yenye ladha ya kipekee.

Makande 

Makande ni chakula cha asili chenye virutubisho vya kutosha kwa mwili. Mahindi na maharage yote yanachukua muda mrefu kuiva. 

Kupika makande kwa pressure cooker huokoa muda na huhifadhi ubora wa vyakula hivi. Kwa muda wa dakika 35 hadi 40, unaweza kupata makande laini na yenye ladha nzuri. Pressure cooker ni suluhisho kwa familia zinazotafuta lishe bora na ufanisi jikoni.

Sio lazima kila siku ule makande ya maharage kuna muda unaweza kubadili ladha kw akupika makange ya kunde au choroko. Picha/ canva

Pressure cooker inabaki kuwa mshirika mwaminifu jikoni, ikirahisisha maisha bila kuathiri ubora wa mlo na wakati huo huo kutunza mazingira.

Iwapo umekuwa ukihangaika kupika haraka au kutumia nishati nyingi bila sababu, basi vyakula hivi vitano ni mwanzo mzuri wa kufanya mabadiliko jikoni kwako.

© Copyright 2021 JikoPoint by Nukta Africa